Nenda kwa yaliyomo

Kitabu cha Yobu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kitabu cha Yobu kwa Kiebrania.
Wachokozi wa Jobu, mchoro wa William Blake (1793).
Jobu na Marafiki wake, mchoro wa Ilya Repin (1869).

Kitabu cha Yobu (kinaitwa pia Ayubu) ni kati ya vitabu vya hekima katika Biblia ya Kiebrania (Tanakh), hivyo pia cha Agano la Kale ya Biblia ya Kikristo.

Miongoni mwa aina nyingi za vitabu vya Biblia vipo hivyo vinavyojulikana kuwa vitabu vya hekima. Kati ya vitabu hivyo, pamoja na Yobu, kuna Methali na Mhubiri, ingawa hata baadhi ya Zaburi na sehemu za vitabu vingine pia vinaweza kuhesabiwa kuwa ni maandiko ya hekima. Tena, kati ya Deuterokanoni, vingi ni vitabu vya hekima.

Mtindo na mpangilio wa uandishi

[hariri | hariri chanzo]

Hakuna hakika kuhusu wakati wa kuandikwa habari za Ayubu wala haijulikani mwandishi wa kitabu chake alikuwa nani. Lakini kutojua mambo haya si kizuizi cha kuelewa ujumbe wa kitabu. Jambo muhimu ili kuelewa kitabu cha Ayubu si kumjua mwandishi wake au wakati wa kuandikwa kwake, bali jinsi kilivyoandikwa na muundo wake.

Ukitoa mwanzo na mwisho wake, kitabu hiki chenye sura 42 kiliandikwa namna ya shairi, na swali lake hasa ni: “Mbona Mungu aliye mwema anaruhusu mateso?”

Hadithi hii inasimulia mateso ya Yobu aliyemcha na kumwabudu Mungu vizuri kabisa. Hata hivyo mali yake yote ilipotea, watoto wake wote walikufa, na mke wake alimshauri kumlaani Mwenyezi Mungu. Yeye lakini hakufanya dhambi.

Alipotembelewa na marafiki watatu katika huzuni yake, walijadiliana naye sababu ya mateso. Sehemu kubwa ya kitabu inaleta majadiliano hayo.

Mwishoni, baada ya Elihu kuingilia kati, Mungu mwenyewe akamjibu Yobu kutoka katika dhoruba.

Inafaa tukisoma kitabu cha Ayubu sawasawa tunavyosoma vitabu vile vya Agano la Kale vyenye lugha ya mjazo wa masimulizi, maagizo ya haki au hotuba zenye wito. Hayo siyo kwa sababu kitabu kina alama za maandiko yenye hekima tulivyokwishaona, bali kwa sababu kiliandikwa kwa mtindo wake. Haya yanaonekana katika kitabu chote, yaani katika masimulizi ya mwanzo wa kitabu, katika mifululizo ya majadiliano na katika mwisho wake wa kuvutia sana.

Kama ilivyo katika utunzi wowote, msemo wake na aina ya utunzi wa maneno unastaajabisha wala maneno yake hayakukusudiwa kutafsiriwa moja kwa moja kila mara. Wala kitabu hiki hakikuandikwa ili kichunguzwe mstari kwa mstari, kwa sababu mara nyingine mstari mzima au hata mfululizo wa mistari kadhaa hutumiwa kueleza wazo moja tu la msingi. Mashairi ya Kiebrania kwa jumla, na hasa maandiko ya hekima ya Kiebrania, yalikuwa na maana ya pekee ambayo iliyafanya yatofautiane na maandiko mengine ya kawaida ya Agano la Kale.

Kwa kuelewa maana hiyo zaidi, kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Kumfahamu Ayubu

[hariri | hariri chanzo]

Ayubu alikuwa tajiri aliyesoma na kumcha Mungu. Aliishi katika nchi ya Usi iliyokuwa mashariki kwa Palestina. Alipopatwa na mfululizo wa maafa, marafiki zake walikazania kwamba shida zile lazima zilisababishwa na dhambi zake za siri. Ayubu alikataa maneno yao. Alijua kwamba hakuwa mtu mkamilifu, lakini pia alijua kwamba maoni ya kawaida ya desturi za nchi ile, kama yalivyoelezwa na marafiki zake, hayakueleza jambo lo lote. Majadiliano marefu yenye uchungu yaliyofuata yalijaza nafasi kubwa ya kitabu chote.

Elifazi (Ayubu 42:7) alikuwa ametoa mashtaka kwa Mungu kwamba watu humtumikia Mungu tu kwa sababu ya vitu wanavyoweza kupata kutoka kwake. Kama wangepata matatizo na shida wangemlaani (1:9-11; 2:4-5). Mungu akaruhusu maafa yaje juu ya Ayubu ili kupima uthabiti wa imani yake, na hivyo kuimarisha imani hiyo na kuongeza uzoefu wa Ayubu na Mungu (taz. Yak 5:11). Mateso ya Ayubu hayakuthibitisha hukumu ya Mungu juu yake, bali yalithibitisha matumaini yake katika Mungu na jinsi alivyomwamini.

Mkazo wa marafiki zake kwamba mateso au shida lazima vitokane na dhambi za mtu binafsi ulimfikisha Ayubu katika hali ambayo nusura ashindwe kuwavumilia zaidi. Lakini pia hali hiyo ilimsababisha amkaribie Mungu zaidi ambaye Ayubu alimwona kuwa tumaini lake pekee. Alipomlalamikia Mungu, inawezekana kuwa alikosa alipotumia lugha isiyostahili, lakini kwa hali yoyote alipeleka malalamiko yake kwa Yule aliyehusika.

Mwisho aliridhishwa, si kwa sababu maswali yake yote yalijibiwa, bali kwa sababu alikutana na Mungu ambaye alimlilia. Inawezekana kwamba Ayubu hakuelewa makusudi ya Mungu, lakini alijifunza kwamba Mungu huyo ambaye hekima yake ni kubwa sana kuliko ufahamu wa wanadamu, alistahili kutegemewa. Mungu hakuhitaji kujitetea kwa wanadamu, bali aliweza kufanya jambo lo lote alilopenda.

Mungu alipomthibitisha Ayubu, aliwaonyesha marafiki kwamba walikosa walipodai kwamba kila shida ni matokeo ya dhambi za mtu binafsi. Pia alionyesha kwamba Elifazi alikosa alipodai kwamba watu wanamwabubu Mungu tu, kwa sababu anawapa mambo mema na fanaka. Ayubu alidumu kuwa mwaminifu kwa Mungu, ingawa alipoteza kila kitu, lakini mwisho Mungu alimbariki kwa mibaraka mikubwa kuliko aliyokuwanayo hapo awali.

Muhtasari

[hariri | hariri chanzo]

1:1-2:13 Elifazi amjaribu Ayubu

3:1-14:22 Mfululizo wa kwanza wa mahojiano

15:1-21:34 Mfululizo wa pili wa mahojiano

22:1-26:14 Mfululizo wa tatu wa mahojiano

27:1-31:40 Mfululizo wa Ayubu

32:1-37:24 Hoja za Elihu

38:1-42:17 Jibu la Mungu

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Yobu kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy