Nenda kwa yaliyomo

Waraka kwa Waroma

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Waraka kwa Warumi)
Mwanzo wa waraka huu katika Codex Alexandrinus.
Agano Jipya

Waraka kwa Waroma ni kitabu kimojawapo cha Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo. Andiko hili ni barua ya Paulo wa Tarso kwa ushirika wa Wakristo katika mji mkuu wa Dola la Roma.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Umuhimu wake

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya maandiko matakatifu ya Agano Jipya na ya Biblia kwa jumla, barua ya Mtume Paulo kwa Wakristo wa Roma ina umuhimu wa pekee uliokusudiwa naye mwenyewe.

Mazingira

[hariri | hariri chanzo]

Paulo alikaa Efeso karibu miaka mitatu, lakini moyo wake wa kimisionari haukutulia kwa sababu alikumbuka alivyotabiriwa atafanya kazi hata mbali zaidi. Ndiyo maana alitaka kwenda Ulaya magharibi, yaani Roma na halafu Hispania, nchi iliyohesabika kuwa mwisho wa dunia. Ila kabla ya kwenda huko alipanga kuwaletea Wakristo wa Yerusalemu mchango wa wenzao wa mataifa.

Basi, mwishoni mwa miezi mitatu aliyokaa Korintho (Mdo 20:2-3) akijiandaa kupanda meli, yaani mwanzoni mwa mwaka 58, Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma ili kuandaa utume atakaoufanya katika jiji hilo.

Huko Ukristo uliingia toka mwanzo kabisa, ukiletwa na baadhi ya Wayahudi wengi walioishi Roma ambao walibatizwa Yerusalemu kwenye Pentekoste ya mwaka 30 (Mdo 2:1-12).

Wayahudi wote walipofukuzwa na Kaisari Klaudio (49), Wakristo wa mataifa mengine wakabaki ndio wengi, nao wakaachana na masharti mbalimbali za dini ya Kiyahudi, kama yale kuhusu vyakula.

Muda mfupi baada ya Klaudio kufa (54), Wayahudi walianza kurudi, kumbe wale ambao kati yao walikuwa wamemuamini Yesu wakakuta mabadiliko hayo makubwa ndani ya Kanisa, nao wakajiona wamewekwa pembeni kidogo, kama si kudharauliwa na Wakristo wa mataifa.

Mtume Paulo akijua umuhimu wa Roma, mji mkuu wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa huko barua ndefu tena nzito kuliko zote. Alitaka kuwaeleza kwa maandishi ya mpango mafundisho yake kuhusu wokovu, kwa sababu walikuwa wamesikia habari tofautitofauti juu yake bila ya kukutana naye.

Pamoja na kuwaandaa hivyo wampokee vizuri, alichukua nafasi ya kuimarisha umoja wao ulioingia dosari.

Akiandika kwa utulivu mkubwa kuhusu mambo aliyokwishawaongelea kwa hasira Wagalatia, Paulo aliweza kuinua pande zote mbili za Kanisa hilo zielewe zaidi fumbo la mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wote, na hivyo ziheshimiane kwa upendo, ulio utimilifu wa Torati.

Hasa aliwaonya Wakristo wa mataifa wasidharau Wayahudi, kwa sababu hao bado ni wateule wa Mungu.

Mpangilio na mada

[hariri | hariri chanzo]

Ingawa haina mafundisho yote ya Paulo, barua hii imechangia teolojia ya Kikristo kwa kiasi kikubwa, hasa upande wa magharibi.

Kwa namna ya pekee inajibu kinaganaga maswali kuhusu wokovu: unapatikana kwa njia gani? Kwa nini Wayahudi wengi walishindwa kumuamini Yesu ili kuupata? Kwa nini mataifa yameupokea badala yao? Aliyepata wokovu anaishi vipi? Je, Wayahudi wametupwa moja kwa moja?

Ndiyo sehemu kuu ya barua (Rom 1:16-32; 2:1-29; 3:9-20; 3:21-31; 4:1-8; 4:23-25; 5:1-21; 6:1-14; 7:7-25; 8:1-39; 9:1-5; 11:1-36), ambayo inafuata salamu (1:1-8) na shukrani.

Paulo alisisitiza kwamba wote ni wakosefu na wanaweza kuokolewa na Mungu tu: hiyo ni neema tupu, maana hakuna anayeweza kuistahili kwa juhudi zake.

Neema hiyo tunaipata kwa kumuamini Yesu ambaye alikufa akafufuka kwa ajili yetu ili sisi tuishi upya kwa ajili yake tukiongozwa na Roho Mtakatifu.

Chini yake Mkristo atafanya mema mengi na makubwa kuliko yale yanayodaiwa na Torati, ambayo ni njema lakini haitutii nguvu ya kuitekeleza.

Upande wa mataifa, toka mwanzo Mungu aliwapa mwongozo mwingine wa maisha, yaani dhamiri.

Hata hivyo pande zote mbili zilishindwa kufaidika na miongozo hiyo wakahitaji msaada bora zaidi ili kumpendeza Mungu.

Uadilifu sasa unapatikana kwa imani na ubatizo katika kifo na ufufuko wa Yesu.

Hiyo njia mpya ya Mungu kuwaokoa watu wote haiendi kinyume cha ahadi zake kwa Israeli ya Kale. Paulo anathibitisha hilo kwa hatua nne akitumia madondoo mengi ya Agano la Kale. Hamzungumzii Myahudi mmojammoja, bali wote jumla; wala hazungumzii jukumu lao kuhusu kifo cha Yesu.

Maadili mema yatafuata kama matunda, na Paulo, kama kawaida ya Wakristo wa kwanza, baada ya ujumbe au fundisho la imani, anayaeleza hasa katika sehemu ya pili ambayo ina mawaidha mbalimbali (Rom 12:1-2,9-21; 13:8-14), yakifuatwa na taarifa, salamu na doksolojia.

Kwa kuwa Paulo hakuwafahamu vizuri Wakristo wa Roma, maneno yake ni ya jumla na si ya kinaganaga. Hasa ni kwamba madai ya Torati hayawezi kuongoza mwenendo wa Mkristo, lakini huyo anatakiwa kuzingatia anavyodaiwa hasa upendo kwa wote.

Maisha ya Mkristo yawe ibada kwa Mungu katika Roho Mtakatifu. Umoja wa Kanisa unamdai ajitahidi kushinda mabaya kwa mema. Kila kiungo cha mwili huo mmoja anadaiwa juhudi kwa ajili ya ustawi wa wote ili maisha yawe sadaka kwa Mungu.

Akigusa zaidi maisha ya Kanisa la Roma ya wakati huo, yaliyovurugwa na masuala madogomadogo kuhusu vyakula na sikukuu, Paulo alidai wenye nguvu watekeleze upendo kwa walio dhaifu zaidi, pamoja na busara, uelewa, mfano wa Yesu na uaminifu kwake.

Maelekezo hayo yanaweza kusaidia daima kukabili mvutano wowote kati ya wenye mitazamo tofauti (finyu na mpana, au wa kizamani na wa kisasa zaidi). Lengo ni ule umoja uliofundishwa katika sura nane za kwanza.

  • Bruce, F. F. (1983). The Epistle of Paul to the Romans: An Introduction and Commentary. Tyndale New Testament Commentaries. Leicester, England: Inter-Varsity Press. ISBN 0851118550.
  • Dunn, J. D. G. (1988b). Romans 9–16. Word Bible Commentary. Dallas, Texas: Word Books, Publisher.
  • Fitzmyer, J. A. (1992). Romans. Anchor Bible Commentary. New York: Doubleday.
  • Dunn, J. D. G. (1988a). Romans 1–8. Word Bible Commentary. Dallas, Texas: Word Books, Publisher.
  • Rutherford, Graeme (1993). The Heart of Christianity: Romans [chapters] 1 to 8. Second ed. Oxford, Eng.: Bible Reading Fellowship. 248 p. ISBN 0-7459-2810-2
  • Stuhlmacher, Peter (1994). Paul's Letter to the Romans: A Commentary. Westminster: John Knox Press. ISBN 0-664-25287-7.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]

Tafsiri ya Kiswahili

[hariri | hariri chanzo]
  • [1] Agano Jipya kwa lugha ya Kiswahili.

Tafsiri nyingine

[hariri | hariri chanzo]

Ufafanuzi

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya Agano Jipya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Waraka kwa Waroma kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy