Upendo ni neno linalotumika kwa maana mbalimbali kuanzia hali ya nafsi ya binadamu hadi kwa Mungu. Linatokana na kitenzi "kupenda" na kufanana na pendo, mapendo, mapenzi, n.k.

Giotto, Upendo, Padua, Italia.
Maadili ya Kimungu

Wamisionari wa Upendo, shirika la kitawa la Kanisa Katoliki lililoanzishwa na Mama Teresa huko Kolkata, India, ili kusaidia watu walio fukara zaidi.
Sehemu ya mfululizo wa makala kuhusu mapendo

Moyo katika mapokeo ya Ulaya
ni mchoro unaowakilisha mapendo.
Vipengele Msingi
Mapendo kadiri ya sayansi
Mapendo kadiri ya utamaduni
Upendo (fadhila)
Upendo safi
Kihistoria
Mapendo ya kiuchumba
Mapendo ya kidini
Aina za hisia
Mapendo ya kiashiki
Mapendo ya kitaamuli
Mapendo ya kifamilia
Mapendo ya kimahaba
Tazama pia
Mafungamano ya binadamu
Jinsia
Tendo la ndoa
Maradhi ya zinaa
Siku ya wapendanao

Hapa linatumika kwa maana ya juu zaidi kulingana na Kigiriki "agape" na Kilatini "caritas".

Katika Ukristo

hariri

Kufuatana na Maandiko Matakatifu, hasa ya Mtume Paulo, katika teolojia ya Ukristo ni mojawapo kati ya maadili ya Kimungu, pamoja na imani na tumaini.

Kadiri ya dini hiyo, inatupasa tumpende Mungu pekee, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, kadiri tunavyoweza, kwa kuwa ndiye asili ya uhai wetu na ya wema wote. “Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote” (Kumb 6:4). “Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu” (Mk 10:18).

Halafu tupende viumbe vya Mungu pia kadiri anavyotaka tuwapende kwa kuwa mwenyewe anawapenda. “Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba” (Hek 11:24). “Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana... Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu’, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye: ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake” (1Yoh 4:11,20-21)[1].

Kielelezo bora cha upendo ni Yesu Kristo, aliyefikia hatua ya kujitoa kafara kwa ajili yetu na kutuombea sisi wakosefu tuliomtesa. “Ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Rom 5:7-8). “Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:15). “Muenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yenu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato” (Ef 5:2). “Katika hili tumelifahamu pendo: kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” (1Yoh 3:16).

Lakini tusimfuate Yesu kama kielelezo tu, bali tuishi ndani yake na kwa ajili yake, kwa kuwa ndiye uhai wetu. “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, kadhalika nabyi, msipokaa ndani yangu” (Yoh 15:4). “Alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao” (2Kor 5:15). “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu” (Kol 3:3-4).

Kadiri ya madhehebu kadhaa, tunaweza kufuata mfano wa watu wengine kadiri walivyomfuata Yesu. Ndio wale tunaowaita watakatifu, kwa kuwa Kanisa limewaweka mbele yetu kama kielelezo wazi cha upendo kamili. “Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate” (2Thes 3:9). “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo” (1Kor 11:1). “Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi... Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo” (Fil 3:17; 4:9).

Upendo wa Mungu si hisia ya moyo, inayoweza kubadilikabadilika, bali ni msimamo wa dhati unaojitokeza katika matendo. “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yoh 3:17-18).

Basi, huo upendo ambao tumpende Mungu na viumbe vyake si pendo la kibinadamu tu, bali ni uleule ambao mwenyewe anajipenda, anatupenda na kutushirikisha, yaani ni Roho Mtakatifu. “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5). “Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu... Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake... Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza” (1Yoh 4:7,16,19).

Tunaweza kuwa na kiasi chochote cha upendo huo wa Kimungu, lakini tuwe daima tayari kuupokea upya na kuutekeleza uzidi kustawi bila mwisho. “Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote” (1Thes 3:12). “Pendo lenu lizidi kuwa jingi sana” (Fil 1:9).

Upendo unatakiwa kustawi zaidi na zaidi bila mwisho, kwa kuwa ndio mfumo wake. Upendo wa kweli haufuati kipimo: kiasi cha kupenda ni kupenda bila kiasi. “Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk 6:36). “Kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo” (Yoh 13:1).

Upendo utakamilika mbinguni, ambapo tutamuona Mungu alivyo na kuvutiwa naye tusiweze kubandukana naye milele. “Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika... Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” (1Kor 13:8,12). “Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:3).

Hivyo Ukristo unatuelekeza kuona maisha haya kama safari ya kulenga upendo kamili, ambapo Roho Mtakatifu anatunasukuma tusonge mbele kwa hatua za upendo mkubwa zaidi na zaidi. “Nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu, katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo” (Fil 3:13-16).

Utekelezaji wa upendo unadai uendane na maadili mengine yote, la sivyo si wenyewe; sanasana ni pendo la kibinadamu tu lisilopatana na Mungu. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote; hutumaini yote, hustahimili yote” (1Kor 13:4-7). “Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu” (Math 6:2).

Maadili mengine yasipoendana na upendo, huwa yamekufa, kwa kuwa upendo ndio uhai wa hayo yote. “Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je, ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, ‘Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba’, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake” (Yak 2:14-17). “Nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu” (1Kor 13:3).

Maadili yanayoendana na upendo ni hasa imani na tumaini. “Hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu” (1Thes 1:3). “Sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu” (1Thes 5:8). “Sikuzote tukiwaombea, tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote, kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni” (Kol 1:3-5). “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo” (1Kor 13:13).

Hayo matatu yanaitwa maadili ya Kimungu kwa kuwa asili na lengo lake ni Mungu mwenyewe. Hatuwezi kujipatia hayo, bali tunamiminiwa naye kwa pamoja tuweze kumsadiki, kumtumaini na kumpenda inavyotupasa tuwe marafiki wake. “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef 2:8). “Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana” (1Thes 4:9).

Pamoja na imani na tumaini, upendo unadai maadili ya kiutu, ambayo yote yanategemea manne ya msingi: busara, haki, nguvu na kiasi. “Huwafundisha watu kiasi, na ufahamu, na haki, na ushujaa; wala hakuna mambo ya kuwafaa zaidi kwa maisha” (Hek 8:7).

Ustawi wa upendo kadiri ya Kanisa Katoliki

hariri

Kwa imani ya Kanisa Katoliki, hakuna wokovu wa binadamu bila huyo kuwa na upendo[2]. Adili hilo la Kimungu, lililo kuu kuliko yote[3] na linalotakiwa kuyaongoza na kuyahuisha mengine pia, halitakiwi kubaki lilivyo, bali kukua ndani mwetu hadi siku ya kufa.

Fundisho hilo linaweza, tena linapaswa kuangaza maisha ya Kiroho, kwa sababu ni msingi wa himizo lolote la kusonga mbele kwa unyenyekevu na moyo mkuu, kwa kutamani muungano wa dhati na Mungu, kwa kujitahidi kuupata pamoja na kuuomba. Basi, tuone kwanza kwa nini upendo unatakiwa kustawi daima, halafu jinsi unavyostawi.

Kwa nini upendo unatakiwa kustawi hadi kufa

hariri

Hata katika kiwango kidogo upendo halisi (ambao tuliupokea kwa ubatizo na kurudishiwa pengine kwa upatanisho) unampenda tayari Mungu Mwokozi kuliko yote, na kwa ajili yake unampenda jirani kama mtu mwenyewe anavyojipenda. Kiwango hicho cha upendo uliomiminwa rohoni kinapita bila kifani pendo la kimaumbile tunaloweza kuwa nalo kwa Muumba na kwa watu; hakimbagui yeyote, kwa kuwa ubaguzi huo ungekuwa dhambi ya mauti inayofuta upendo. Lakini upendo huo wa wanaoanza uko mbali na ushindi dhidi ya umimi wowote. Unaendana bado na kujipendea ambako kunasababisha si dhambi ya mauti, bali dhambi nyepesi nyingi na hivyo kunazuia upendo usiweze kutenda na kupamba vizuri.

Ni wazi kuwa upendo huo unatakiwa kustawi: “Hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana” (Fil 1:9). “Bwana awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu” (1Thes 3:12-13). “Mwenye haki na azidi kufanya haki, na mtakatifu azidi kutakaswa” (Ufu 22:11). “Njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu” (Mith 4:18). Hapa duniani Mkristo ni msafiri anayemuelekea Mungu na kumkaribia kwa vitendo vya upendo kamili zaidi na zaidi, kwa “hatua za upendo” (Gregori Mkuu). Upendo wake unaweza na kupaswa kustawi mfululizo, la sivyo badala ya kusafiri atasimama kabla hajafika. Lengo la njia ni kutembea, si kulala.

Kila mtu anayeelekea uzima wa milele anatakiwa kukua katika upendo ili azidi kumkaribia Mungu: si tu wanaoanza na wanaoendelea, bali hata waliokamilika. Tena hao wa mwisho wanapaswa kwenda kasi zaidi kadiri wanavyomkaribia na kuvutwa naye. Nguvu ya maisha yao ya Kiroho inaongezeka zaidi na zaidi, elekeo la roho yao linainuka zaidi na zaidi; kwao hakuna machweo: mwili tu unadhoofika kwa uzee.

Bwana alisema, “Mimi nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu” (Yoh 12:32). “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka” (Yoh 6:44). Mungu ndiye anayetufanya twende, anakotuvutia ni kwake: ndiye mwanzo na mwisho wa yote, ndiye wema mkuu unaovuta upendo kwa nguvu kadiri tunavyomkaribia. Ndiyo sababu katika maisha ya watakatifu, ustawi wa upendo miaka yao ya mwisho ni mkubwa sana; ingawa wanalemewa na uzee na udhaifu upande wa hisi (k.mf. kumbukumbu) wanang’amua ukweli wa maneno, “Ujana wako unarejezwa kama tai” (Zab 103:5). Maendeleo hayo ya kasi zaidi na zaidi yalikuwepo hasa katika bikira Maria, kwa kuwa ndani mwake hayakuzuiwa na chochote, tena yalikuwa ya haraka kadiri ilivyokuwa kubwa neema ya kwanza aliyojaliwa. Basi, upendo hautakiwi tu kustawi hadi kufa, bali kustawi zaidi na zaidi, kama vile kasi ya kitu kinachoanguka inavyozidi hadi kikafika ardhini.

Ikiwa ni hivyo, upendo unastawi vipi ndani mwetu? Kwa kuwa hata katika kiwango cha chini unampenda tayari Mungu na majirani wote, hauwezi kuenea zaidi: lakini unaweza kuongezewa nguvu na kutia mizizi ndani ya utashi wetu zaidi na zaidi. Upendo hauongezeki kwa wingi kama nafaka, bali unakua kwa ubora, kwa kuongezewa nguvu katika utashi, ukizidi kuuelekezea mema yapitayo maumbile na kuuepusha na maovu. Mfano wake ni elimu ya msomi ambayo haipati daima taarifa mpya, ila inazidi kuzichimba na kuwa na hakika nazo; vivyo hivyo upendo unastawi ndani mwetu, ukitufanya tuwapende kwa namna kamili na safi zaidi na zaidi Mungu kwa ajili yake mwenyewe na jirani kwa ajili ya Mungu. Tukielewa hayo, tutaona haja ya kutakaswa kila uchafu ili kudhihirisha jinsi maadili makuu yanavyolenga ukweli na wema wa Mungu. Basi, upendo kama joto, unastawi kwa ubora, kwa kupata nguvu zaidi na zaidi; na hiyo inafanyika kwa namna tatu: kwa stahili, kwa sala na kwa sakramenti.

Ustawi wa upendo kwa njia ya stahili zetu

hariri

Tendo linalotokana na upendo (au adili lolote linalohuishwa nao) linastahili tuzo lipitalo maumbile, hasa ustawi wa upendo wenyewe. Stahili hazisababishi ustawi huo, kwa kuwa upendo si adili la kujipatia, bali la kumiminiwa, yaani Mungu tu anaweza kuutia ndani mwetu (kwa sababu ni kushiriki uzima wake wa ndani), naye tu anaweza kuustawisha: “Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye… ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu” (1Kor 3:6-9). Yeye “atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu” (2Kor 9:10). Ingawa matendo ya upendo hayawezi kusababisha ustawi wa adili hilo, yanauchangia kwa namna mbili, yaani kwa kuustahili na kwa kutuandaa tuupokee.

Stahili ni haki ya kupata tuzo; haiisababishi ila inaipata. Mwadilifu akitenda mema yapitayo maumbile anastahili upendo wake ustawi. Bwana kabla hajampa tuzo ya mbinguni anampa ile ya kukua katika upendo wake. Wazushi walioitwa Watulivu walidharau tuzo wakijidai eti! Hawajitafutii faida. Kumbe kadiri mtu alivyo na upendo, anatamani tuzo hiyo: kumpenda Mungu kwa nguvu na usafi mkubwa zaidi na zaidi, jambo lisilotenganika na ustawi wa maadili mengine ya kumiminiwa na wa vipaji vya Roho Mtakatifu.

Matendo ya upendo (na ya maadili yanayohuishwa nao) hayastahili tu ustawi huo, bali pia yanaandaa kuupokea, kama kwa kufungua na kupanua akili na utashi ili uzima wa Mungu uweze kuvipenya zaidi, na kwa kuvitakasa uviinue juu zaidi. Hiyo ni kweli hasa kwa matendo motomoto ya upendo. Tendo moja la namna hiyo linaathiri pengine maisha yote ya baadaye na kustahili ustawi mkubwa wa upendo, likituandaa kuupokea. Ni kama kuinuliwa hadi ghorofa ya juu, tunapopewa mtazamo mpya wa mambo ya Mungu na kuvutiwa nayo zaidi. Tunaongezewa talanta, yaani Roho Mtakatifu anakuwemo ndani mwetu kwa namna mpya inayotenda zaidi.

Kwa kawaida yeye anamsukuma mtu kulingana na kiwango cha maadili na vipaji alichonacho au kulingana na usikivu wake. Kama angemsukuma atende kwa upungufu, angekuwa amempa bure kiwango kikubwa cha maadili na vipaji. Basi, mwadilifu asipozuia kazi ya Mungu, atapokea neema kubwa zaidi na zaidi apande mbio kwake.

Wanateolojia kadhaa wamefundisha kuwa Mungu anatukuzwa na tendo moja la upendo la talanta kumi kuliko anavyotukuzwa na vitendo kumi vya upendo vya talanta mojamoja; vilevile mwadilifu kamili mmoja anampendeza kuliko wengine wengi wanaobaki katika wastani. Ubora ni muhimu kuliko wingi. Ndiyo sababu ukamilifu wa Bikira Maria unapita ule wa watakatifu wote, kama vile almasi moja ilivyo na thamani kuliko vito vingine vingi.

Basi, upendo unatakiwa kustawi kwa njia ya stahili zetu hadi siku ya kufa. Pamoja nao utakua pia utayari wetu wa kupokea ongezeko lingine. Moyo unapanuka zaidi na zaidi na ujazo wake wa Kimungu unaongezeka: “mioyo yetu imekunjuliwa… Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa… nanyi pia mkunjuliwe mioyo” (2Kor 6:11,13).

Mara nyingi tunasahau tuko safarini kuelekea uzima wa milele, na tunajaribu kustarehe katika maisha haya kana kwamba yangedumu moja kwa moja. Mfano wake ni maabiria wa treni bora ambamo wanakula na kulala kama hotelini hata wakasahau wako safarini; pengine wakiangalia dirishani wanaona mandhari ikibadilika haraka na baadhi ya wenzao wakiteremka: hapo wanajisemea kuwa wao pia watawahi kufikia mwisho wa safari. Shida ni kwamba, ingawa tunaona wengi kufa, hatupati hakika ya ndani kuwa siku fulani itakuwa zamu yetu.

Basi, tunatakiwa kuishi kwa kukazia macho mwisho wa safari, kusudi tusipoteze tena muda tuliojaliwa, bali tuujaze iwezekanavyo matendo ya kustahili uzima wa milele.

Ustawi wa upendo kwa njia ya sala

hariri

Ustawi wa upendo (pamoja na maadili mengine na vipaji) unapatikana si kwa njia ya stahili tu, bali kwa sala pia, kama Kanisa linavyoomba, “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuzidishie imani, tumaini na upendo” (Jumapili ya 30 ya mwaka).

Tukumbuke tofauti iliyopo kati ya kuomba na kustahili: asiye na neema inayotia utakatifu hawezi kustahili (kwa kuwa neema hiyo ndiyo asili ya stahili yoyote ipitayo maumbile); lakini kwa neema ya msaada anaweza kujiombea (k.mf. neema ya uongofu) na akiomba kwa unyenyekevu, imani na udumifu, atapata. Stahili inahusu haki ya Mungu; kumbe sala inaelekea huruma ya Mungu ambayo mara nyingi inanyanyua walioanguka na kusikiliza ombi lao lisilostahili chochote. Mtu duni kuliko wote, aliyetumbukia vilindi asimoweza kustahili tena, anaweza kulilia huruma hiyo: “Kilindi chapigia kelele kilindi” (Zab 42:7), yaani kilindi cha unyonge kinalilia kile cha huruma. Mkosefu akisihi kwa moyo wote anasikilizwa, roho yake inainuliwa, na Mungu anatukuzwa. Nguvu ya sala haitegemei tu neema inayotia utakatifu iliyo ya lazima ili kustahili.

Tukishaongoka, tunaweza kustawishiwa uzima wa neema kwa stahili na kwa sala pia. Hiyo ikiwa na unyenyekevu, imani na udumifu, inatupatia ustawi wa maadili ya Kimungu tunaoomba katika maombi matatu ya kwanza ya Baba Yetu. Sala ya mwadilifu, anayependa kutafakari polepole na kujilisha kwa undani maombi hayo (hata kusimama pengine nusu saa kuzamia mojawapo kwa upendo), inastahili pamoja na kuomba neema: inampa haki ya kustawishiwa upendo ulioisababisha, na kwa nguvu ya ombi inapata kuliko inavyostahili. Tena, ikiwa motomoto kweli, inapata mara. Hapo tunaweza kuona matunda ya sala na jinsi inavyomvuta Mungu ajitoe kwetu kwa dhati, nasi tujitoe kwake. Hapo moyo unazidi kutanuka upokee neema kwa wingi zaidi; roho inajitenga na malimwengu na kumtamani zaidi Mungu, ambaye ndani yake inakuta yale yote yanayostahili kupendwa, tena kwa ngazi ya juu. Hakutatosha kamwe kuyaishi hayo katika sala ya moyo, k.mf. katika kimya kikubwa cha usiku, ambapo mtu yuko peke yake na Muumba na Mwokozi wake. Hapo anang’amua kuwa Mungu ni mwema kupita kiasi, na sala ni mwanzo wa uzima wa milele.

Kwa kusali mwadilifu anaweza kupata neema kadhaa asizoweza kustahili, hasa ile ya kudumu mpaka mwisho. Hawezi kustahili zawadi hiyo kwa sababu ni kudumu kwa hali ya neema iliyo chanzo kisichostahilika cha stahili. Lakini kifo chema kinapatikana kwa sala nyenyekevu, yenye imani, ya kila siku. Kanisa Katoliki linatualika kukariri kwa bidii, “Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina”. Vivyo hivyo tunaweza kumuomba Mungu neema ya kumjua kwa ndani zaidi na zaidi, yaani ya kuzama katika sala, ambayo matokeo yake ni kuungana naye kwa namna imara na yenye matunda mengi zaidi: “Neno moja nimelitaka kwa Bwana, nalo ndilo nitakalolitafuta: nikae nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa Bwana na kutafakari hekaluni mwake” (Zab 27:4), yaani nione kila siku vizuri zaidi jinsi wema wake usivyo na mipaka kwa wale ambao wanamtafuta na kumpata.

Ustawi wa upendo kwa njia ya sakramenti

hariri

Hatimaye upendo (pamoja na maadili mengine na vipaji) unastawi ndani mwetu kwa njia ya sakramenti, hasa ekaristi. Stahili na sala za mwadilifu zinapata zawadi za Mungu kulingana na imani na upendo alivyonavyo; kumbe sakramenti zinaleta neema kwa nguvu zake zenyewe katika wale wasioweka kizuio. Kwa kuwa ziliwekwa ili kutugawia stahili za Mwokozi, zenyewe zinasababisha neema bila kutegemea sala na stahili za yule anayeziadhimisha wala za yule anayezipokea. Padri mwovu, na hata mtu asiye Mkristo, anaweza kubatiza mradi awe na nia ya kufanya Kanisa linavyofanya.

Hata hivyo sakramenti zinaleta neema kwa kiasi tofauti kulingana na juhudi za yule anayezipokea. “Kila mmoja anapokea uadilifu kadiri Roho Mtakatifu anavyomtakia kulingana na utayari wake” (Mtaguso wa Trento). Moto unawaka wenyewe, lakini sisi tunafaidi joto lake kadiri tunavyoukaribia. Vivyo hivyo tunafaidika na sakramenti kadiri imani yetu ilivyo hai na utashi wetu ulivyo motomoto. Kwa msingi huo Mkristo anapoondolewa dhambi anapata neema kadiri ya majuto yake. “Nguvu ya majuto ya mwenye kuungama ni kubwa, sawa au pungufu kuliko kiwango cha neema alichokipoteza; hapo anapata tena neema kwa kiwango kikubwa, sawa au pungufu kuliko awali” (Thoma wa Akwino). Kwa mfano, aliyekuwa na talanta tano kabla hajazipoteza kwa dhambi ya mauti, akiwa na majuto kama ya talanta mbili, anapata tena neema, lakini kwa kiasi kidogo kuliko awali. Kinyume chake, kwa majuto makubwa anaweza kuipata kwa kiwango kikubwa zaidi. Hilo ni muhimu kwa wale wanaoanguka wakati wa kupanda mlima; wanaweza kuinuka kwa bidii na kuendelea na safari yao kuanzia pale walipoanguka. Lakini wakiinuka kwa kuchelewa na bila bidii wanajikuta chini, badala ya kuendelea tu kupanda.

Kwa msingi huohuo komunyo moja yenye bidii inafaa kuliko nyingi vuguvugu. Kadiri tunavyomkaribia Yesu ekaristi kwa imani hai, tumaini imara na upendo motomoto tunafaidi neema za mwanga, upendo na ushujaa za kututosha hata tukashirikisha wengine. Kinyume chake, tunda la komunyo ni dogo tukikaribia meza takatifu kwa namna ambayo inatosha tu tusikufuru. Hayo yatufikirishe tuking’amua kuwa hatuendelei kweli baada ya kukomunika kila siku kwa miaka kadhaa (ingawa ni kweli pia kwamba mtu akiendelea, anazidi kufahamu unyonge wake kadiri anavyokuja kujua ukuu wa Mungu). Tuwe na bidii za kutosha itutokee kama kwa watakatifu: kwamba kila komunyo iwe na upendo mkubwa na matunda mengi kuliko ile iliyotangulia. Kumbe mara nyingi uzembe na uvuguvugu vinazuia ustawi huo: kwa kuambatana na dhambi nyepesi fulani, tunda la komunyo linazidi kupungua, kama kasi ya jiwe lililorushwa hewani wima ambayo inazidi kupungua mpaka jiwe likaanguka tena ardhini.

Upendo kwa Mungu

hariri

Dalili za upendo kwa Mungu usiokamilika

hariri

Upendo kwa Mungu haujakamilika ikiwa katika kumtumikia tunashikamana na faida yetu, tunajifanya lengo na kutamani turidhike. Kinachodhihirisha zaidi upungufu huo ni kwamba tukinyimwa faraja tulizokuwa tunazipata kwa Mungu, mara huo upendo haututoshi wala haudumu, bali unafifia na kupoa zaidi na zaidi. Upungufu huohuo upo katika kumpenda jirani: tunajifanya lengo la matendo ya upendo, tunaridhika na utendaji wetu wa kibinadamu, ambamo mna kiasi kikubwa cha harakaharaka na umimi, kikifuatwa na ubaridi tusiporudishiwa shukrani.

Mfumo wa upendo na dalili za ustawi wake

hariri

Dalili za ustawi wa upendo zinaelea katika mfumo wake wa kuwa urafiki unaotupasa tuwe nao kwa Mungu kutokana na wema wake usio na mipaka ambao unang’aa juu yetu ukituhuisha na kutuvuta kwake. Biblia inasema sehemu mbalimbali kuwa mwadilifu ni “rafiki wa Mungu” kama Abrahamu (Yak 2:23): hekima “huwafanya wanadamu kuwa rafiki za Mungu” (Hek 7:27); na Yesu alisema, “Ninyi nimewaita rafiki” (Yoh 15:15).

Basi, urafiki halisi una sifa tatu: kwanza ni upendo wa kumtakia mwingine mema tunayojitakia, tofauti na pendo tunalojitakia jema fulani, k.mf. chakula. Tunapaswa kuwatakia marafiki wetu mema yanayowafaa, na kumtakia Mungu ufalme wake uenee katika akili na nyoyo za watu. Pili, urafiki unadai wawili wapendane, yaani haitoshi upendo uwepo upande mmoja. Kadiri mema wanayotakiana ni bora, urafiki wao unakuwa bora. Uadilifu ndio msingi wake wasipotakiana tu mambo ya kupendeza na kuleta faida, bali uaminifu katika wajibu na maendeleo ya Kiroho. Tatu, urafiki unadai kufahamiana, kuchanga maisha walau kwa kubadilishana mawazo na miguso ya siri. Urafiki huo unaelekea muungano wa dhati wa mawazo, miguso, matakwa, sala, sadaka na utendaji. Sifa hizo tatu za urafiki halisi zinapatikana katika upendo unaotuunganisha na Mungu na watu ndani yake.

Kilindini mwa utashi wetu umbile linatuelekeza kumpenda Mungu, asili ya uhai wetu, kuliko tunavyojipenda na tunavyopenda lolote lile, kama vile kiungo kinavyompenda mwenye nacho kuliko kinavyojipenda ili kudumisha uhai. Lakini elekeo hilo, lililopunguzwa na dhambi asili, lisipoponywa na neema haliwezi kutufanya tumpende kimatendo Mungu kuliko yote.

Juu ya hilo, katika ubatizo tumepokea upendo ambao tunamtakia Mungu, asili ya neema, mema yanayomfaa, yaani awatawale watu moja kwa moja, kama vile yeye anavyotutakia mema sasa na milele. Urafiki huo unategemea kuishi pamoja, kwa kuwa Mungu anatushirikisha uhai wake mwenyewe: kwa neema tumezaliwa naye na kufanana naye kama watoto na baba yao. Upendo kati yetu na Mungu unadhihirika hasa akituangazia na kutuinua tutekeleze upendo wa kumiminiwa jinsi tusivyoweza kwa neema ya msaada ya kawaida. Ni ushirika wa Kiroho ulio utangulizi wa ule wa milele. Hata kwa kiwango cha chini, unatufanya tumpende Mungu kuliko tunavyojipenda na tunavyopenda zawadi zake, walau upande wa tathmini, ingawa pengine hatuhisi upendo huo (k.mf. wakati wa ukavu), nao mwanzoni hauna nguvu na ari zinazopatikana katika waliokamilika na hasa mbinguni. Mama anahisi upendo alionao kwa mwanae aliyempakata kuliko ule alionao kwa Mungu asiyemuona; lakini akiwa Mkristo kweli anampenda kitathmini Mungu kuliko mtoto. Halafu, upendo wa tathmini ukistawi unazidi kupata nguvu (na kuitwa ari) mpaka mbinguni utashinda mapendo yetu makuu. Upendo huo hauhitaji elimu, inatosha kumjua Baba wa mbinguni kwa imani. Tukiacha kumpenda kwa dhambi yoyote ya mauti, mara tunaanza kupotea. Tunavyoona, upendo wa tathmini ni kinyume cha miguso inayoonyesha upendo isionao.

Upendo ukiwa hivyo, dalili za ustawi wake ni hizi zifuatazo. Kwanza ni zile za neema inayotia utakatifu: 1° kutojisikia kuwa na dhambi yoyote; 2° kutotafuta malimwengu (anasa, mali, heshima); 3° kumfurahia Mungu na kumfikiria, kumuabudu, kumshukuru, kumuomba msamaha, kusema naye, kumtamani. Tuongeze dalili zifuatazo: 4° kutaka kumpendeza Mungu kuliko wale wote tunaowapenda; 5° kumpenda jirani kwa matendo (ingawa ana kasoro kama sisi) kwa sababu ni mtoto wa Mungu na anapendwa naye. Hapo tunampenda Mungu katika jirani, na tunampenda jirani katika Mungu. Heri anayependa hivyo, akifurahia tu kumpendeza Mungu. Akiwa mwaminifu siku moja ataonja utamu wa upendo huo na kuridhika pasipo mfano ndani ya yule aliye wema usio na mipaka.

Upendo wa Mungu na silika yetu

hariri

Tungeangukia uzushi wa Pelaji kama tungedhani upendo wa Mungu unagawiwa kadiri ya sifa na maelekeo ya umbile. Kumbe “kila mmojawetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo” (Ef 4:7). “Upendo upitao maumbile ambao Mungu kwa wema wake anatumiminia moyoni… unapatikana katika ncha ya juu ya roho… isiyotegemea maumbile yoyote… Hata hivyo ni kweli kwamba watu ambao kiumbile wanaelekea mapenzi, wakishatakaswa vizuri kutoka pendo kwa viumbe, wanafanya maajabu katika mapenzi matakatifu, kwa kuwa ndani mwao upendo una urahisi mkubwa wa kuenea popote. Ndiyo asili ya utamu wa kupendeza sana usiojitokeza katika wenye silika kali, chungu, ya huzunihuzuni na ambao ni vigumu kushirikiana nao. Lakini, ikiwa watu wawili, ambao kwa maumbile mmojawao anaelekea mapenzi na upole, na mwingine ukali na uchungu, wana kiwango kilekile cha upendo, bila shaka watampenda Mungu sawa, ingawa si kwa namna moja. Moyo mpole kiumbile utapenda kwa urahisi, upendevu na utamu mkubwa zaidi, ila si kwa imara na ukamilifu zaidi; kumbe upendo utakaoota kati ya miba na karaha ya umbile kali na kavu utakuwa wa kishujaa na mtukufu zaidi, kama vile wa kwanza ulivyo mzuri na wa kupendeza zaidi. Basi, si muhimu sana mtu kuelekea kupenda kiumbile tunaposema juu ya upendo upitao maumbile na ambao kwao tunatenda kwa namna ipitayo umbile tu. Lakini, ee Theotimo, ningependa kuwaambia watu wote: enyi watu wa kufa, mkiwa na moyo unaoelekea kupenda, mbona hamlengi upendo wa kimbingu na wa Kimungu? Ama mkiwa na moyo mkali na mgumu, enyi maskini, kwa kuwa mnakosa pendo la kiumbile, mbona hamlengi upendo upitao maumbile ambao mtajaliwa kwa upendo na yule anayewaita kitakatifu mumpende?” (Fransisko wa Sales).

Kulingana zaidu na zaidi na matakwa ya Mungu yaliyo wazi

hariri

Upendo wa kulingana na matakwa ya Mungu ni sisi kutaka yale yote ambayo wema wake unatuonyesha una nia nayo. Unayaonyesha kwa njia ya amri, mashauri yanayolingana na wito wetu, na matukio. Ndiyo tunayoyazungumzia tukisema, Utakalo lifanyike. Basi, tuone tunavyopaswa kulingana nayo zaidi na zaidi. Kumpenda Mungu katika ustawi ni kwema, mradi tusipende ustawi sawa naye au kuliko yeye. Kwa vyovyote hicho ni kiwango cha chini, rahisi kwa wote. Kupenda matakwa ya Mungu unapokoma urahisi wa kutimiza wajibu, ni kiwango kamili zaidi, lakini tunapaswa kumuiga Yesu kwa kumpenda Mungu hata katika mambo ya tabu na yasiyotarajiwa, katika matatizo ya kila siku na dhiki ambazo maongozi yake yanaacha zitokee kwa ajili ya jambo jema zaidi. Hatuwezi kumpenda kweli tusipopenda dhiki hizo, si kwa zenyewe, bali kwa ajili ya mema ya Kiroho yanayotokana na uvumilivu wa kuzistahimili. Basi, kupenda mateso na machungu kwa ajili ya Mungu ndiyo kiwango cha juu cha upendo ambapo yanayotupata yanageuka kuwa mema.

Plato alisema pendo motomoto ni fukara, uchi, hoi, unahitaji daima, unalala nje mahali pagumu, kwa sababu unamfanya mtu aache vyote kwa yule anayempenda, unaondoa usingizi na kulenga muungano wa dhati zaidi na zaidi. Hayo aliyoyasema kuhusu pendo la kimaumbile ni ya kweli zaidi kuhusu upendo wa Mungu unapochoma kwa ndani: “Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao… Tumefanywa kama takataka za dunia” (1Kor 4:11,13). “Nani alimfikisha kwenye hali hiyo kama si upendo? Upendo ndio uliomtupa Mt. Fransisko wa Asizi uchi miguuni pa askofu wake na uliomfanya afe uchi ardhini; upendo ndio uliomfanya ombaomba maisha yake yote. Upendo ndio uliomtuma shujaa Fransisko Saveri akiwa fukara, mwenye shida, amevaa nguo zilizochanika, huko na huko kati ya Wahindi. Upendo ndio uliomfanya kadinali bora Mt. Karolo Borromeo, askofu mkuu wa Milano, afikie ufukara mkubwa hivi hata akaonekana kama mbwa nyumbani mwa bwana wake” (Fransisko wa Sales).

Upendo wa kulingana na matakwa ya Mungu ni kama moto ambao mwali wake ni mzuri na safi kadiri ulivyolishwa na kuni bora, kavu na zilizotakaswa. Ndiyo sababu pendo lolote lisilotokana na mateso ya Bwana ni la juujuu na la hatari. Kifo cha Yesu, tokeo kuu la upendo wake kwetu, ndiyo sababu hasa ya kumpenda. Hakuna kinachoridhisha kuliko upendo wake, kwa njia ya kuachana kikamilifu na vyote ili kuungana kwa ndani na matakwa ya Mungu.

Huo upendo wa kulingana na matakwa yake yaliyo wazi unatuwezesha kujiachilia kwa matakwa ya Mungu yasiyo wazi bado, ambayo yanaongoza ya kesho. Yaliyo wazi yanadai utiifu, na yasiyo wazi bado yanadai tujiachilie kwake kitoto kwa imani, tumaini na upendo. Azimio la “kushika uaminifu na kujiachilia” linaoanisha kutenda na kukubali kutendewa, likishinda utulivu wa kivivu na mahangaiko yasiyozaa kitu ya wanaojiamini bila kuwa na sala ya dhati. Kujiachilia kwa Mungu ndiyo njia ya kufuata; uaminifu wa kila nukta ndiyo hatua za kupigwa katika njia hiyo. Uaminifu katika mwanga wa amri unatuingiza katika fumbo lenye giza la matakwa ya Mungu kuhusu wokovu wetu.

Moyoni mwetu hatuna upendo ule wote tunaouhitaji: ndiyo sababu ni upumbavu kuutapanya ovyo kwa viumbe. Upendo wa Mungu unapoa kwa dhambi nyepesi (au kwa kuambatana nayo). Kinyume chake tendo karimu la upendo linatustahilisha ustawi wa adili hilo ambalo linayauhisha mengine yote na kufanya yastahili. Ustawi huo unatuandaa kumuona na kumpenda Mungu vizuri zaidi milele. Basi, tunachotoa ili kujipatia hazina hiyo isiyopimika tukione si kitu. Tunapompa Mungu upendo wetu, daima anatupatia wa kwake. Tena anatutangulia kwa kuwa hatuwezi kushinda umimi wetu pasipo neema yake tunayopaswa kujiombea mfululizo kama tunavyopumua.

Mungu anatamani tumpende kila siku zaidi. Hatutakiwi kamwe kusema tunampenda vya kutosha, bali tunapaswa kuendelea mfululizo katika upendo huo. Tunamuendea Mungu kwa hatua za upendo, yaani kwa matendo ya upendo yanayozidi kuwa makuu. Safarini tunaimba wimbo wa upendo, ule wa liturujia ulio sauti ya Bibi arusi wa Kristo. Si vibaya kutetemeka pengine mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini upendo unatakiwa kutawala. Tunapaswa kumcha Mungu kwa upendo wa kitoto, si kumpenda kwa hofu ya kitumwa; ndiyo sababu uchaji unaoogopa dhambi unastawi pamoja na upendo, kumbe hofu ya adhabu inazidi kupungua.

Huo upendo unastawi kwa kubeba msalaba: “Moyo wenye bidii zaidi unajilisha misalaba na mateso; kumbe waoga wanaridhishwa na mafanikio yao tu. Zaidi ya hayo upendo safi wa Mungu unatekelezwa kwa urahisi mkubwa katika mapingamizi kuliko katika raha, kwa sababu tabu haina lolote la kuvutia ndani mwake, isipokuwa mkono wa Mungu unaoituma… wakati mafanikio yanayo yenyewe vivutio vinavyonasa hisi” (Fransisko wa Sales). Upendo wa kulingana na matakwa ya Mungu ukistawi unafanya mateso unayojilisha yawe matamu; hapo unasonga mbele kwa hakika.

Upendo huo unastawi kila tunapofisha umimi wetu. Ili tuwe na hamu motomoto ya upendo wa Mungu tunapaswa kukomesha yale yote usiyoweza kuyahuisha. Hapo unayafanya maadili yampendeze kuliko yanavyompendeza kwa yenyewe kwa kuwa stahili ya matendo maadilifu inategemea kiwango cha upendo. Kwa hiyo, kutimiza wajibu wetu kunaweza kutakaswa hivi kwamba hata dakika moja isipotee milele. Ikiwa tuliwahi kuwa na upendo mkubwa halafu hatujatenda dhambi yoyote ya mauti, ila tumepoa kwa kuambatana na dhambi nyepesi, tunayo bado hazina hiyo, ingawa uwezo wake wa kuenea umepungua, kama ilivyo kwa mwanga katika chemni chafu. La muhimu ni kuondoa moshi upesi. Kiutekelezaji, tuone tunavyoweza kuweka mapendo yetu yoyote chini ya upendo wa Mungu: “Naweza kupinga hamu ya utajiri na tamaa za kidunia ama kwa kuvidharau vinavyostahili, ama kwa kutamani yasiyokwisha; kwa njia hiyo ya pili pendo la kihisi na la kidunia litaangamizwa na upendo wa kimbingu… Hivyo upendo wa Mungu unashika nafasi ya mapendo na maono na kuyatiisha” (Fransisko wa Sales).

Huo upendo wa kulingana na matakwa ya Mungu unafikisha kwenye upendo wa kufurahia yale yote yanayochangia utukufu wa Mungu, pamoja na wazo la kuwa hekima na heri zake hazina mwisho, la kuwa ulimwengu wote unadhihirisha wema wake, na la kuwa wateule watamtukuza milele. Tunaweza tukahisi upendo huo wa kufurahia hayo kwa uvuvio maalumu wa Mungu, wakati upendo wa kulingana na matakwa yake unaweza kuwepo kwa neema ya msaada ya kawaida.

Upendo wa kidugu, mng'ao wa ule kwa Mungu

hariri

Kumpenda jirani ni tokeo la lazima na ishara ya upendo kwa Mungu: “Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu’, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo” (1Yoh 4:20). Kwenye hatua ya mwanga upendo wa kidugu ni moja kati ya dalili kuu za maendeleo yanayotakiwa kupatikana. Ni muhimu tusisitize sababu hasa ya kuutekeleza, tusije tukauchanganya na mengineyo, k.mf. upendevu, tabia ya kijamii au urahisi wa kuruhusuruhusu lolote; urahisi huo unaonekana kufanana na upendo, lakini unatofautiana na adili hilo la kumiminiwa kwa kuwa unapuuzia imani na ukweli, kumbe upendo unavidai kama msingi wake. Ili tuwe na mtazamo sahihi tufikirie upendo wa Yesu kwetu.

Upendo kwa Mungu unatakiwa kuenea kwa jirani

hariri

Upendo wa kidugu ambao Bwana anadai tuwe nao unatofautiana na elekeo la kibinadamu la kutenda mema ili kupendeza, na lile la kuwapenda wanaotutendea mema, kuwachukia wanaotutenda mabaya na kutojali wengine wote. Pendo la kimaumbile linatufanya tumpende jirani kwa sifa njema za umbile lake na kwa misaada anayotupatia. Kumbe upendo wa Kikristo ni wa juu: “Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu wa mbinguni… Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je, nao hawafanyi yayo hayo?” (Math 5:43-46). Tunapaswa kuwapenda maadui kwa upendo uleule tulionao kwa Mungu, kwa sababu hakuna maadili mawili ya upendo, moja kwa Mungu na lingine kwa jirani, bali ni moja tu linaloelekea kwanza kwa Mungu, anayependwa kuliko yote, halafu kwetu wenyewe na kwa jirani.

Kuhusu kuwapenda Kimungu watu wenye kasoro kama sisi, ni kwamba anayempenda rafiki yake, anawapenda pia watoto wa rafiki na kuwatakia kila la heri kutokana na upendo kwa baba yao. Kwa ajili yake ataharakisha kuwasaidia na atakuwa tayari kuwasamehe wakimkosea. Basi, kwa kuwa watu wote ni wana wa Mungu kwa neema, au walau wanaitwa kuwa hivyo, tunapaswa kuwapenda kwa upendo upitao maumbile na kuwatakia heri ya milele kama tunavyojitakia: tunatakiwa kuelekea lengo hilo wote sawia kwa msaada wa neema na kwa kuishi upendo uleule.

Hivyo upendo ni kiungo cha ukamilifu kinachotuunganisha ipasavyo na Mungu na jirani yeyote: unatufanya tumpende Mungu ndani ya binadamu na binadamu ndani ya Mungu. Upendo huo ni wa nadra kwa kuwa wengi wanajitafutia faida hasa na kuelewa kwa urahisi zaidi usemi ufuatao: “Jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino” (Law 24:20). Kabla ya Yesu amri ya upendo wa kidugu ilikuwa inatekelezwa kidogo tu, hata ikampasa kuisisitiza toka hotuba ya kwanza mlimani hadi maneno yake ya buriani. Mitume wakafanya vilevile katika barua zao.

Ili tumpende Kimungu jirani yetu tunapaswa kumtazama kwa imani na kujiambia, “Mtu huyu, mwenye tabia tofauti na ya kwangu, amezaliwa na Mungu au anaitwa kuzaliwa naye na kushiriki uhai na heri ya Mungu sawa nami”. Mbele ya Wakristo wasiotupendeza tujiambie, “Pamoja na yote, huyu ni kiungo cha mwili wa Kristo, pengine jirani na moyo wake; ni jiwe hai ambalo Mungu analichonga ili kuliweka mahali pake katika Yerusalemu ya mbinguni. Niwezeje kutompenda nikimpenda Mungu, Baba yetu sote? Nisipompenda, upendo wangu kwa Mungu ni uongo tu; kumbe nikimpenda ni dalili ya kuwa nampenda Mungu”.

Pengine mafundisho hayo yanapingwa kwa kusema, “Je, ndiyo namna ya kumpenda mtu kweli, au ni kumpenda Mungu tu ndani ya binadamu, kama tunavyopenda almasi katika sanduku lake?” Hakika, mtu anataka kupendwa kwa ajili yake mwenyewe, lakini kwa msingi huo hawezi kupendwa Kimungu. Tena upendo haumpendi Mungu tu ndani ya binadamu, bali unampenda mtu ndani ya Mungu na kwa ajili ya Mungu. Unampenda kweli jinsi anavyotakiwa kuwa, kiungo cha milele cha mwili wa Kristo, nao unafanya yote unayoyaweza ili afike mbinguni. Unampenda vilevile jinsi alivyo kwa neema, na asipokuwa nayo, unapenda umbile lake, si kadiri lilivyo kisha kuanguka na kuvurugika, bali kadiri lilivyo sura ya Mungu lenye uwezo wa kupandikiziwa neema ili kuwa mfano wake.

Ufanisi wa upendo huo wa Kimungu

hariri

Tukimpenda jirani ndani ya Mungu na kwa ajili ya Mungu, tunampenda zaidi na kwa ukamilifu mkubwa zaidi. Hatupendi kasoro zake, ila tunazivumilia; ndani yake tunapenda yale yote yaliyo bora, yanayokusudiwa kustawi na kuchanua katika uzima wa milele. Badala ya kuwa upendo usio na matendo, unatuelekeza kumtazama jirani yeyote kwa haki, kumkubalia matakwa yake kadiri yasivyopingana na amri za Mungu, kukwepa migogoro au kuitatua mapema. Wema huo unang’aa na kutufanya tupende mfululizo si yaliyo mema kwetu tu, bali yaliyo mema kwake kwa mtazamo wa Mungu, tumtakie mema yasiyopita kamwe, hasa kumpata moja kwa moja yeye, aliye wema mkuu.

Upana na utaratibu wa upendo

hariri

Kwa hiyo, upendo wetu unatakiwa kuwaelekea bila mipaka wala ubaguzi wote duniani, toharani na mbinguni na kusimama mlangoni pa moto wa milele tu. Walaaniwa tu hatuwezi kuwapenda kwa kuwa hawawezi tena kuwa wana wa Mungu: wanamchukia milele, hawamuombi msamaha wala neema ya toba; hawana nia ya kuongoka hata chembe. Pamoja na hayo, wanafaidi huruma ya Mungu kwa kuadhibiwa kidogo kuliko wanavyostahili; jambo hilo linapendeza upendo wetu ambao kwa namna hiyo unafikia huko pia. Tusipokuwa na hakika kuhusu laana ya milele ya malaika au mtu fulani, tunadaiwa kumpenda kila mmoja.

Ili upendo uwaenee wote si lazima uwe sawa kwa wote; ustawi wake katika hatua ya mwanga unazidi kuonyesha utaratibu wa upendo ambao unaheshimu na kuinua vizuri ule wa maumbile. Hivyo tunapaswa kumpenda Mungu kuliko yote, halafu roho yetu, halafu ile ya jirani, hatimaye mwili wetu ambao tuwe tayari kuutoa kwa wokovu wa roho yoyote, hasa tukiwa na majukumu kwake (k.mf. kama wachungaji wa jimbo au wa parokia). Kadiri upendo unavyostawi ndani mwetu, tunaelewa tunavyopaswa kupenda zaidi kitathmini walio bora, karibu zaidi na Mungu, ingawa tunaelekea kupenda zaidi kihisi walio karibu nasi (kwa vifungo vya damu, jamii, wito au urafiki).

Mpangilio huo tunaozidi kuutambua unatuonyesha kuwa Mungu anataka kutawala mioyo yetu, pasipo kuzuia mapendo halali ambayo upendo wake unakuja kuyahuisha, kuyainua, kuyatakasa na kuyaongezea ukarimu. Ustawi wa upendo unafuta “usisi”, yaani tabia ya kujikuza kama kundi kwa kupuuzia wengine. “Kwa hali na ahadi siwezi kuwa wa mashirika mbalimbali, lakini kwa elekeo la upendo mimi ni wa yote… Nakiri kwa unyofu kwamba nilihuzunika sana kila nilipoona nyumba za kitawa kuoneana wivu… Je, damu iliyowapatia watawa wowote mema yote waliyonayo, si ile ya Yesu Kristo? Au ni ile ya Mt. Augustino, ya Mt. Benedikto au ya Mt. Bernardo? Mungu wangu! Dumisha imara uelewano kati ya watumishi wako… Mashirika mbalimbali ya kitawa ni miili tofauti, lakini yanatakiwa kuwa moyo mmoja, roho moja tu kama tunavyosoma kuhusu Wakristo wa kwanza” (L. wa Ballon). La sivyo tunarudia ule ufinyu wa mawazo alioulaumu Mt. Paulo, “Maana hapo mtu mmoja asemapo, ‘Mimi ni wa Paulo’, na mwingine, ‘Mimi ni wa Apolo’, je, ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye” (1Kor 3:4-7). “Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?” (1Kor 1:13). “Basi, mtu yeyote asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu” (1Kor 3:21-23).

Huo utaratibu wa upendo unatakiwa uzidi kuonekana ndani ya anayeendelea: kwa namna fulani moyo wake unapaswa kupanuka kama ule wa Mungu kutokana na ustawi wa upendo ambao ni kushiriki uhai wa Mungu, upendo wa milele. Upendo huo unatakiwa kuwa si wa ndani tu, bali wa vitendo, kama vile Yesu alivyotupenda hadi kufa msalabani, na kama watakatifu wengi walivyowapenda wenzao hadi kuwapa ushahidi wa damu. Ndio upendo wa kidugu ulio uenezi wa ule wa Mungu.

Namna ya kuendelea katika upendo huo wa kidugu

hariri

Nafasi za kuuvunja ziko nyingi hata katika mazingira bora, kwanza kutokana na kasoro za hawa na hawa ambao hawajafikia ukamilifu hata wakiulenga. Kila mmoja wetu ni kama piramidi isiyo na kilele: mara nyingi tunamuona jirani kuwa hivyo lakini tunasahau kwamba yeye pia anatuona hivyo. Tunatazama “kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu” yetu, tusione “boriti iliyo ndani ya jicho” letu wenyewe (Math 7:3).

Hata kama kasoro zote zingekoma kabla ya kuingia mbinguni, nafasi za kubishana na kukwaruzana zingedumu kutokana na tofauti za tabia, maelekeo, akili na malezi, halafu uchovu na shetani. Huyo anapenda kufitini hasa katika mazingira bora ili azuie mema mengi yanayoweza kufanyika huko, kuliko katika yale anayoyatawala tayari kwa mawazo mapotovu yaliyoenea na mifano mibaya inayotolewa. Tunavyosoma katika Injili na katika maisha ya watakatifu, adui anasia magugu kwenye ngano bora naye anaweka lenzi katika ubunifu wa waadilifu waone chembe ni mlima.

Maongozi ya Mungu yanawaachia kwa makusudi nafasi nyingi za kujinyenyekeza na kutimiza upendo wa kidugu kati yao. Katika udhaifu ndipo neema ya Mungu inapoonyesha nguvu yake, na ndipo uadilifu wetu unapokamilika; udhaifu wetu unatunyenyekesha na ule wa wenzetu unatuzoesha. Mbinguni tu nafasi zote za kubishana zitakoma, kwa kuwa wenye heri wanaona ndani ya Mungu yale yote wanayotakiwa kuyawaza, kuyataka na kuyatenda. Hapa duniani watakatifu wenyewe wanaweza wakashindana, na kwa muda fulani hakuna aliye tayari kukubali mtazamo wa mwingine kwa sababu dhamiri inamdai ashike msimamo asiweze kuachana na wajibu wake, isipokuwa kujinyima haki tu. Kwa mfano watakatifu Karolo Borromeo na Filipo Neri hawakuelewana kuhusu kuanzisha shirika moja; hakika Bwana alitaka yaanzishwe mawili.

Kati ya matatizo mengi hivyo, upendo wa kidugu unatakiwa kustawi namna mbili: kwa kumtazama jirani kwa wema kadiri ya imani, halafu kwa kumtendea mema mbalimbali.

Kwanza tumtazame jirani kwa imani, si kwa macho au akili vilivyoathiriwa na umimi. Ni lazima tujikane ili kutambua uhai wa Kimungu chini ya sura duni ya wengine. Mara nyingi kinachotuchukiza kwa jirani si makosa makubwa dhidi ya Mungu, bali kasoro za silika aliyo nayo ingawa ni mwadilifu kweli. Pengine tuko tayari kuvumilia walio mbali na Mungu lakini wanapendeza kiumbile, kumbe wengine waliopiga hatua katika ukamilifu ni zoezi kubwa la subira kwetu. Basi tuamue kuwatazama wote kwa imani ili kutambua ndani mwao kile kinachompendeza Mungu na ambacho sisi pia tunapaswa kukipenda.

Kinachopingana zaidi na mtazamo huo wa wema ni hukumu isiyo na msingi wa kutosha. “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa” (Math 7:1-2). Si kushuku tu, bali kuhukumu kwa kutegemea dalili ndogo; tunaona mbili na kudai ni nne, kwa sababu ya kiburi chetu. Ni dhambi ya mauti dhidi ya haki kumhukumu jirani kwamba ametenda dhambi ya mauti, hasa kukitolewa nje kwa maneno au matendo. Kwa kuwa jirani, pamoja na haki ya kutimiza wajibu wake, anayo ile ya kuwa na sifa njema, nayo ni muhimu kuliko ile ya kumiliki vitu. Tuheshimu haki yao tukitaka ya kwetu iheshimiwe. Kwa hiyo tutafsiri kwa wema mkubwa iwezekanavyo mambo yasiyo na hakika. Tusipoweza kuondoa shaka, tunaweza kujihadhari naye asije akatudanganya, lakini tusitoe hukumu imara kwa dalili ndogo: mara nyingi hukumu zisizo na msingi wa kutosha ni za uongo. Tuhukumuje kwa hakika nia za mtu ambaye hatujui shaka, makosa, shida, vishawishi, hamu na majuto yake? Tuhukumuje tusipokuwa na faili za kesi?

Hata kama hukumu ni za kweli zinabaki kuwa kinyume cha haki kwa sababu tunatumia mamlaka isiyo yetu. Kanisa lenyewe halihukumu undani wa mtu. Zaidi tena, hukumu hizo ni kinyume cha upendo, zinatokana na ubaya katika kumtazama mtu, ingawa mara nyingi zinatamkwa chini ya kinyago cha wema. Hatufuati huruma bali umimi na kiburi, na tunamwekea sheria Roho Mtakatifu kwa kutaka njia ya kufuatwa iwe ile ya kwetu tu. Badala ya kumuona jirani kuwa ndugu, tunamuona ni mgeni au adui ambaye aondoshwe au kushushwa. Ndicho kinachozuia sala ya kumiminiwa kama ushungi unaofunika macho ya roho. Tusipofika mbali hivyo, inatutokea pengine kuhukumu undani wa mtu ili kujidai tunasoma mioyo; kumbe Mungu tu anaiona wazi. Tuangalie kwamba tunapohukumu hatutabiri kuwa baada ya kitambo tutatumbukia kosa kubwa kuliko lile tunalowalaumu wenzetu.

Uovu ukiwa wazi, Mungu hadai tusiuone, ila anatukataza tusisengenye kwa kiburi. Pengine anatuagiza, kwa msingi wa upendo, ukosoaji wa kidugu ambao ufanywe kwa wema, unyenyekevu, upole na busara kadiri ya Injili: “Ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu: akikusikia, umempata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru” (Math 18:15-17). Tufikirie kwanza kama utafaa na kama kuna tumaini la mtu kutubu, au kama ni lazima tumuarifu mkubwa wake. Tendo kamili ni kumhurumia mkosefu kwa kubeba kosa lake mbele ya Mungu, kama vile Bwana alivyobeba msalabani dhambi zetu zote na kutuambia, “mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yoh 15:12).

Kisha kumtazama jirani kwa wema, tumpende kwa vitendo, kwa kuvumilia kasoro zake, kumrudishia mema kwa mabaya, kuepa kijicho, kuomba umoja wa mioyo. Tunaweza kuvumilia kasoro za watu tukizingatia kuwa mara nyingi kinachotusumbua kwao si dhambi ya mauti bali silika (k.mf. hasirahasira au utulivu mkubwa mno), ufinyu wa mawazo, kimbelembele n.k. Hata kama wana kosa kubwa, tusidhani tumekamilika tukiwasema kama alivyofanya Farisayo hekaluni. Tukumbuke Mungu haachi mabaya yatokee isipokuwa kwa ajili ya mema makubwa zaidi, tofauti na sisi tusioweza kusababisha mema isipokuwa kwa njia ya mema. Kukwazwa na maovu na kupatwa na ari chungu kulifanya marekebisho kadhaa ya utawa yasizae matunda. Tuseme ukweli kwa kiasi na wema, si kumtupia mtu usoni kwa dharau. Tunapaswa vilevile kutumia busara tusiseme juu ya makosa ya jirani bila sababu ya kutosha, la sivyo tunasengenya na hata kusingizia.

Injili inatufundisha pia kurudisha mema kwa mabaya, kwa njia ya sala, mifano mizuri na kusaidiana. Namna mojawapo ya kujipatia fadhili za Teresa wa Yesu ilikuwa kumtaabisha, kwa kuwa alifuata shauri la Bwana: “Mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia” (Math 5:40). Hii ni kwa sababu si muhimu kutetea haki zako za kidunia bali kumuokoa ndugu yako apate uzima wa milele. Kumuombea jirani wakati wa kuteseka kwa ajili yake kuna nguvu za pekee, kama kwa Yesu alipowaombea watesi wake na kwa Stefano alipopigwa mawe.

Tunapaswa pia kukwepa kijicho, tukifurahia sifa walizojaliwa wenzetu. “Mguu ukisema, ‘Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili’; je, si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, ‘Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili’; je, si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio, ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, ‘Sina haja na wewe’; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, ‘Sina haja na ninyi’… bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake” (1Kor 12:15-21,25-27). Tutimize upendo hasa kwa wadogo wetu kwa sababu ni dhaifu zaidi, na kwa wakubwa wetu waliobeba mzigo mkubwa zaidi. Tusiangalie kasoro zao: pengine mahali pao tungekuwa nazo nyingi zaidi. Kinyume chake tuwasaidie iwezekanavyo, kwa busara na kama kwa kutojitokeza.

Hatimaye tuombe umoja wa roho na mioyo, alivyofanya Bwana: “Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja” (Yoh 17:22). Katika Kanisa la mwanzoni “jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika” (Mdo 4:32). Baadaye, lilipoenea duniani kote, halikuweza kudumisha hali hiyo kati ya viungo vyote, lakini mashirika ya kitawa na vyama vya Kikristo vinatakiwa kukumbusha huo umoja wa asili. Mahali ambapo vitu vya nje na vipindi vya sala ni vya pamoja, ni lazima uwepo umoja wa ndani, la sivyo vingekuwa uongo kwa Mungu, kwa watu na kwetu sisi. Umoja wa mioyo unachangia kulipamba Kanisa kwa sifa angavu ya utakatifu. Ukikusanya viungo mbalimbali vya mwili wa Mwokozi unathibitisha kuwa Neno alifanyika mwili akakaa kwetu ili atuunganishe na kutupa uzima: “Wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi” (Yoh 17:23).

Ari kwa utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa watu

hariri

Ili tuelewe upendo unavyotakiwa kuwa hasa kwenye hatua ya mwanga, ni lazima tuzingatie ari inayompasa hasa mtu aliyewekwa wakfu kwa Mungu. Ari kwa utukufu wake na kwa wokovu wa watu ni ari moja, ni umotomoto wa upendo uleule unaotakiwa kuwepo hata katika ukavu na majaribu ya kila aina; pengine huo umotomoto wa utashi una juhudi na stahili kadiri mtu asivyouhisi.

Upendo wa kishujaa

hariri

Ili tuelewe upendo wa kishujaa ni nini, tunapaswa kuzingatia ulivyo kwanza kwa Mungu, halafu kwa jirani.

Upendo wa kishujaa kwa Mungu: kulingana kikamilifu na matakwa yake na kuupenda msalaba

hariri

Upendo wa kishujaa kwa Mungu unadhihirishwa kwanza na hamu motomoto ya kumpendeza, kwa kuwa kumpenda fulani kwa ajili yake ni kumtakia mema, kutaka yale ambayo yanamfaa na kumpendeza. Kumpenda Mungu kishujaa ni kutaka, hata katika matatizo makubwa, kwamba matakwa yake matakatifu yatimizwe na utawala wake uwaenee wote. Hamu hiyo ni upendo unaothibitishwa na matendo, kwa kulingana na matakwa ya Mungu katika kutekeleza maadili yote. Hivyo mtu anafikia uaminifu wa kudumu katika mambo madogo kama katika yale makubwa na magumu zaidi.

Upendo huo wa kishujaa unadhihirika katika utakaso wa Kimungu wa roho, tunapopaswa kumpenda kwa ajili yake pasipo faraja yoyote, katika ukavu mkubwa wa muda mrefu na vishawishi vya ukinaifu, uzembe na ulalamishi. Bwana akionekana kutuondolea zawadi zake na kutuacha tufadhaike si kwamba amepungukiwa wema wake usio na mipaka, asistahili tena kupendwa kwa usafi. Ikiwa hapo, bila kujali ukavu huo, mtu anapenda kukaa peke yake na Mungu, hasa mbele ya sakramenti kuu, na maisha yake yanazidi kuwa sala ya kudumu, basi hiyo ni dalili ya upendo wa kishujaa.

Ulinganifu wa kishujaa na matakwa ya Mungu unadhihirika mtu anapopokea kwa upendo yale ambayo hayampendezi na yanamtia tabu, akizidi kuona ukweli wa neno hili: “Mema na mabaya, uzima na mauti, umaskini na utajiri, hayo yote yatoka kwa Bwana” (YbS 11:14). Hapo ana hakika ya dhati ya kuwa Mungu anatumia hata uovu wa binadamu ili kuwastahilisha wale wanaotaka kuishi kwa ajili yake tu. Ndivyo Ayubu alivyopokea misiba na Daudi alivyovumilia matusi ya Shimei. Katika matatizo makubwa watakatifu, pamoja na kufanya wanavyoweza, wanasema, “Yote yatatokea anavyotaka Mungu wetu mwema”. Dalili hiyo inathibitishwa na kwamba, aliyejinyima hivyo matakwa yake, anaonja furaha takatifu: kwa kuyalinganisha zaidi na zaidi na yale ya Mungu anayo yale yote anayoyataka.

Bernardo wa Clairvaux alifafanua hatua za upendo wa kishujaa akisema, “Upendo wa Mungu unasababisha tumtafute bila kukoma; tufanye kazi mfululizo kwa ajili yake; tuvumilie majaribu yote pamoja na Kristo, bila kuchoka; tumuonee kiu halisi Mungu; tumkimbilie haraka; tutende kwa uhodari mtakatifu na ushujaa usioogopa; tuambatane na Mungu moja kwa moja; tuwake moto mtamu na kama kuteketea kwa ajili yake; hatimaye tuungane naye kabisa mbinguni”. Dalili kuu ya upendo wa kishujaa kwa Mungu ni kuupenda msalaba, ambako ndiko subira na ulinganifu na matakwa ya Mungu tulivyozungumzia vinakofikisha. Bwana alimuambia Mt. Katerina wa Siena, “Ndiyo dalili iliyoonekana ndani ya mitume walipompokea Roho Mtakatifu. Walitoka ghorofani, wakiwa wameondolewa hofu yoyote, wakatangaza neno langu na kuhubiri mafundisho ya Mwanangu pekee. Badala ya kuogopa mateso, wakawa wanayaona ni utukufu kwao… Wenye hamu ya heshima yangu, na njaa ya wokovu wa watu, wanakimbilia meza ya msalaba mtakatifu… Hakuna kinachoweza kulegeza mwendo wao: wala matusi, wala dhuluma, wala anasa ambazo ulimwengu unawatolea… Moyo uliogeuzwa kabisa na upendo unafurahia na kuonja lishe hiyo ya wokovu wa watu, ukiwa tayari kuvumilia yote kwa ajili yao… Ndicho kinachothibitisha bila shaka kwamba mtu anampenda Mungu wake kikamilifu na pasipo kujitafutia faida… Hao nawajalia neema ya kusikia kwamba sitenganiki nao kamwe”. Yaani utekelezaji bora wa upendo unaendana kwa kiasi kilekile na tendo la kipaji cha hekima linalowawezesha kama kung’amua uwemo wa Mungu ndani mwao. Ndiyo maisha halisi ya kuzamia mafumbo, yanayowezekana tu kwa kuupenda msalaba, ambako tena kunawezekana tu kwa kulikazia macho fumbo la Yesu kufa kwa kutupenda. Ndiyo sababu Bwana alimuambia tena, “Mara wewe na watumishi wangu wengine mtakapojua ukweli wangu hivyo, mtakuwa tayari kuvumilia hadi kufa tabu zote, dharau, matusi ya maneno na matendo kwa utukufu na heshima ya jina langu. Ndivyo utakavyopokea na kuvumilia tabu, yaani kwa subira, shukrani na upendo”. Ndizo dalili za upendo wa kishujaa kwa Mungu: kulingana kikamilifu na matakwa yake katika majaribu, na kuupenda msalaba. Kuna dalili nyingine bado: upendo kamili kwa jirani.

Upendo wa kishujaa kwa majirani: hamu motomoto ya wokovu wao; wema unaowaenea wote

hariri

Upendo unatuelekeza kumpenda jirani ndani ya Mungu na kwa ajili ya Mungu, yaani kwa sababu Mungu anampenda na kama Mungu anavyompenda. Unatufanya tutamani jirani awe wa Mungu tu na kumtukuza milele. Upendo wa kishujaa kwa jirani upo tayari tunapotawala mara vishawishi vikali vya kijicho, ugomvi na ubaguzi, na vile vya kujiamini vinavyotuelekeza kukataa msaada wa wengine baada ya kukwaruzana nao.

Upendo huo kamili unadhihirika ikiwa, kati ya matatizo makubwa, tunampenda jirani kwa mawazo, maneno na matendo, yaani kwa kumpima kwa wema, kusema vema juu yake, kumsaidia katika shida, kumsamehe kwa moyo na kujifanya yote kwa wote. Unadhihirika zaidi tukiwaelekea hasa walioanguka na kupotea, ili kuwainua na kuwaelekeza tena njia ya mbinguni. Sifa kuu mojawapo ya upendo wa kishujaa kwa majirani ni hamu motomoto ya wokovu wao, kulingana na neno la Yesu msalabani, “Naona kiu” (Yoh 19:28). Huo upendo wa kishujaa uliwafanya watakatifu kadhaa wajiuze kama watumwa ili kukomboa waliotekwa na hivyo kuondoa familia zao katika ufukara. Ari hiyo ilidhihirika ndani ya Mt. Paulo hata akasema, “Ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli” (Rom 9:3-4). Ari hiyo ndiyo iliyochochea utendaji wa wamisionari bora.

Dalili nyingine ya upendo wa kishujaa kwa jirani ni wema wa kuwaenea wote kati ya matatizo makubwa, kadiri ya neno, “Heri wapatanishi” (Math 5:9), yaani wale ambao hawadumishi amani yao tu wakati wa vurugu, bali wanawashirikisha wengine na kuwatia moyo waliovurugika zaidi. Wema unaoenea, upendo kwa jirani unaofikia hatua ya kujitoa sadaka kila siku bila kutambulikana, ndiyo dalili ya hakika ya uwemo wa Mungu rohoni. Pengine wema huo unaelekeza kukosoa, lakini pasipo uchungu, wala ukali, wala utovu wa subira; na kusudi ukosoe vema unatokeza ndani ya yule anayestahili kukosolewa mema aliyonayo, yaliyo kama mbegu nzuri inayotakiwa kustawishwa. Hapo anayekosolewa anatiwa moyo akijiona anaeleweka na kupendwa. Bikira Maria angetutokea kutukosoa, angetuambia juu ya kasoro zetu kwa wema mkubwa hivi hata tungekubali mara maneno yake na kuchota humo nguvu ya kusonga mbele. Upendo huo kamili kwa jirani unatokana na muungano wa dhati na Mungu na kumfikisha jirani kwenye muungano huohuo. Kadiri mtu alivyoungana na Mungu, anamvutia wengine badala ya kujivutia tu. Ndani mwake unaelea wema wa Kimungu ambao unaenea, unavuta kwa nguvu na upole na hatimaye unashinda kizuio chochote. Upendo huo unaoshinda hivyo uovu, unawashirikisha watakatifu ushindi wa Kristo juu ya dhambi na shetani. Ni utukufu mmojawapo wa mwili wake wa fumbo; kwa njia yake unadhihirika ukuu wa uhai wa Kanisa, uzazi wake katika kila aina ya wema; ndiyo thibitisho la asili yake ya Kimungu.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. "SUMMA THEOLOGIAE: The object of charity (Secunda Secundae Partis, Q.25)". www.newadvent.org. Iliwekwa mnamo 2 Aprili 2018.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. "Catechism of the Catholic Church". usccb.org. Iliwekwa mnamo 2 Aprili 2018.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "SUMMA THEOLOGIAE: Charity, considered in itself (Secunda Secundae Partis, Q. 23)". www.newadvent.org. Iliwekwa mnamo 2 Aprili 2018.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Upendo kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy