Kitabu cha Yoshua ni cha sita kati ya vitabu vya Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na vya Agano la Kale katika Biblia ya Ukristo.

Yoshua akiagiza jua lisimame juu ya bonde la Gibeon alivyochorwa na John Martin.

Kitabu hicho chenye sura 24 kinatupasha habari za uvamizi wa nchi takatifu ambao Waisraeli waliufanya chini ya Yoshua, ambaye ni mfano wa Yesu (hata jina lao kwa Kiyahudi ni moja, linalotafsiriwa “Mungu anaokoa”): ndiye aliyewaingiza watu katika nchi ya ahadi, si Musa.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Mazingira

hariri

Kitabu cha Yoshua kinahusika zaidi na Waisraeli walipoteka nchi ya Kanaani na nchi hiyo ilivyogawiwa kati ya makabila yake 12.

Tangu wakati wa Ibrahimu, Mungu alikuwa ameahidi kwamba Kanaani ingekuwa mali ya Waisraeli (Mwa 13:14-17), lakini karne kadhaa zilipita mpaka Waisraeli walipokuwa taifa kubwa la kutosha kwa kuteka na kumiliki nchi hiyo.

Taifa la Israeli lilikua na kuongezeka hasa katika nchi ya Misri, na wakati ulipowadia, Musa aliwaongoza watu hao kutoka Misri kuelekea Kanaani (Kut 3:7-10; 12:40-41). Lakini watu walipofika karibu, ambapo wangeweza kuandaa mashambulio, waliwaogopa Wakanaani wakamwasi Mungu. Kwa ukaidi wao, watu walikataa kumtegemea Mungu na kuingia Kanaani, isipokuwa viongozi wawili, yaani Yoshua na Kalebu. Mungu akawaadhibu jangwani mpaka walipokufa watu wazima wote (waliokuwa na miaka 20 na kuzidi, isipokuwa Yoshua na Kalebu) na kizazi kipya kilipokuwa na nguvu ya kutosha (Hes 14:28-35).

Wakati huo, miaka 40 baada ya wazazi wao kuondoka Misri, watu wa kizazi kile kipya walikuwa tayari kuingia Kanaani. Kambi yao kubwa ilikuwa mashariki mwa Mto Yordani kukabili Yeriko (Hes 22:1). Musa alikuwa amekufa tangu muda mfupi (Kumb 34:1-5), na Yoshua alipewa jukumu la kuwaongoza Waisraeli baada ya kifo cha Musa kwenye miaka 1210-1200 hivi KK (Kum 34:9; Yos 1:1-2).

Kiongozi mpya wa Israeli

hariri

Yoshua alizaliwa na kukulia Misri, lakini miaka ya taabu huko ilimsaidia kujenga tabia, uwezo na imani ya kumtegemea Mungu ambayo siku moja itamfanya awe mtu wa maana sana katika taifa lake.

Muda mfupi baada ya Waisraeli kuondoka Misri, Yoshua alionyesha uwezo wake wa kuongoza alipokusanya kwa haraka sana jeshi dogo na kuwafukuza wachokozi Waamaleki (Kut 17:8-16).

Waisraeli walipofika Mlima Sinai, Yoshua alikuwa msaidizi maalumu wa Musa. Yeye peke yake alifuatana naye alipokwea mlima, ambapo Musa alikutana na Mungu katika wingu, lakini Yoshua alibaki nje (Kut 24:13).

Vile vile Yoshua hakutoka katika hema ambamo Musa alikutana na Mungu (Kut 33:11; taz. Hes 11:28).

Siku moja, Waisraeli walipomwasi Mungu jangwani, Yoshua alionyesha imani yake yenye ujasiri ambapo yeye na Kalebu walisimama imara kinyume cha wenzao wote (Hes 14:9).

Imani yake ya kumtegemea Mungu ilimpa uvumilivu na kumlinda asije akachukuliwa na tamaa ya ubinafsi ya kutaka makuu. Hakuwa na kijicho dhidi ya Musa kuwa kiongozi wa Israeli, bali alijaribu kumtetea watu wengine walipojaribu kushambulia daraja yake ya pekee (Hes 11:26-30).

Mungu alimchagua Yoshua awe kiongozi wa taifa baada ya Musa, lakini alionyesha wazi kwamba Yoshua asingekuwa na mamlaka kubwa sawa sawa na Musa, kwa kuwa baada ya kufa kwake, uongozi wa kiraia na ule wa kiroho ukawa juu ya watu tofauti. Tangu wakati huo kawaida ilikuwa kwamba, kiongozi wa kiraia alipata maagizo ya Mungu kwa njia ya kuhani mkuu (Hes 27:18-23).

Hata hivyo, Yoshua alikuwa mtu aliyemwelewa Mungu. Uzoefu wake kama kiongozi wa kiroho, mtawala wa kiraia na mkuu wa jeshi ulimfaa sana kuwaongoza Waisraeli katika nchi yao mpya na katika wakati mpya uliowakabili (Kumb 31:7, 14, 23; 34:9).

Mtindo wa Kitabu cha Yoshua

hariri

Kitabu cha Yoshua kimepata jina lake kutokana na mtu ambaye habari zake zimesimuliwa zaidi humo, lakini hakimtaji mwandishi wake.

Inawezekana kwamba mwandishi alipata habari kutokana na kumbukumbu ambazo Yoshua mwenyewe aliziandika (Yos 24:25-26) na vitabu vingine vya historia vya wakati ule (Yos 10:13) na ripoti za kikabila na za kitaifa kuhusu mahali, koo na matukio mbalimbali (Yos 18:8-9).

Ingawa kitabu kinaeleza utekaji wa nchi ya Kanaani, hakitoi orodha ya kinaganaga kuhusu matukio yote ya historia. Vita vya kuteka Kanaani vilichukua muda mrefu (Yos 11:18) usiopungua miaka mitano (Yos 14:7, 10), lakini mwandishi alitaja baadhi ya vita virefu katika mistari michache tu, na mambo mengine yasiyokuwa na maana sana ya kivita aliyaandika kirefu.

Sababu ya tofauti hizo katika masimulizi ni kwamba, madhumuni maalumu ya mwandishi hayakuwa kuandika kinaganaga kuhusu vita na siasa, bali alitaka kuonyesha kazi ya Mungu na watu wake. Mwandishi alikuwa mhubiri kuliko mwandishi wa ripoti na orodha mbalimbali tu. Alikuwa nabii kuliko mwandishi wa historia.

Kwa Waisraeli kazi ya kwanza ya nabii haikuwa kutabiri mambo ya usoni, bali kuwajulisha watu mapenzi ya Mungu (Isa 1:18-20; Yer 1:7,9; Amo 3:7-8; taz. Kut 4:10-16; 7:1-2). Wao waliona historia yao kama ufunuo wa matendo ya Mungu, na kwa sababu hiyo kitabu hiki na vingine kadhaa vya Biblia tunavyoviona vya historia, Waisraeli waliviita vya unabii. Waandishi wengi wa historia katika Israeli walikuwa manabii (1 Nya 29:29; 2 Nya 9:29; 12:15).

Waisraeli waligawanya vitabu vyao vya unabii katika sehemu mbili zilizoitwa Vitabu vya Unabii wa Awali (Yoshua, Waamuzi, Samweli na Vitabu vya Wafalme), na Vitabu vya Unabii wa Baadaye (kitabu cha Isaya, kitabu cha Yeremia, kitabu cha Ezekieli na vitabu 12 vya manabii wadogo). Katika vitabu vya Unabii wa Awali, Mungu alidhihirisha makusudi yake kwa njia ya historia ya Waisraeli, na kwa kweli mataifa yote yalikuwa chini ya utawala wake mkuu. Katika vitabu vya Unabii wa Baadaye, Mungu alidhihirisha makusudi yake zaidi kwa njia ya maneno ya wasemaji wake.

Kwa sababu ya namna hiyo ya pekee ya Waisraeli kutazama historia, mwandishi wa kitabu cha Yoshua hakujaribu kuorodhesha kila tukio lililotokea wakati ule, wala hakuandika katika utaratibu maalumu wa mfululizo wa matukio. Zaidi alichagua na kupanga mambo yake kadiri ya kusudi lake kuu la unabii. Alitaka kuwasaidia watu wamjue Mungu zaidi, akishughulika na matukio yale yaliyokuwa na maana kubwa katika uhusiano wa taifa na Mungu wake.

Habari za kitabu chenyewe

hariri

Mara baada ya kushika uongozi, Yoshua alituma wapelelezi nchini; huko Yeriko, mji wa zamani kuliko yote ya dunia, walisaidiwa na Rahabu, kahaba aliyeamini kuwa ushindi utakuwa wa Mungu wa Israeli (Yos 2): kwa hiyo akaokolewa pamoja na ndugu zake, tena akajaliwa kuwa bibi wa babu wa mfalme Daudi, hata akatajwa na Injili kama bibi wa Yesu Kristo (Math 1:5-6), halafu akachukuliwa kama mfano wa imani (Eb 11:31) na wa matendo mema (Yak 2:25).

Kadiri ya kitabu hicho, Yoshua aliwavusha Waisraeli pakavu kati ya mto wa Yordani (Yos 3-4) na hivyo akawaingiza katika nchi takatifu. Hapo ikawabidi kwanza wafunge tena agano na Mungu kwa kutahiriwa wanaume wote na kwa kuadhimisha Pasaka ambapo kwa mara ya kwanza walikula mazao ya nchi hiyo waliyoahidiwa: ndio mwisho wa mana na wa kipindi cha jangwani (Yos 5:1-12). Hata sisi tutaacha kula mkate toka mbinguni tutakapoingia pale tulipoahidiwa.

Baada ya matendo hayo ya kidini Mungu alimtokea Yoshua kama amiri jeshi wa Israeli ili kumhakikishia kwamba mwenyewe ataongoza mambo, hivyo Yoshua amtegemee akijisikia chombo chake tu (Yos 5:13-15). Ni rahisi kwa kila binadamu aliyeshika uongozi kujisikia mwenyewe na hivyo kuacha kumtegemea Mungu. Kumbe Yoshua kwa kupokea ujumbe huo akaweza kushinda watu wenye maboma, nguvu na silaha kali kuliko Waisraeli.

Kwamba hiyo ni nguvu ya Mungu inaonekana wazi hasa katika simulizi la kuteka Yeriko (Yos 6:1-21): huko Waisraeli walifanya maandamano ya ibada mpaka kuta za mji zikaanguka. Vita vyetu vya kiroho na vya kitume vitegemee hasa sala.

Baada ya vita vingi Yoshua akayagawia makabila 12 ya Israeli nchi yote, ikiwa ni pamoja na sehemu zilizobaki chini ya wenyeji (Yos 12:1-13:14).

Huko Shekemu aliwadai wote wachague kumtumikia YHWH au miungu mingine, akisisitiza ugumu wa kumtumikia sawasawa Mungu aliye mtakatifu na mwenye wivu kwa watu wake. Lakini wao walikubali kwa moyo wote kumtumikia Mungu tu, wakasimamisha jiwe kubwa kama kumbukumbu (Yos 24:1-28).

Kabla hajafa Yoshua akawaita Waisraeli wote ili kuwaimarisha katika imani na umoja kwa kuwakumbusha maajabu waliyotendewa na Mungu na kwa kuwahimiza wamuonyeshe shukrani (Yos 23). Kukumbuka ni jambo muhimu ili tuishi kwa imani bila ya kudanganywa na maisha yanayosahaulisha kwa urahisi mambo ya Kimungu.

Muhtasari

hariri

1:1-5:15 Kuingia Kanaani

6:1-12:24 Kuteka nchi

13:1-22:34 Kugawanya nchi

23:1-24:33 Yoshua anaaga

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Yoshua kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy