Nenda kwa yaliyomo

Hatua ya muungano

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mozaiki ya karne ya 11 ya Maria akisali katika kanisa kuu la Hekima Takatifu huko Kiev, Ukraina. Ndiye kielelezo cha juu cha muungano na Mungu.

Hatua ya muungano ni ya juu kati ya tatu za safari ya maisha ya Kiroho kadiri ya waandishi wengi, hasa wa Kanisa Katoliki.

Hatua zinazotangulia ni ile ya utakaso na ile ya mwanga.

Baada ya hizo na za utakaso mchungu wa usiku wa roho, kuna aina ya ufufuko na mwanzo wa maisha mapya. Ndicho walichokionja Mitume wa Yesu siku ya Pentekoste ambapo, kisha kuondolewa ubinadamu wa Bwana wao, waligeuzwa kwa kuangazwa na kuimarishwa na Roho Mtakatifu wakahubiri Injili mpaka miisho ya dunia iliyojulikana wakaithibitishe kwa damu yao.

Kwa mtu aliyesoma taratibu za juu za ustawi wa neema inayotia utakatifu, wa upendo na wa vipaji vya Roho Mtakatifu, maneno ya watakatifu juu ya muungano huo hayashangazi: yanaonekana matunda bora yanayoundika ndani ya ua la upendo kwa athari ya dhati zaidi na zaidi ya mlezi wa ndani anayefundisha kwa mpako wake, pasipo kelele, akivuta kwa nguvu kubwa zaidi na zaidi.

Muungano wa fumbo ni tunda bora lakini la kawaida la uwemo wa Utatu Mtakatifu ndani mwetu, kwa kuwa Nafsi za Kimungu zinakaa ndani ya mwenye neema inayotia utakatifu kama katika hekalu ambamo zinaweza kujulikana, na pengine kweli zinajulikana kama kwa mang’amuzi kutokana na upendo wa kumiminiwa. Zinajitambulisha kama uhai wa maisha yetu, na huo ujuzi hai wa Nafsi tatu zilizomo mwetu pamoja na upendo huo wa kumiminiwa vinapokomaa ipasavyo vinaunda muungano halisi. Hivyo uwemo wa Utatu ndani mwetu ndio kiini ambacho maisha yote ya Kiroho yanatoka na kurudi. Ndio utimilifu wa maneno ya Mtume Yohane: “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:16). Hayo tuliyoyasema yanaonekana ya kweli zaidi tukimzingatia si huyu au huyu, bali binadamu alivyo na hasa neema ya maadili na vipaji ilivyo: si mbegu ya muungano wa fumbo tu, bali kwa kawaida ni pia mbegu ya heri ya kumuona Mungu.

Basi, tuone sifa kuu za hatua ya waliokamilika zinazoitofautisha na zile zilizotangulia. Hasa tunahitaji kuzingatia sifa za ujuzi wao juu ya Mungu na juu yao wenyewe na sifa za upendo wao.

Kumjua Mungu kama kwa mang'amuzi na kwa mfululizo

[hariri | hariri chanzo]

Waliokamilika wanamjua Mungu kama kwa mang’amuzi si ya mara kwa mara, bali karibu ya mfululizo. Wanamuelekea si wakati wa ibada au sala tu, bali pia nje yake, katikati ya shughuli; hawapotewi na uwepo wake, bali wanadumisha muungano wao naye. Mtu anayejipendea, ajue asijue, anajifikiria daima na kuhusisha yote naye mwenyewe; anaongea mfululizo na nafsi yake kuhusu tamaa zake, huzuni zake na furaha zake za juujuu; maongezi hayo ya ndani hayazai kitu. Kinyume chake, aliyekamilika anamfikiria mfululizo Mungu, utukufu wake na wokovu wa watu na kuelekeza yote huko, ajitambue asijitambue. Ndani mwake haongei tena na nafsi yake bali na Mungu, na maneno ya Injili yanamjia mara nyingi kuangazia maisha ya kila siku, matukio yoyote, ya furaha au ya huzuni. Anaimba utukufu wa Mungu na kueneza mwanga na joto la Kiroho anavyovipata mfululizo toka juu. Sababu ni kwamba hamtazami tena Mungu kama wanavyofanya wale wanaoanza, yaani kupitia vitu vinavyoonekana au mifano ya Injili, jambo ambalo haliwezi kufanyika mfululizo. Katika kivuli cha imani anatazama wema wenyewe wa Mungu, kwa mfano wa mwanga ambao unatuzunguka na kuangaza vyote.

Ni ujuzi wa wema mkuu unaoangaza yote; hapo mtu anaona kama kwa mang’amuzi kwamba Mungu amefanya yote, upande wa maumbile na upande wa neema, ili kuridhisha wema wake; tena kwamba akiacha baya litokee ni kwa kulenga jema kubwa zaidi. Kutokana na usahili wake wa hali ya juu, mtazamo huo wa Kiroho unaweza kudumu mfululizo, tena hauzuii kuona matukio yanayofuatana maishani, bali unayaona yote toka juu, kidogo kama anavyofanya Mungu, au kama mtu ambaye mlimani anaona yote yanayotokea bondeni. Mtazamo huo unaona vizuri ajabu maana ya dhati hata ya mambo madogomadogo muhimu. Hivyo unafuta kasoro zinazotokana na haraka ya kibinadamu, kujifanya lengo la yote bila kujitambua, na kukosa zoea la kujikusanya.

Yatokanayo ni kwamba waliokamilika wanajifahamu si ndani mwao tu, bali ndani ya Mungu, aliye chanzo chao na kikomo chao. Ndani mwake wanaona unyonge wao na umbali usiopimika unaowatenga na Muumba. Ni kama wanajisikia wakidumishwa na upendo wake wa hiari; wanang’amua mfululizo wanavyohitaji neema yake kwa tendo lolote la kuwaletea wokovu. Kwa makosa yao hawakati tamaa, bali wanajifunza unyenyekevu halisi. Wanajiona kwa unyofu watumishi wa bure, ambao peke yao hawawezi kitu, ila Bwana anaridhika kuwatumia atende makuu yanayoandaa uzima wa milele. Wakiona makosa ya jirani, wanafikiri hakuna dhambi ambayo wasingeweza kuitenda kama wangekuwa na urithi uleule na kuwekwa katika hali zilezile na vishawishi vilevile vya kwake. Kumbe wakiona maadili makubwa ya mwingine wanayafurahia kwa ajili ya Bwana na kwa ajili yake, wakikumbuka kwamba katika mwili wa Kristo kiungo hakiwezi kustawi viungo vingine visifaidike.

Mtazamo huo wa kumiminiwa unatokana na imani hai iliyoangazwa na kipaji cha hekima ambacho kwa uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu kinaonyesha hakuna linalotokea pasipo Mungu kutaka (kama ni jema) au pasipo Mungu kuacha litokee (kama ni baya la lazima kwa upatikanaji wa jema kubwa zaidi). Kutokana na usahili na upana wake, mtazamo wa juu hivi unaweza kuwa karibu wa kudumu, kwa maana matukio ya kila siku yanajipanga kama mafundisho ya kimatendo toka kwa Mungu mwema, na kama utekelezaji wa Injili katika maisha ya kila mmoja. Ni Injili inayozidi kuandikwa rohoni mwa watu hadi mwisho wa nyakati. Hapo Mkristo, kwa kujua ukamilifu wa Mungu na maadili ambayo ayatekeleze, ameacha nyuma si wazo la juujuu tu, bali wazo la teolojia pia, na kufikia wazo hai lenye utajiri wa mang’amuzi linalomuelekeza alitekeleze kwa faida ya watu. Ni wazo hai la wema usio na mipaka, la usahili kamili na la unyenyekevu halisi unaomfanya apende kuwa si kitu ili Mungu awe yote.

Kumpenda Mungu kwa roho yote

[hariri | hariri chanzo]

Hivyo aliyekamilika anafikia ule urafiki wa dhati na Bwana ulio lengo la upendo. Ni kutakiana mema na kuishi wawili pamoja katika ushirika wa Kiroho wa kudumu. Kama vile mwenye umimi akijifikiria mfululizo anajipenda vibaya katika vyote, aliyekamilika akimfikiria Mungu karibu mfululizo anampenda kwa kudumu, si tu kwa kukwepa dhambi na kuiga maadili ya Bwana, bali “kwa kuambatana naye, kumfurahia na kutamani kifo ili kuwa naye” (Thoma wa Akwino). Hilo ni tendo la moja kwa moja, sahili, ambalo linageuza utashi wetu na kuwa chanzo cha matendo yaliyofikiriwa. Kwa kweli aliyekamilika anajipenda ndani ya Mungu kwa kumpenda kuliko nafsi yake, na anatamani mbingu ili kutukuza milele wema wa Mungu, asili ya mema yote, kuliko kwa kupata heri yake binafsi. Ndio upendo safi wa Mungu na wa watu ndani mwake, ndiyo ari ya kitume, motomoto kuliko awali, lakini pia nyenyekevu, tamu, vumilivu. Aliyekamilika hainukii mara kwa mara tu kilele hicho cha roho, bali ni kana kwamba amehamia humo, amekuwa mtu wa Kiroho na wa Kimungu anayeabudu katika Roho na ukweli. Kwa hiyo anadumisha amani karibu mfululizo, hata katika hali za kusikitisha na zisizotarajiwa, na mara nyingi anaishirikisha hata kwa watu waliovurugika zaidi. Ndiyo sababu heri ya wenye amani inahusiana na kipaji cha hekima ambacho, pamoja na upendo, kinawatawala moja kwa moja.

Ndizo sifa za hatua hiyo: kuongea kwa ndani karibu mfululizo na Mungu anayependwa kwa usafi kuliko vyote na kwa hamu hai ya kufanya ajulikane na kupendwa.

Uwemo wa Utatu Mtakatifu katika roho iliyotakata

[hariri | hariri chanzo]

Mbinguni Nafsi tatu za Mungu wanaishi katika roho iliyotakata kama katika hekalu ambamo wanajulikana na kupendwa. Utatu Mtakatifu unaonekana wazi ndani mwa roho hiyo unayoidumisha katika uhai na katika neema isiyoweza kupotezwa. Hivyo kila mwenye heri ni kama tabenakulo hai, kama hostia iliyogeuzwa, tena yenye ujuzi na upendo upitao maumbile. Utangulizi wa hali hiyo unapatikana duniani katika mtu aliyekamilika aliyefikia muungano unaotugeuza tutakaouzungumzia mbele. Kwa sasa tuseme kuwa muungano huo wa dhati ni wa nadra lakini si nje ya utaratibu wa kawaida, kwa sababu ni mwendelezo wa uwemo wa Utatu Mtakatifu ndani ya kila mwadilifu. Uhai unaoletwa na neema inayotia utakatifu ni mbegu ya utukufu; kimsingi ni uhai uleule wa milele. Ikiwa mbinguni Utatu Mtakatifu umo rohoni mwa mwenye heri ambamo unaonekana bila kizuio, ni lazima uwemo tayari ndani ya mwadilifu katika giza la imani, ukijulikana na kama kung’amuliwa naye kadiri alivyotakata. Kama vile roho inavyojing’amua kuwa asili ya matendo yake, inajaliwa pia kumtambua Mungu kama asili ya matendo yapitayo maumbile ambayo isingeweza kuyasababisha pasipo uvuvio maalumu toka juu. Kadiri mtu alivyotakata, anatofautisha ndani mwake yale yanayotokana naye kwa msaada wa kawaida wa Mungu, na yale yanayotokana na uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu.

Utambuzi huo wa uwemo wa Mungu unategemea hasa kipaji cha hekima kinachotufanya tupime mambo ya Kimungu kwa kulingana nayo, kwa hisi ipitayo maumbile inayotegemea upendo, na kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu anayetumia hisi hiyo aliyotutia ili tumtambue. Hivyo tunaonja mafumbo ya wokovu na uwemo wa Mungu ndani mwetu kwa mfano wa wanafunzi wa Emau walioambiana, “Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia Maandiko?” (Lk 24:32). Ni ujuzi ambao unafanana na mang’amuzi, unapita mifuatano ya mawazo na kulingana na ule wa roho inayojifahamu kama asili ya matendo yake. Mungu, asili ya neema na ya wokovu, yumo ndani mwetu kuliko sisi wenyewe, naye anatuvuvia tutende mambo ya dhati tusiyoyaweza peke yetu, na ndivyo anavyojitambulisha kwetu kama chanzo cha maisha ya Kiroho.

Ujuzi huo unafanana tu na mang’amuzi kwa sababu mbili: 1) haumfikii Mungu moja kwa moja, inavyotokea kwa kumuona mbinguni, bali katika tendo la upendo wa kitoto analolisababisha ndani mwetu; 2) hatuwezi kutofautisha kwa hakika matendo hayo ya upendo yapitayo maumbile na miruko ya moyo wetu inayofanana nayo: hivyo tusipojaliwa ufunuo maalumu hatuwezi kuwa na hakika ya mia kwa mia ya kwamba tuna neema inayotia utakatifu.

Uwemo wa Utatu Mtakatifu unadumu hata usingizini, mpaka tunapodumu kuwa tumeunganika na Mungu kutokana na hali ya neema. Lakini ni wazi kuwa muungano huo wa kawaida unalenga muungano tunaouzungumzia sasa, hata ule wa dhati zaidi unaotugeuza. Basi, katika roho iliyotakata inazidi kuonekana hali ipitayo maumbile ya kufanana na Mungu. Roho kwa umbile lake inayo tayari sura ya Mungu, kwa kuwa si mwili na inaweza kujua na kupenda. Kwa neema inayotia utakatifu, asili ya maadili ya Kimungu, inaweza pia kumjua na kumpenda Mungu kwa namna ipitayo maumbile. Kadiri neema hiyo na upendo vinavyokua vinatutenganisha na mambo ya chini na kutuunganisha na Mungu. Hatimaye mbinguni neema kamili itatuwezesha kumuona moja kwa moja anavyojiona na kumpenda anavyojipenda. Hapo hali ya kufanana naye itakamilika, upendo usioweza kupotezwa utatufananisha na Roho Mtakatifu aliye upendo-nafsi; heri ya kumuona Mungu itatufananisha na Neno ambaye akiwa uangavu wa Baba atatufananisha naye. Kutokana na hayo tunaelewa unavyotakiwa kuwa tangu hapa duniani muungano kamili ambao ni utayari wa moja kwa moja wa kujaliwa heri ya kumuona mara baada ya kufa bila kupitia toharani. Ndiyo siri ya maisha ya watakatifu. Pengine hali hiyo ipitayo maumbile ya kufanana na Mungu na Yesu inadhihirika mwilini pia.

Dalili za Utatu Mtakatifu kuwemo katika roho iliyotakata

[hariri | hariri chanzo]

Dalili hizo zilitajwa na Thoma wa Akwino alipojiuliza kama mtu anaweza kujua ana hali ya neema. Ingawa hazimwezeshi kuwa na hakika ya imani juu ya hali hiyo, zinamwezesha kukaribia meza ya Bwana bila kuogopa kukufuru. Zile muhimu zaidi zinaorodheshwa kama ifuatavyo kuanzia zile za chini.

1) Ushuhuda wa dhamiri njema isiyojisikia kuwa na dhambi yoyote ya mauti. Ndiyo dalili ya msingi inayodaiwa na zile ambazo zinaifuata na kuithibitisha.

2) Furaha ya kusikia Neno la Mungu, si kwa kulisikiliza tu, bali kwa kulitekeleza.

3) Kuonja hekima ya Mungu hata kujisomea Injili ili kutafuta roho yake ndani ya maneno na kujilisha hata kuhusu fumbo la msalaba, ukiwa ni pamoja na ule wa kuubeba siku kwa siku.

4) Elekeo la kuongea na Mungu kwa ndani, na kuanza tena maongezi hayo yakikatika. “Urafiki unamuelekeza mtu atake kuongea na rafiki yake. Maongezi ya mtu na Mungu yanafanyika kwa kumkazia macho katika sala ya kumiminiwa, kadiri ya maneno ya mtume Paulo, ‘Sisi wenyeji wetu uko mbinguni’ (Fil 3:20). Kwa kuwa Roho Mtakatifu anatutia upendo wa Mungu anatuelekeza vilevile kumtazama. Ndiyo sababu mtume alisema pia, ‘Sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho’ (2Kor 3:18)” (Thoma wa Akwino). Kabla ya hayo, mwalimu huyo wa Kanisa aliandika kuwa maongezi ya ndani na Mungu ni kama ufunuo wa mawazo ya siri zaidi, kwa maana sisi hatuna cha kumficha, naye anatukumbusha maneno ya Injili yanayotuonyesha yale yote yanayotupasa dakika kwa dakika. Ndiyo matokeo ya urafiki ambao “kwa namna fulani unaunganisha mioyo miwili kuwa mmoja, hivi kwamba tunachomfunulia rafiki halisi tunaona hakijatutoka”.

5) Kumfurahia Mungu, kwa kukubali kwa dhati matakwa yake hata katika mapingamizi. Pengine wakati wa kuvunjika moyo tunatiwa furaha safi na ya juu inayoondoa huzuni yoyote. Hiyo ni dalili kubwa ya kutembelewa na Bwana. Yesu alipomuahidi Roho Mtakatifu alimuita Mfariji. Kwa kawaida tunamfurahia kadiri tunavyotimiza amri zake, kwa kuwa hivyo tunazidi kuwa moyo mmoja naye.

6) Uhuru wa wana wa Mungu. “Wana wa Mungu wanaongozwa na Roho Mtakatifu si kama watumwa, bali kama viumbe huru… Roho Mtakatifu anatufanya tutende akiongoza utashi wetu wenye hiari utake, kwa sababu anatufanya tumpende Mungu na anatuelekeza tutende kwa upendo wake, si kwa hofu kama watumwa” (Thoma wa Akwino). “Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Rom 8:15-16). “Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru” (2Kor 3:17), yaani ukombozi kutoka utumwa wa dhambi. “Kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi” (Rom 8:13). Ndio ukombozi halisi, yaani uhuru mtakatifu wa wana wa Mungu wanaotawala pamoja naye juu ya tamaa, juu ya roho ya ulimwengu na juu ya uovu.

7) Kumzungumzia Mungu kama kwa kufurika toka moyoni. Kwa namna hiyo “mahubiri yanatakiwa kutokana na ukamilifu wa kuzama katika mafumbo ya imani” (Thoma wa Akwino). Roho Mtakatifu anazidi kujitokeza kwetu kama chemchemi ya neema mpya daima, “chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele” (Yoh 4:14), chemchemi isiyokwisha ya mwanga na upendo. Ndiyo faraja yetu kati ya huzuni za hapa uhamishoni. Katika matatizo ya kimataifa ya wakati huu, linadumu tumaini kubwa, kwa kuwa mkono wa Bwana haujafupika. Tunaona alivyo mwingi wa huruma daima katika watakatifu anaozidi kuwaleta ulimwenguni. Ndio watumishi wake wakuu wenye mifano bora ya imani, tumaini na upendo, ambayo mingi tunaweza kuifuata.

Kwa msimamo huo inafaa wanaoishi Kiroho wajiweke wakfu kwa Roho Mtakatifu ili kuongozwa naye zaidi kwa kutambua na kufuata minong’ono yake, kama vile wanavyojiaminisha kwa Maria ili awaongoze kwa Mwanae, na wanavyojiweka wakfu kwa Moyo mtakatifu wa Yesu awafikishe kwa Baba yake.

Upendo kwa Msulubiwa na kwa Maria katika hatua ya muungano

[hariri | hariri chanzo]

Teresa wa Yesu aliandika hivi juu ya watu waliofikia makao ya sita, “Mnaweza mkadhani kwamba hao wanaofurahia matamu hayo ya hali ya juu hawapaswi tena kutafakari mafumbo ya ubinadamu mtakatifu sana wa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwamba kazi yao ni kupenda tu… Tutawezaje kusogea kwa hiari mbali na yule aliye hazina na dawa yetu pekee?… Yesu alisema kuwa ndiye njia. Alisema pia kuwa ndiye mwanga na kwamba hakuna mtu aendaye kwa Baba ila kwa njia yake. Na kweli wale ambao Bwana amewaingiza katika makao ya saba karibu hawatenganiki kamwe na Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa namna ya ajabu, yupo nao kiaminifu kwa ubinadamu wake na umungu wake kwa pamoja... Maisha ni marefu na tunakabiliana na tabu nyingi. Ili tuzivumilie inavyofaa tunahitaji kuzingatia jinsi kielelezo chetu Yesu Kristo, mitume na watakatifu walivyozivumilia. Urafiki wa Yesu mwema ni bora: basi tusijitenge naye wala na Mama yake mtakatifu… Narudia tena, wanangu, muangalie: njia hiyo ni ya hatari. Shetani anaweza akatufikisha hadi kupotewa na ibada kwa sakramenti kuu”.

Ushindi wa Kristo na uenezi wake

[hariri | hariri chanzo]

“Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida… Ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo” (Fil 1:21,23). Kama vile vita ndiyo maisha ya askari, na elimu ndiyo maisha ya msomi, Kristo amekuwa daima maisha ya watakatifu wote, lengo la kudumu la upendo wao na chemchemi ya nguvu zao. “Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu… Maana naliazimu nisijue neno lolote kwenu, ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa” (1Kor 1:22-24; 2:2). “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake, aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu… Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef 1:18-20; 3:17-19). Watakatifu wote waliishi hadi mwisho kwa kuzamia mateso ya Yesu msulubiwa, hasa wale waliolingana naye zaidi.

Katika hatua ya muungano zinazidi kudhihirika hazina zisizopimika za roho ya Mwokozi, za akili yake, za utashi wake na za hisi zake. Unazidi kugundulika utakatifu wake wa asili, wa dhati, usioumbwa, unaoundwa na Nafsi yenyewe ya Neno inayomiliki kwa ndani na moja kwa moja roho yake na mwili wake. Inazidi kueleweka thamani ya ukamilifu wa neema, wa mwanga na wa upendo ulioenea rohoni mwake kutokana na Neno; ukamilifu ambao ulikuwa chemchemi ya amani kuu na heri timilifu tangu duniani hapa, na kwa wakati huohuo ulisababisha ukali wa mateso ya Kristo kuhani na sadaka, kwa sababu mateso yake kwa dhambi za watu alizozibeba yalikuwa na ukuu uleule wa upendo wake kwa Baba aliyechukizwa nazo na kwetu sisi aliokuja kutukomboa.

Katika hatua ya muungano mtu anazidi kuelewa ushindi mkuu alioupata Kristo katika mateso yake hadi msalabani; ushindi juu ya dhambi na shetani uliodhihirika siku ya tatu kwa ushindi juu ya kifo. Ushindi huo unazidi kueleweka unavyotokana na tendo la upendo wa Mungu-mtu ambalo katika Nafsi ya Kimungu ya Neno lilichota thamani yake isiyo na mipaka kwa kutoa fidia na kutustahilia uzima wa milele. Tendo hilo “lilimpendeza Mungu kuliko yalivyomchukiza maovu yote pamoja” (Thoma wa Akwino) kwa kuwa lilitokana na Nafsi ya Mwana aliye sawa na Baba na kustahili kuliko jumla ya stahili zote za malaika na za binadamu. “Jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yoh 16:33); katika nafasi ngumu na za dhuluma ni faraja iliyoje kwetu kufikiri kwamba Msulubiwa ameshapata ushindi wa moja kwa moja na kwamba upande wetu tunapaswa tu kujitoa kwake ili atushirikishe. Duniani mapambano yanaendelea, lakini ushindi umeshapatwa na Kichwa cha mwili wa fumbo ambao sisi ni viungo vyake. Hapo ibada kwa mateso ya Mwokozi inazidi kuwa ibada kwa Kristo mtukufu.

Katika hatua ya muungano yanazidi kueleweka aliyoyasema Thoma, “Mungu anapenda zaidi yaliyo bora, kwa kuwa upendo wake ndio chemchemi ya mema yote, hivyo kiumbe kisingekuwa bora kuliko kingine kama kisingependwa zaidi na Mungu. Kwa hiyo Mungu anampenda Kristo si tu kuliko binadamu wote, bali kuliko viumbe vyote pia, kwa kuwa alimtakia mema makuu zaidi na kumkirimia jina lile lipitalo kila jina akimjalia kuwa Mungu kweli. Ubora wa Mwokozi haupunguzwi na ukweli kwamba Mungu alimtoa afe kwa wokovu wetu. Kinyume chake Yesu amekuwa hivyo mshindi mtukufu”.

Kwa namna hiyo inaeleweka zaidi sababu gani Mungu aliacha itukie dhambi asili na matokeo yake. “Mungu haachi mabaya yatokee isipokuwa kwa ajili ya mema makubwa zaidi. Ndiyo maana mtume Paulo aliandika, Dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi (Rom 5:20). Nalo Kanisa linapobariki mshumaa wa Pasaka linaimba, Lo! Kosa lenye heri, lililostahili kumpata Mwokozi mkuu kama huyo!” (Thoma wa Akwino). Kifo cha Yesu msalabani ndio ufunuo mtukufu zaidi wa huruma na uweza wa Mungu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee” (Yoh 3:16). Hayo yote yanazidi kuwa wazi kwa mtu aliyemiminiwa sala na yanamfanya aone pia kila siku zaidi thamani isiyopimika ya sadaka ya misa ambayo inadumisha ile ya msalabani na kutushirikisha matunda yake.

Heshima kwa Maria katika hatua ya muungano

[hariri | hariri chanzo]

Ili kupenya zaidi fumbo la Kristo mtu aliyemiminiwa sala anatakiwa kumuomba Maria, inavyothibitishwa na liturujia, k.mf. katika sekwensya ya Mama wa Mateso: “Mama kwa upendo wako / Nijulishe teso lako / Nililie na wewe. / Ewe, washa moyo wangu / Kwa kumpenda Yesu Mungu, / Ili nimwelekee. / Yesu Bwana kifo chake, / Teso lake nishike, / Wazie majeraha. / Nijeruhi kama Yeye, / Msalabani unilevye, / Kwa damu ya Mwanao”. Ndiyo sala ya mtu anayetamani kujua donda la upendo na kushirikishwa mafumbo ya uchungu kwa kuabudu na kufidia, kama walivyofanya Mt. Yohane na Mt. Maria Magdalena karibu na Maria huko Kalivari, na pia Mt. Petro alipomwaga machozi mengi. Machozi hayo ya majuto na ibada tungependa kuyamwaga daima kwa sababu kadiri tunavyosikitikia chukizo tulilomtendea Mungu, tunafurahia sikitiko hilo: “Aliyetubu asikitike daima pamoja na kufurahia sikitiko lake” (Augustino). Ndivyo inavyosema sekwensya hiyo pia, “Mimi nawe nimlilie, / Msulibiwa huzunie, / Maisha yangu yote. / Natamani kusimama / Msalabani nawe Mama, / Niomboleze nawe”.

Tusiache chemchemi hizo zibubujike bure: kutoka madonda ya Kimungu yanatiririka yale maji hai tunayopaswa kuyanywa kwa wingi. Katerina wa Siena, aliyejaliwa mara kadhaa kunywea donda la moyo wa Yesu, hakuchoka kusisitiza thamani ya damu yake. Bwana atuinue hadi Moyo wake mtakatifu tunaposhiriki sadaka ya misa na kukaribia meza yake. Kuzama hivyo katika stahili zisizo na mipaka za Mwokozi ni sehemu ya njia ya kawaida ya utakatifu; bila kufanya hivyo hatuwezi kupenda msalaba, ambako kimsingi ni kumpenda motomoto Yesu msulubiwa. Ndiyo njia ya kifalme ya kuendea mbinguni.

Mtu fulani aliyejaribiwa kuliko kawaida aliandika, “Nimetegemezwa mara nyingi na neno la Kimungu la Mwokozi, ‘Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu’ (Yoh 16:33). Ushindi wake wa moja kwa moja, ambao unaangaza malimwengu kwa nuru ya faraja kubwa, unanitia furaha isiyosemekana. Ninapojisikia kuangamia, nikiinua macho kwa Mwalimu mwema na kumnong’onezea kwa huzuni, ‘Bwana, nahitaji furaha!’, basi naona ushindi wake wa fahari mwishoni mwa nyakati, na mwanga huo kutoka juu unaangaza giza nene la usiku na kuleta utulivu kati ya dhiki zozote. Ni kana kwamba kutoka pwani ningeona kupita mikondo ya maji ya kutisha. Duniani mambo yanakwenda vibaya hivi! Misingi ya ulimwengu inatikisika, lakini yeye habadiliki, anabaki daima mwema tu!” Tukimfuata hivyo hatutatembea gizani kamwe, bali tutazidi kupokea mwanga wa uzima.

Namna mbalimbali za hatua ya muungano

[hariri | hariri chanzo]

Hatuwezi kupata picha halisi ya hatua ya muungano tusipoongea juu ya namna zake mbalimbali kama vile maisha kamili ya kitume yalito tunda la kuzama katika mafumbo, halafu maisha ya malipizi.

Tutaweza tu kuripoti kifupi tunayoyaona muhimu zaidi katika ushahidi wa watakatifu. Sisi ni kama watazamaji ambao, tukiwa bado bondeni, tunaangalia wanaopanda hadi kilele cha mlima.

Maisha kamili ya kitume

[hariri | hariri chanzo]

Haifai tuzungumzie muungano wa dhati na Mungu bila kusema juu ya matunda yake katika maisha kamili ya kitume yanayounganisha sala ya kumiminiwa na utendaji. Ni lazima tudumishe uwiano na umoja wa pande hizo mbili kwa kulingana iwezekanavyo na maisha ya Bwana na ya mitume wake.

Chemchemi ya juu ya utume

[hariri | hariri chanzo]

Katika hotuba ya Mtume Petro siku ya Pentekoste, na katika barua za Mtume Paulo, tunakuta Neno la moto likiongozwa na uvuvio wa Mungu. Mababu wa Kanisa ili wawaokoe watu waliwalisha matunda ya sala waliyomiminiwa. Kuzama kwa upendo katika mafumbo ni bora kuliko vitendo vya toba na kuliko masomo: ndiyo roho ya utume. Mtume yeyote awe anashirikisha mang’amuzi yake ya sala ya kumiminiwa ili kuwatakasa na kuwaokoa watu, kadiri ya maneno ya Thoma wa Akwino: “Kuzama katika mafumbo na kuwashirikisha wengine yaliyotazamwa hivyo”. Ili maisha hayo yadumu kuwa na umoja, sala ya kumiminiwa na utendaji haviwezi kuwemo katika msingi wa usawa; ni lazima kimoja kiwe chini ya kingine, la sivyo vitadhuriana na hatimaye itabidi kuchagua kimojawapo tu. Wengi, wajue wasijue, wanapotosha fundisho la mapokeo, wakisema maisha ya kitume lengo lake kuu ni utendaji wa kitume, ila yanalenga pia sala kama chombo cha lazima kwa ajili ya utendaji. Lakini je, kweli mitume na wamisionari watakatifu, k.mf. Fransisko Saveri, waliona kuzama kwa upendo katika mafumbo ya imani ni chombo tu kinacholenga utendaji? Je, kweli Yohane Maria Vianney alitazama hivyo sala na misa? Kudhani hivyo ni kupunguza umuhimu wa muungano na Mungu, ulio chemchemi ya utume wowote. Kwa mtazamo huo, ambao pengine hautokezwi wazi, ungefikiwa uzushi wa kupindua mpangilio wa upendo kwa kusema ule kwa jirani ni wa juu kuliko ule kwa Mungu.

Kuzama katika mafumbo yake na hivyo kuungana naye hakuwezi kuwa njia ya kulenga utendaji, kwa sababu ni jambo la juu zaidi. Duniani hakuna lolote la juu kuliko kuungana na Mungu kwa sala ya kumiminiwa na upendo: “Kwa umbile lake maisha ya sala hasa yanatangulia yale ya utendaji, kwa sababu yanalenga mambo makuu na bora, halafu yanasukuma na kuongoza katika maisha ya utendaji” (Thoma wa Akwino). Utume hauna thamani kubwa usipotokana na chemchemi hiyo kama sababu ya juu. Tena wenyewe ni njia inayolenga muungano na Mungu tunaotaka kuwafikishia watu. Kwa hiyo tunapaswa kulenga hasa kuzama katika mafumbo ambako kunazaa utume.

Yesu Kristo hakuridhika na maisha ya sala tu, bali alichagua yale ambayo yanatokana na utajiri wa sala ya kumiminiwa na yanashuka kuwashirikisha watu kwa njia ya mahubiri. Uhusiano wa kuzama katika mafumbo na kutenda unafanana na ule wa umwilisho na ukombozi. Umwilisho wa Neno hauhusiani na ukombozi wetu kama njia ya chini inavyolenga shabaha ya juu, bali kama sababu ya juu inayoleta tokeo la chini. Tangu milele Mungu alipanga umwilisho si kwa kulenga ukombozi bali kwamba uzae ukombozi. Vivyo hivyo alipanga maisha ya kitume yawe na sala ya kumiminiwa na muungano na Mungu si kwa kulenga utendaji, bali kwamba vizae matunda katika utume.

Ni lazima utume utokane na kuzama katika mafumbo ya wokovu ili mahubiri na uongozi wa roho viwe viangavu, hai, sahili, vyenye hakika ya dhati ambayo inachoma na kuvutia mioyo. “Anayewaletea wengine neno la Mungu anatakiwa kuwaelimisha, kuivuta mioyo yao kwa Mungu na kuchochea utashi wao watekeleze sheria yake” (Thoma wa Akwino). Inatakiwa iwe hivyo ili mahubiri yasishirikishe herufi tu, bali roho ya Neno la Mungu, ya mafumbo yapitayo maumbile, ya amri na ya Mashauri ya Kiinjili. Si suala la miguso ya juujuu, bali la uvuvio wa ukweli wa Mungu unaotokana na imani kubwa na upendo motomoto kwa Mungu na kwa watu.

Ili tuelewe mahubiri ya Injili yanavyotakiwa kuwa, tukumbuke kwamba sheria mpya si Maandiko kwanza, bali sheria iliyomiminwa rohoni, yaani neema ya Roho Mtakatifu. Ili tuishi kwa neema hiyo ilibidi tuelimishwe kwa maneno ambayo yalitamkwa na kuandikwa kuhusu mafumbo ya kusadikiwa na amri za kutekelezwa. Mahubiri ya Injili yanatakiwa kuwa roho na uzima; ili mtume asikate tamaa katika mapingamizi yote anayopambana nayo ni lazima awe na njaa na kiu ya haki ya Mungu, awe na kipaji cha nguvu aweze kudumu mpaka mwisho na kuvuta watu. Hizo njaa na kiu zinakua katika liturujia na sala ya moyo. Hasa adhimisho la misa, pamoja na muungano na Mungu unaopatikana humo, ndio kilele ambapo ububujike mto wa mahubiri hai ya Neno la Mungu. Ili awe “Kristo mwingine”, padri anatarajiwa kuzama katika sadaka ya msalaba inayodumu kutolewa altareni. Huko kuzama kuwe roho yenyewe ya utume inayofanana na chemchemi hai daima zinazotiririsha mito mikubwa. Kifupi ni kwamba, ili tuwalete wengine kwa Mungu ni lazima kwanza tuwe tumeungana naye kwa dhati.

Masharti na matunda ya utume

[hariri | hariri chanzo]

Matunda ya utume yanatakiwa kuwa uongofu wa wasio Wakristo na wa waamini wakosefu pamoja na maendeleo ya waadilifu: kwa jumla, ni wokovu wa roho. Lakini kwa ajili hiyo Bwana hakuridhika kuhubiri ukweli, bali alikufa msalabani. Vivyo hivyo mitume hawawezi kuokoa watu kwa mahubiri tu, bila kuteseka kwa ajili yao. “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; sikuzote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu” (2Kor 4:8-10). Mwenyewe, alipowaahidia mara mia wale wanaomfuata aliwatabiria dhuluma za namna hiyo (taz. Mk 10:30).

“Kama vile Bwana wetu alivyotimiza ukombozi wa ulimwengu kwa msalaba wake tu… hata watenda kazi ya Injili wanagawa tu neema za ukombozi kwa msalaba wao na kwa dhuluma zinazowatesa. Kwa hiyo hakuna cha kutumainia kutokana na huduma yao isipoendana na mapingamizi, masingizio, matusi na mateso. Baadhi wanadhani kutenda maajabu kwa sababu mahubiri yao yametungwa vizuri, wanayatoa kwa ufasaha, wanasifiwa na kupokewa vema kila mahali. Lo! Wanavyodanganyika! Njia wanazozitegemea si zile ambazo Mungu anazitumia ili kutenda makuu. Ili kuokoa ulimwengu inahitajika misalaba. Mungu anaongoza katika njia ya msalaba wale anaowatumia kuokoa watu” (Alois Lallemant). Wamisionari wengi waliuawa kikatili, na damu yao ikawa mbegu ya Wakristo wapya! Uhai wa Kanisa, kama ule wa mwanzilishi wake umepitia mautini na hivyo unadumu kuwa na nguvu na kuzaa matunda yasiyoisha.

Kwamba utume unatakiwa “utokane na utimilifu wa sala ya kumiminiwa” (Thoma wa Akwino) ni uthibitisho mwingine wa kwamba, kuzama katika mafumbo kwa imani hai iliyoangazwa na vipaji vya Roho Mtakatifu ni katika njia ya kawaida ya utakatifu, hasa kwa padri anayetakiwa kuongoza watu, kuwaangaza na kuwafikisha kwenye ukamilifu.

Maisha ya malipizi

[hariri | hariri chanzo]

Kuhusu muungano wa waliokamilika na Mungu tunapaswa bado kuzungumzia walau kidogo maisha ya malipizi, ambayo ni utume unaofanyika kwa sala na sadaka ili utume wa Neno uzae matunda mengi. Bwana wetu aliokoa ulimwengu kwa upendo wake wa kishujaa msalabani kuliko kwa mahubiri yake. Maneno yake yametuangaza na kuelekeza njia, lakini kifo chake ndicho kilichotupatia neema ya kuifuata. Maria, anayeitwa pengine mkombozi mshiriki na mgawaji wa neema zote, ndiye kielelezo cha wanaoishi kwa kufidia dhambi za watu. Kwa uchungu wake chini ya msalaba ametustahilia kwa msingi wa urafiki wake na Mungu yale yote ambayo Neno aliyefanyika mwili ametustahilia kwa msingi wa haki. Hivyo akawa mama wa Kiroho wa binadamu wote.

Katika misa sadaka ya Yesu haifanyiki kwa mateso mapya kama pale msalabani, ila mateso yake yanatakiwa kuendelea katika mwili wake wa fumbo, na kweli yataendelea hadi mwisho wa dunia. Kwa kuwa Yesu akizidi kuwaunganisha naye waamini anaowahuisha, anachapa ndani mwao chochote cha mafumbo ya furaha, mwanga na uchungu ya maisha yake kabla hajawashirikisha utukufu wake mbinguni. Kwa lengo hilo anawashirikisha kazi yake ya kuokoa watu, waifanye pamoja naye, kwa ajili yake na ndani mwake wakifuata njia zilezile alizozifuata mwenyewe. Kwa maana hiyo Mt. Paulo aliandika, “Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu, tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake” (Kol 1:24). Kwa yenyewe mateso ya Kristo hayapungukiwi kitu, kwa kuwa thamani yake haina mipaka kutokana na Nafsi ya Kimungu ya Neno; kilichopungua ni kiasi cha uenezi wake ndani mwetu. Ndio utume mkuu wa mateso unaowashirikisha watakatifu uchungu wa Mwokozi na neema ya kuitia kazi yao mhuri alioitia kazi yake msalabani.

Maisha ya malipizi ya padri

[hariri | hariri chanzo]

Padri anatakiwa kuwa “Kristo mwingine” kwa namna ya pekee. Yesu ni kuhani na kafara, naye padri hawezi kushiriki ukuhani wa Kristo asishiriki hali yake ya kuwa kafara kadiri alivyopangiwa na Mungu. Ndivyo walivyoelewa mapadri watakatifu, k.mf. Yohane Maria Vianney ambaye wakati wa kutolea mwili na damu takatifu ya Bwana alikuwa anatolea mateso yake yote kwa ajili ya waamini waliomuendea. Charles wa Foucauld, aliyeutia mhuri wa damu utume wake kati ya Waislamu, aliandika maneno yafuatayo katika daftari alilolichukua daima ndani ya mavazi yake, “Ishi kana kwamba leo ni siku yako ya kufia dini. Kadiri tunavyokosa vyote duniani, tunakikuta kitu bora zaidi ambacho dunia inaweza kutupatia, yaani msalaba”.

Maisha ya malipizi ya wanaopaswa kubeba msalaba mzito

[hariri | hariri chanzo]

Mkristo yeyote anapaswa kubeba “msalaba wake kila siku” (Lk 9:23) na kuunganisha mateso yake na sadaka ya Yesu inayozidi kutolewa altareni: anapaswa kuyatoa kwa ajili yake na ya watu anaoshughulikia wokovu wao. Kwa mfano wa Maria, mabibi arusi wengi wa Kristo wanashiriki mateso yake na hivyo kuwa mama wa Kiroho kwa wale wote waliokombolewa na damu ya Mwanae. Maria hakutiwa rohoni alama isiyofutika ya upadri lakini “alijaliwa ukamilifu wa roho ya kipadri” (M. Olivier) yaani roho ya Mkombozi. Alipenya fumbo la altareni kuliko Mtume Yohane aliyeadhimisha misa mbele yake na kumkomunisha. Alistawisha utume wa Thenashara akijitoa pamoja na sadaka ya misa. Kwa mateso yake ya ndani, kama yale yaliyompata uzushi ulipoanza kujitokeza, alikuwa mama wa Kiroho wa watu kwa kiwango kisichofikirika pasipo mang’amuzi ya dhati ya utume huo uliofichika. Kwa namna hiyo aliendeleza sadaka ya Mwanae.

“Mwili wa fumbo wa Kristo hauwezi kuishi pasipo mateso, kama vile macho yetu yasivyoweza kuishi bila mwanga wa jua. Hapa chini kadiri mtu alivyo karibu na Mungu, yaani kadiri anavyompenda, anawekwa wakfu kwa mateso. Kwa watu waliopata yote kwa njia ya Kanisa, je, si wito bora kuishi na kujitoa sadaka kwa ajili ya Mama yao?… Inahitajika subira, lakini nitaipata: Bwana wetu atanipatia… Namuambia daima: ‘Namtaka mtu huyu kwa gharama ya mateso yoyote’… Hadi mwisho wa dunia Kristo atateseka katika viungo vyake, na kwa mateso hayo Kanisa, Bibi arusi wake, litazaa watakatifu… Tangu Yesu afe, sheria haijabadilika: watu wanaokolewa tu kwa kuteseka na kufa kwa ajili yao… Moyo wa Yesu uliotukuzwa milele hautateseka tena kwa sababu hauwezi kuteseka tena. Sasa ni zamu yetu… Ni heri iliyoje kwamba kuteseka ni zamu yetu, si zamu yake tena!” (Fransiska wa Yesu).

Bwana anawaambia watu wa malipizi kama sista huyo aliyeishi miaka kadiri ya kweli hizo, “Je, hujaniomba kushiriki mateso yangu? Chagua: unataka furaha ya imani isiyo na vivuli, ambayo ikupate na kukujaza matamu, au unataka giza na uchungu ili uchangie kuokoa watu?” Anawaalika waamue kwa hiari tu; lakini wao, wakivutwa na nguvu isiyoshindikana, wanajichagulia uchungu na giza lote ili wengine wapewe mwanga, utakatifu na wokovu. Pengine Bwana anawaonyesha ugumu wa mioyo, na ni kana kwamba mashetani wote wanajaribu kwa kila namna kuwakatisha tamaa; kwa saa kadhaa wanapambana nao roho kwa roho ili kumfuata kwa vyovyote Mwalimu mwema mpaka mwisho. Naye anawajalia kuelewa zaidi na zaidi anavyotarajia wapende kudharauliwa na kuangamia, kama chembe ya ngano iliyomwagwa ardhini ioze ikazae kwa wingi.

Ndiyo dalili ya upendo kamili ambao “unatolewa na Roho Mtakatifu akiushirikisha utashi nguvu yake mwenyewe” (Katerina wa Siena). Bwana alimuambia mtakatifu huyo kuwa wanaotamani wokovu wa watu “hawana lengo lingine isipokuwa kuteseka na kukabili uchovu wowote kwa manufaa ya jirani, wakichukua mwilini mwao madonda ya Kristo, kwa kuwa upendo msulubiwa unaowajaa unajitokeza katika kujidharau, kufurahi kudhalilishwa, kupokea mapingamizi na mateso mengine ninayowajalia toka pande zote na kwa namna yoyote… Hivyo wanalingana na Mwanakondoo asiye na doa, Mwanangu pekee ambaye msalabani alikuwa na heri na uchungu kwa wakati mmoja… Nani anaweza kuninyang’anya na kusogeza mbali nami watu hao, waliozama katika moto wa upendo, kwa kutokuwa na matakwa yoyote ya kwao tena na kwa kuwaka kabisa kwa ajili yangu?”

Ndio ulinganifu kamili na Yesu Kristo unaozaa na kuangaza katika maisha ya malipizi. Hata kwa wasiopokea upadri ni kushiriki hali ya kafara ya Yesu na kuungana kwa dhati na kuhani wa milele: “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo” (1Pet 2:4-5).

Maandishi ya Yohane wa Msalaba yanaweza yakaleta picha ya kwamba usiku wa roho ni hasa utakaso wa binafsi kwa ajili ya muungano kamili na Mungu. Utakaso huo wa Kimungu unaoendana na kuzama katika mafumbo ni wa lazima ili kuondoa kasoro za walioendelea. Mwishoni giza na fadhaa vinaacha nafasi kwa mwanga wa juu na furaha ya muungano unaotugeuza na kuandaa moja kwa moja uzima wa mbinguni. Inaonekana baadaye hakuna tena haja ya kuingia handaki la namna hiyo. Kumbe maisha ya watumishi kadhaa wa Mungu yanaonyesha uwezekano wa mwendelezo fulani wa usiku wa roho hata baada ya kuingia muungano unaotugeuza. Ikitokea hivyo ni kwamba jaribio hilo halilengi hasa utakaso bali malipizi.

Yohane wa Msalaba, ingawa hakusisitiza hilo, alidokeza mara kadhaa majaribu ya ndani yaliyowapata watakatifu kwa ajili ya wakosefu. Teresa wa Yesu pia alisema juu ya ukarimu mkubwa wa walioingia makao ya saba, “Mfalme mkuu hawezi kutujalia kitu bora kuliko maisha yanayolingana na yale ya Mwanae mpenzi. Nina hakika imara kwamba neema hizo lengo lake ni kuimarisha udhaifu wetu na kutuwezesha kuvumilia mateso makubwa kwa mfano wa huyo Mwana wa Mungu. Ama hatuoni kwamba wale wote waliomkaribia zaidi Bwana wetu Yesu Kristo ni wale waliopatwa na tabu nyingi zaidi? Tuzingatie zile za Mama yake mtukufu na za mitume watakatifu”.

Tusisahau kwamba mateso makubwa ya rohoni yaliyowapata Bwana na Mama yake hayakuwa kwa utakaso wao, bali kwa ukombozi wetu, na kwamba, kadiri watu wanavyoendelea mateso yao ya ndani yanafanana na yale ya Yesu na Maria. Watumishi wa Mungu wanajaribiwa kwa namna ya pekee, ama kwa sababu wanahitaji utakaso wa dhati zaidi, ama kwa sababu wanatakiwa kufuata njia zilezile za Bwana katika kushughulikia lengo kubwa la Kiroho.

Tukisoma kijuujuu kuhusu mwisho wa maisha ya Alfonso Maria wa Liguori, tutadhani alikuwa akipitia usiku wa hisi, ambao mara nyingi unaendana na vishawishi vikali dhidi ya usafi wa moyo na ya subira. Kwa mzee huyo aliyekwishatimiza miaka 80 vilikuwa vikali hivi hata mtumishi wake akajiuliza kama atarukwa na akili. Lakini tukizingatia kazi yote iliyokwishatendwa na neema rohoni mwa mtakatifu mkubwa kama huyo, tutatambua majaribu hayo yalimpata hasa kwa ajili ya wengine, na ya shirika alilolianzisha kwa mateso mengi.

Mfano wa kushtua zaidi ni ule wa Paulo wa Msalaba, mwanzilishi wa Wapasionisti, aliyeishi miaka 81. Ilitokea nini katika maisha hayo marefu yaliyowekwa wakfu kwa Mungu tangu utotoni katika ugumu wa hali ya juu? Kwenye umri wa miaka 19 alipiga hatua kubwa, hata akaita kipindi hicho kuwa cha “uongofu wake”; kilikuwa na dalili za utakaso wa Kimungu wa hisi. Tangu hapo maisha yake ya kuzama katika mafumbo yalipitia vipindi vitatu. Cha kwanza kilichukua miaka 12, ambapo aliinuliwa ngazi kwa ngazi hadi muungano unaotugeuza. Cha pili kilichukua miaka 45, ambapo aling’amua kwa dhati ya pekee maisha ya malipizi. Cha tatu kilichukua miaka 5, ambapo nderemo ziliongezeka kadiri alivyokaribia mwisho wa maisha yake, ingawa majaribu nayo yaliendelea.

Ngazi za muungano

[hariri | hariri chanzo]

Kwanza kunamuungano mkavu na mchungu, yaani usiku wa roho, halafu muungano wa kutoka nje ya nafsi, yaani uchumba wa Kiroho, na hatimaye muungano unaotugeuza, yaani arusi ya Kiroho.

Muungano mkavu na mchungu

[hariri | hariri chanzo]

Hapo Mungu anafanya mtu atamani mema makuu aliyomuandalia akimpitisha katika tabu za kutisha: “Akili huwa imepatwa na giza isiweze kuushika ukweli; inasadiki yale yote ambayo ubunifu unaichorea na shetani anaiambia. Bila shaka Bwana wetu anamruhusu huyo amshawishi mtu, na pengine hata kumdanganya kwamba, eti! Amelaaniwa na Mungu… Katika dhoruba hiyo mtu hawezi kupokea faraja yoyote… Hakuna dawa nyingine isipokuwa kuitumainia huruma ya Mungu. Naye isipotarajiwa kwa neno moja analomuelekezea au kwa tukio moja linalomtokea anamkomboa kutoka mabaya yake yote. Ungedhani mawingu hayajawahi kuwepo … na mtu anamtukuza Bwana, kwa kuwa ndiye aliyempigania na kumpa ushindi. Mtu anaona wazi kabisa kwamba hajaanza kupambana mwenyewe… Hapo anatambua unyonge wake na uwezo mdogo tulionao Bwana akitunyima msaada wake. Hahitaji tena kutafakari aelewe kweli hizo” (Mt. Teresa wa Yesu). Kwa kuwa sasa anaelewa vizuri maneno ya Mwalimu: “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yoh 15:5) kuhusu wokovu, na anazidi kuelekea kukubali ya kuwa neema inatenda yenyewe na kusababisha juhudi zetu, badala ya kudhani kuwa inawezeshwa na juhudi hizo ifanye kazi.

“Kwa kuwa tabu hizo zinatoka juu, viumbe haviwezi kufanya kitu. Mungu wetu anataka tukiri ukuu wake na unyonge wetu… Njia bora ya kufikia kuvumilia mafadhaiko hayo ni kuwajibika katika kazi za upendo na kutegemea yote kutoka huruma ya Mungu. Yeye hawaachi kamwe wanaomtumainia… Mateso ya nje yanayosababishwa na mashetani ni ya nadra zaidi… tena tabu zote wanazoweza wakasababisha ni ndogo sana ukizilinganisha na hizo nilizokwishazieleza” (Teresa wa Yesu).

Baada ya tabu za ndani ambamo mna uwemo mchungu wa Mungu, mtu anapata ujuzi wa ukuu wa Mungu ambao mara nyingi unasababisha atoke nje ya nafsi yake walau kiasi.

Muungano wa kutoka nje ya nafsi unavyoonekana na ulivyo

[hariri | hariri chanzo]

Kutoka nje ya nafsi ndiko kusimama kwa hisi za nje; hakudai daima mwili uinuke juu kutoka ardhini. Kunajitokeza kwa mtu kutohisi tena walau kiasi, kwa upumuaji kulegeza mwendo na kwa joto la mwili kupungua. “Mtu anatambua kwamba joto la uhai linapungua na mwili unazidi kuwa baridi, lakini kwa utamu na raha isiyosemekana… Mwili unaganda, macho yanaelekea moja kwa moja jambo lisiloonekana: pengine kope zinashuka… Hali hiyo, badala ya kudhoofisha mwili, inauongezea nguvu mpya; inaweza ikatokea kwamba mtu ambaye kwa kawaida anashindwa kuwa amepiga magoti muda mrefu, wakati wa kutoka nje ya nafsi anabaki vile pasipo shida” (Teresa wa Yesu). Pengine kusimama kwa hisi si kamili na kunamruhusu mtu aseme anapata mafunuo gani ili yaandikwe. Muungano wa kutoka nje ya nafsi kwa wenyewe hausimamishi kazi zote za mwili, kama vile kupumua.

Kupotewa na utumiaji wa hisi za nje katika hali hiyo kunatokana na roho kuvutwa na Mungu kwa neema ya pekee ya mwanga na upendo. Mwanga mwingi unaotolewa hapo kuhusu mafumbo ya imani unasababisha mshangao na upendo mkubwa kwa Mungu. Utashi unatekwa na utendaji wa Mungu, ni kama unajeruhiwa nao, na unamuelekea kwa nguvu zote, kama vile dira inavyoelekea kaskazini. Mshangao wa akili unakua kwa upendo, na upendo unakua kwa mshangao: “kutazama uzuri kunatufanya tuupende, na upendo unatufanya tuutazame” (Fransisko wa Sales). Mtu akiwa ametekwa hivyo na mshangao na upendo kwa Mungu, anapotewa na utumiaji wa hisi zake kwa sababu utendaji wake wote unakwenda upande wake wa juu: “Roho ikifuata kabisa utendaji wa kipawa chake kimojawapo, mtu anaacha kutenda kwa kipawa kingine” (Thoma wa Akwino). Ikiwa mwanasayansi anaweza akazama katika utafiti wake kiasi asisikie tena anachoambiwa, zaidi inaweza ikamtokea mwanasala neema kubwa inapomfanya ahisi ukuu usio na mipaka wa Mungu na avutwe kuutazama kwa raha. Hali hiyo inaweza kuwa matokeo ya kawaida ya kuzama ndani ya Mungu. Tutakavyoona, kesi ya roho kutekwa ghafla na kwa nguvu ili kuinuliwa izame katika mafumbo kwa namna ya juu ni tofauti kwa sababu hapo utekaji unatangulia tendo la kuzama badala ya kulifuata.

Je, upendo unaotoka nje ya nafsi una hiari na stahili bado? Bila shaka! Hiari ya tendo la upendo, ambayo ni sharti la kustahili, inatoweka mbinguni tu, roho inapomuona Mungu uso kwa uso, inavutwa naye isiweze kumuacha, na inampenda kwa upendo wa kujiotea usio wa hiari tena: ni upendo mkuu kuliko hiari.

Muda wa kutoka nje ya nafsi unaweza ukawa tofautitofauti; kama ni kamili kwa kawaida kunadumu nukta chache, sanasana nusu saa: lakini zipo kesi za hisi kusimama hata siku nne na zaidi. Kwa kawaida hali hiyo inakwisha kwa mtu kuzinduka mwenyewe na kuanza kutumia tena hisi zake polepole tu, kana kwamba angetokea ulimwengu mwingine. Kuzinduka kunaweza kukasababishwa na agizo la kiongozi, liwe limetolewa kwa sauti au kwa wazo tu. Utiifu huo wakati wa kutoka nje ya nafsi ni moja kati ya dalili zinazothibitisha asili yake ya Kimungu, kutokana na uadilifu unaofanya utashi wa binadamu umtii Mungu hata kwa kuacha hali hiyo.

Mara nyingi hali hiyo ikiwa bandia ni rahisi kuipambanua na ile halisi. Mtu akitoka nje ya nafsi kwa neema hachangamki kwa namna za ajabuajabu na za kimwili tu wanavyofanya wenye ugonjwa wa nafsi, halafu wakapoa na kuishiwa nguvu. Bali roho na mwili wake wote vinaelekea jambo la Kimungu kwa utulivu mkubwa; roho inavutwa na nguvu ya fumbo itoke nje ya hisi zake, kwa kawaida kutokana na njozi iliyoipata. Mwisho wake ni kurudia hali ya kawaida kwa utulivu, likibaki tu sikitiko la kutoweka kwa njozi na furaha ya kimbingu iliyosababishwa nayo. Mtu dhaifu anaweza akazimia kutokana na ubunifu wake kuchangamka au sala kumgusa mno: hapo ni lazima tuzuie iwezekanavyo kuzimia huko kwa kuimarisha mwili kwa lishe bora zaidi. Hatimaye hali ya namna hiyo inaweza ikasababishwa na shetani: dalili zake ni kwamba mtu anaishi katika dhambi, anajisokotasokota, anasema maneno yasiyo na maana anayayosahau baadaye, anatafuta kuonekana hivyo penye watu wengi, na hasa anapokea ujumbe unaoelekeza kutenda maovu au kutenda mema kwa lengo baya.

Tofauti kati ya kutekwa na kutoka nje ya nafsi

[hariri | hariri chanzo]

Kutoka nje ya nafsi ni aina ya kuishiwa nguvu inayotokea kwa utamu kutokana na jeraha la upendo. “Mtu anasikia amepata jeraha la kupendeza… ambalo asingependa lipone kamwe. Anamlalamikia Bwana arusi wake hata kwa nje kwa maneno ya upendo. Hawezi kujizuia kwa sababu yeye anamfanya asikie uwemo wake asijidhihirishe kwa namna anayoweza kumfurahia” (Teresa wa Yesu). Hiyo ni kama ziara fupi kabla ya muungano wa kudumu zaidi unaoitwa muungano unaotugeuza.

Kutoka nje ya nafsi kwa kuishiwa nguvu ni tofauti na kutekwa na Mungu kwa ghafla na kwa nguvu. Tukio hilo “linaiongezea kitu hali ya kutoka nje ya nafsi… kutekwa kunaiongezea aina ya kutumiwa mabavu” (Thoma wa Akwino). Mara nyingi kutekwa hivyo ndiyo kilele cha uchumba wa Kiroho; hapo mtu ni kama amelewa asiweze kushughulikia kingine isipokuwa Mungu. Kutekwa kunafuatwa na mruko wa roho, ambapo mtu anajiona amehamishiwa mahali pengine, pa Kimungu tu.

Matokeo ya muungano wa kutoka nje ya nafsi

[hariri | hariri chanzo]

Huko kuvutwa ndani ya Mungu kunasababisha utengano mkubwa na viumbe, ambavyo ubatili wake unazidi kuonekana wazi; halafu kunasababisha uchungu mkubwa kwa dhambi zilizotendwa na kwa yale yote yanayosogeza mbali na Mungu. Mtu anazidi kuona thamani ya mateso ya Mwokozi na ya uchungu wa Maria chini ya msalaba, na katika kuzama ndani ya mafumbo hayo anachota subira ya ajabu ili avumilie majaribu ambayo Bwana anataka kumtumia tena ili achangie wokovu wa watu.

Kwa kifupi, matokeo ya muungano wa kutoka nje ya nafsi ni utakatifu mkubwa maishani. “Tukimuona mtu ambaye anatekwa katika sala… lakini hatoki nje ya nafsi yake katika maisha, yaani hana maisha bora yanayoambatana na Mungu, kwa kujinyima malimwengu na kufisha matakwa na maelekeo ya kibinadamu, kwa upole, usahili na unyenyekevu wa ndani, na hasa kwa upendo wa kudumu, unisadiki, Teotimo, kwamba kutekwa kwake ni kwa shaka na kwa hatari sana” (Fransisko wa Sales).

Utakaso wa upendo

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya muungano wa kutoka nje ya nafsi, kuna utakaso mchungu wa upendo kama maandalizi ya muungano unaotugeuza. “Mtu anajisikia kama kuchomwa kwa mshale wa moto… ndani mwake kabisa… Uchungu wa ndani ni mkali hivi kwamba hajali tena mwili… Anahisi upweke wa ajabu; hakuna kiumbe duniani kinachoweza kumfariji… yote yanamtesa. Ni kama mtu aliyeelea hewani; ardhi haimtegemezi hata kidogo, wala hawezi kujiinua juu mbinguni. Anateswa na kiu asiweze kuifikia chemchemi… Ni haki kabisa kwamba kitu cha thamani sana kilipwe sana. Mtu anaelewa thamani isiyopimika ya utakaso huo mchungu wa upendo na kujitambua hastahili kamwe kuupata… Katika kiwango hicho cha ukali, jaribu hilo linachukua muda mfupi: sanasana saa tatu au nne; la sivyo udhaifu wetu wa kibinadamu usingeweza kulistahimili… Kifodini hicho ni kichungu, lakini kinamuachia matokeo ya ajabu. Hasa kinamuondolea hofu ya tabu ambazo zinaweza zikampata, kwa kuwa anaziona si kitu akizilinganisha na mateso makali yaliyompata… Mwenyewe amejitenga na viumbe zaidi sana kwa kuelewa kwamba Muumba tu anaweza kumfariji na kumshibisha” (Teresa wa Yesu).

Muungano unaotugeuza, utangulizi wa ule wa mbinguni

[hariri | hariri chanzo]

Sasa tunataka kusema juu ya ustawi wa uzima wa neema unaowezekana duniani katika mtu aliyevuka utakaso wa Kimungu wa roho. Akitoka hizo tabu za ndani ana ujuzi wa ukuu wa Mungu unaomfanya pengine azame ndani yake, pengine ashangilie sifa za Mungu asiweze kujizuia. “Shangwe hizo zinamzamisha katika kujisahau pamoja na viumbe vyote hata asiweze kuwaza wala kusema isipokuwa kwa kumpatia Mungu sifa zile ambazo ni kama tunda la furaha yake” (Teresa wa Yesu). Hiyo furaha takatifu, inayotegemea muungano na Mungu, inaweza kutamaniwa, wakati haifai hata kidogo kutamani njozi na mafunuo ambavyo ni fadhili za pekee zisizohusiana na ustawi wa uzima wa neema ndani mwetu. “Kwa kupokea fadhili nyingi za namna hiyo mtu hastahili ongezeko la utukufu… Kuna idadi kubwa ya watakatifu wasiojua maana ya kupokea neema hizo, kumbe wapo wengine wasio watakatifu wanaozipokea… Mara nyingi kwa fadhili moja tu ya namna hiyo Bwana anapeleka wingi wa tabu” (Teresa wa Yesu).

Neema zinazoweza zikaendana na muungano unaotugeuza

[hariri | hariri chanzo]

Pengine arusi ya Kiroho inaadhimishwa kwa ishara za maana, kama vile mtu kupewa pete iliyopambwa kwa vito, ambayo baadaye anaweza akaiona mara kadhaa, au mtu kusikia nyimbo za mbinguni. Pengine ishara hizo zinazofikiwa na hisi zinaendana na njozi ya Bwana na kuuona Utatu Mtakatifu kwa akili.

Mwono huo kwa njia ya wazo la kumiminiwa na ya mwanga mkuu, unawadhihirishia tofauti za Nafsi tatu na umoja wa hali yao kuliko anavyoweza kufanya mwanateolojia bora kwa maelezo yake. Hawana mwono wa moja kwa moja wa umungu, fumbo hilo halijawa wazi kwao, hawajaona kwamba asingekuwa Nafsi tatu asingekuwa Mungu. Wanabaki katika ngazi ya imani, lakini imani yao imekuwa inapenya mafumbo, inaangaza na kunoga kwa namna ya pekee. Wanaelewa kuliko zamani kwamba Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu na Roho Mtakatifu ni Mungu, na kwamba hata hivyo Baba si Mwana wala hao si Roho Mtakatifu. Kwa namna fulani wanaanza kuona kwamba Baba katika uzazi wake usio na mipaka anamshirikisha Mwana umungu wote, na kwamba hao wanamshirikisha Roho Mtakatifu kwa uenezi kamili wa wema wa Kimungu na kwa umoja wa dhati. Katika hilo wanaona kielelezo cha ajabu cha ushirika wa ekaristi na cha muungano wa dhati wa roho na Muumba na Baba yake. Huo mwono wa kiakili wa Utatu Mtakatifu si bora kama ule wa mbinguni, uangavu wake una kiasi tofauti, unapatikana kwa kwikwi, na si lazima uendane na muungano unaotugeuza ambao hapa duniani ndio mwisho wa kupanda kwa Mungu.

Muungano unaotugeuza wenyewe

[hariri | hariri chanzo]

Kwa kawaida katika hatua hiyo hali ya kutoka nje ya nafsi haipatikani tena. “Roho inapotewa na udhaifu huo mkubwa ambao ulikuwa unampa tabu sana asiweze kabisa kuachana nao. Labda hiyo inatokana na kwamba Bwana wetu ameiimarisha, ameipanua na kuiwezesha kufanyiwa kazi” (Teresa wa Yesu). Hivyo muungano na Mungu unakuwa karibu wa kudumu, kwa kuwa unaweza kufanyika bila kuzuia matumizi ya vipawa. Hapo vipawa vya juu vinavutwa na kiini cha roho unamokaa Utatu Mtakatifu. Kwa neema hiyo mtu hawezi kutia shakani uwemo wa Nafsi za Kimungu ndani mwake wala karibu hapotewi kamwe na uhusiano nazo. “Katika matendo fulanifulani ya siri mtu anatambua kwamba Mungu ndiye anayeihuisha roho” (Teresa wa Yesu).

Yohane wa Msalaba alitoa mifano mbalimbali, “Jiwe linavutwa daima na kiini cha dunia… likifikia humo, tunaweza kusema limefikia kiini cha dhati zaidi. Basi, kiini cha roho ni Mungu; roho ikimfikia kadiri ya mfumo wake na ya nguvu zote za utendaji wake na za elekeo lake, itakuwa imeona kiini chake cha dhati ndani ya Mungu… itamjua, itampenda na kumfurahia kikamilifu. Kabla haijafikia kiwango hicho… inalenga daima muungano kamili zaidi… Ikifikia kiwango cha mwisho, upendo wa Mungu utakuwa umeitia jeraha katika kiini chake cha dhati zaidi, na kwa roho hilo litakuwa mageuzo na maangazo ya nafsi yake yote, ya uwezo na nguvu yake yote, kadiri inavyoweza kupokea, hivi kwamba inaonekana imekuwa Mungu. Hapo ni kama kioo safi na kiangavu kilichofikiwa na nuru… Ikiwa nuru hiyo ni tele zaidi, kioo kinaonekana kuchanganyikana nayo… Ni kama pale ambapo moto, baada ya kushambulia ukuni na kuukausha kwa mwali wake, hatimaye unaupenya na kuugeuza ndani mwake”. Bado ni ukuni, lakini ukuni wa moto, uliopata sifa za moto. Vivyo hivyo moyo uliotakata unatoka karibu mfululizo mwali unaomuelekea Mungu.

Teresa wa Yesu alitumia mfano mwingine, “Ni kama maji ambayo yanamwagika kutoka mbinguni ndani ya mto na kuchanganyikana nao visiweze kupambanuliwa tena”. Ulitolewa pia mfano wa mishumaa miwili ambayo miali yake inaunganika kuwa mmoja. Kuna aina ya muungano kati ya uhai wa roho na uhai wa Mungu. Undani wa hali hiyo ya juu si muujiza hata kidogo, bali ni “hali kamili ya maisha ya Kiroho” (Yohane wa Msalaba): ndio ustawi kamili wa neema ya maadili na vipaji.

Basi, muungano unaotugeuza ni wa dhati na kuleta amani kubwa, ambayo karibu isiweze kuvurugika, walau kwenye kilele cha vipawa vya juu. Hata hivyo inaweza ikatokea kwamba roho “ina huzuni nyingi kiasi cha kufa” (Mk 14:34), Yesu akitaka kuishirikisha tena maisha yake ya malipizi na kuileta kwenye Getsemane kwa wokovu wa wakosefu. Katika bustani hilo mwenyewe, ambaye hakuhusiana na Mungu kwa muungano unaotugeuza tu bali kwa umoja wa nafsi, hata hivyo alitaka kuonja huzuni hiyo ili sadaka yake ya kuteketezwa iwe kamili.

Ufafanuzi wa teolojia kuhusu hali hiyo

[hariri | hariri chanzo]

Yohane wa Msalaba aliandika kuhusu vyumba vya ndani kwamba, “Tunaweza kusema vyumba hivyo ni saba, na vinakaliwa vyote mtu akiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu kikamilifu, kadiri anavyoweza kuvipokea hapa duniani… Wengi wanafikia na kuingia chumba cha kwanza, kila mmoja kadiri ya ukamilifu wa upendo alionao, lakini wachache sana wanaingia kuanzia maisha haya katika chumba cha mwisho, cha ndani zaidi; kwa sababu humo umeshafanyika muungano kamili na Mungu ambao ni desturi kuuita arusi ya Kiroho”. Kwa maneno mengine, mtu anapokuwa na ukamilifu wa kipaji cha hekima, ambacho ndicho cha juu kati ya vyote saba alivyovipokea pamoja na neema ya utakaso, amefikia hekalu la ndani mwake unamokaa Utatu Mtakatifu. Hapo muungano na Mungu unafanyika kweli na kwa namna fulani unamgeuza; ingawa kati ya kiumbe na Muumba kuna umbali usiopimika, muungano huo unafanyika kwa ujuzi unaofanana na mang’amuzi na kwa upendo wa dhati. Roho inakuwa ya Kimungu kwa kushirikishwa kikamilifu umungu: “Yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye” (1Kor 6:17).

Hapo muungano unatugeuza kwa sababu roho, bila kupotewa na umbile lake, inazidishiwa kwa kiasi kikubwa neema inayotia utakatifu na upendo, tena kwa sababu upendo motomoto unatugeuza katika yule ambaye tunampenda kama mimi mwingine, na kumtakia mema yote ya kumfaa kama tunavyojitakia. Ikiwa huyo ni Mungu, watakatifu wanamtakia awatawale kwa dhati zaidi, awe ndani mwao kuliko walivyo wenyewe, kuliko hewa ilivyo ndani ya mapafu au kuliko damu mpya ilivyo ndani ya moyo. “Kadiri roho ilivyo safi na tupu katika imani yake hai na kamili, ina wingi wa upendo wa kumiminiwa na Mungu; na kadiri ilivyo na upendo, Roho Mtakatifu anaiangaza na kuishirikisha vipaji vyake, hivi kwamba upendo ndio sababu na njia ya ushirikishaji huo” (Yohane wa Msalaba).

Furaha ya muungano wa uchumba haidumu zaidi ya nusu saa hivi, ambapo mtu anamng’amua Mungu aliyemo ndani mwake na kumkumbatia, kumbe katika arusi ya Kiroho, ambayo inafungwa hapa duniani na kutimia mbinguni, muungano wa upendo na Mungu, anayejulikana kama kwa mang’amuzi katika kiini cha roho, unakuwa wa kudumu zaidi. “Kati ya watu waliopo katika uchumba wa Kiroho, mmoja anapokea kuliko mwingine: mmoja kwa namna moja, mwingine kwa namna nyingine” (Yohane wa Msalaba). Vilevile katika muungano unaotugeuza kuna viwango mbalimbali hadi kile cha juu zaidi alichokifurahia bikira Maria. Katika viwango hivyo wamefikia kiini chao cha dhati kadiri ya uteule wao. Ndio utimilifu wa ombi la Yesu: “Wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi” (Yoh 17:22-23).

Matokeo ya muungano unaotugeuza

[hariri | hariri chanzo]

Matokeo ya hali hiyo ni yale ya maadili ya Kimungu na ya vipaji vilivyostawi kikamilifu. “Nionavyo mimi, roho haiwezi kamwe kujaliwa hali hiyo pasipo kuthibitishwa moja kwa moja katika neema inayotia utakatifu” (Yohane wa Msalaba) kwa maana neema hiyo ni kushiriki utakatifu usioweza kupotewa wa wenye heri wa mbinguni kwa njia ya ustawi mkubwa wa upendo unaozidi kutusogeza mbali na dhambi. Ustawi huo unakamilishwa na ulinzi wa pekee wa Mungu, ambaye anazuia nafasi za dhambi na kuimarisha kadiri inavyohitajika hivi kwamba tangu hapo mtu anakingiwa daima dhambi ya mauti na kwa kawaida hata dhambi nyepesi ya makusudi. Mt. Teresa alisema tu kuwa mtu karibu anaondolewa usumbufu wowote unaotokana na maono, na kwamba hatendi dhambi nyepesi ya makusudi wakati wote ambapo neema ya muungano unaotugeuza inaendelea kufanya kazi, “Mtu aliyeingizwa katika makao hayo hatawaliwi tena na mabadiliko ya hisi na ubunifu; walau hayo hayawezi kumdhuru wala kumuondolea amani. Inaweza ikaonekana kwamba nataka kusema aliyefadhiliwa hivyo ana hakika kuhusu wokovu wake na hawezi kuanguka tena. Lakini wazo langu ni tofauti. Kila ninaposema kuwa yuko salama, ni lazima kuelewa hivi, kwamba yuko salama mpaka Mungu Mkuu atakapomshika mikononi mwake na mpaka mwenyewe hatamkosea”. Mbele ya misimamo hiyo tofauti kidogo, labda tuseme tu kuwa hapo Roho Mtakatifu anamthibitishia mtu hakika ya tumaini ya kulenga wokovu akikuza ndani yake upendo wa kitoto.

Pengine katika hali hiyo kuna miguso ya Kimungu ya dhati hivi kwamba inatiwa katika undani wa roho. Mguso wa Kimungu ni tendo lipitalo maumbile linalofanyika katika utashi na akili, mle vinamotokana na undani wa roho. Mungu yumo ndani mwetu kuliko tulivyo sisi wenyewe, kwa kuwa ndiye anayetudumisha kwa tendo la kuendeleza uumbaji. Vilevile ndiye anayedumisha neema inayotia utakatifu katika undani wenyewe wa roho, na pengine anajivutia undani wa utashi na akili kwa uvuvio maalumu unaoanzia ndani ya vipawa hivyo.

Ni kana kwamba Mungu anakumbatia roho, pengine kwa nguvu kubwa kweli. Pengine katika undani wa vipawa hivyo vya juu mna jeraha la upendo, jeraha tamu rohoni ambalo linaweza likaendana na jeraha chungu mwilini, hasa upande wa moyo. “Kwa kawaida Mungu haujalii mwili fadhili yoyote kabla hajaijalia roho hasa, na hapo, kadiri ya ukubwa wa furaha na nguvu ya upendo unaosababishwa na jeraha la roho, ni mkubwa vilevile uchungu unaosababishwa na jeraha la mwili. Yote mawili yanakua pamoja kwa sababu watu hao, wakiwa wametakata na kuimarika ndani ya Mungu, kile kinacholeta uchungu upande wa mwili unaoelekea kufa, ni utamu na raha kwa roho iliyopata nguvu na afya” (Yohane wa Msalaba). Ni Mungu anayejeruhi roho akiivuta kwa nguvu kwake na kuitia hamu kubwa ya kumuona moja kwa moja isitengane naye kamwe. Ndio msimamo unaowezesha kupata mara heri hiyo: kwa namna yake hamu hiyo imo pia katika roho za toharani mwishoni mwa utakaso wao.

Mungu hawezi akajionyesha moja kwa moja kwa watu wasio na hamu kubwa ya kuwa naye milele. Mwenyewe anawaandaa kwa hilo kwa mguso wa Kimungu wenye ladha ya uzima wa milele. Miguso ya namna hiyo haipatikani pasipo kubandukana kikamilifu na malimwengu yote, lakini mmojawapo kati ya miguso hiyo unalipa juhudi zote alizofanya mtu. “Lo! Mwali hai wa upendo, / jinsi unavyokijeruhi kwa upole / kiini cha dhati cha roho yangu! / Kwa kuwa si mchungu tena, / timiza kazi yako, ukipenda: / chana sitara ya mkutano huo mtamu” (Yohane wa Msalaba). Yaani, timiza kazi ya muungano wetu, kata uzi wa maisha ya duniani, ambao ndio kizuio cha mwisho cha kukutana na Mpenzi. Sitara hiyo inaruhusu kumchungulia Mungu, lakini inazuia muungano wa moja kwa moja. Mwali hai ndiye Roho Mtakatifu anayesababisha ndani ya mtu matendo ya upendo yanayostahili kuliko yale yote aliyoweza kuyafanya kabla yake. “Jambo la ajabu! Huo moto wa Kimungu, ambao unaweza kuangamiza ulimwengu mara elfu kwa urahisi mkubwa kuliko moto wa kawaida unavyoweza kuteketeza uzi wa kitani, hata hivyo hauangamizi wala hauteketezi. Hivyo siku ya Pentekoste huo moto wa Kiroho ulipowashukia mitume, wakawa wanawaka kwa ndani upendo mtamu wa kupanua na kufurahisha roho” (Yohane wa Msalaba).

“Ni vema kueleza hapa sababu gani ni wachache hivi wanaofikia hiyo hali ya juu ya ukamilifu na ya muungano na Mungu. Kwa hakika si kwa sababu Mungu anataka kuijalia idadi ndogo tu ya watu bora: kinyume chake hamu yake ni kwamba huo ukamilifu mkuu uwe wa wote. Ila anachotafuta mara nyingi bure ni vyombo vinavyoweza kupokea ukamilifu huo. Mungu anamtumia mtu majaribu mepesi, lakini huyo anadhihirika kuwa dhaifu na kukimbia mateso kadiri anavyoweza, hataki kupokea uchungu wowote, wala kujifisha walau kidogo, tena anakosa kabisa ile subira imara anayotakiwa kuwa nayo. Hapo Mungu haendelei kuwatakasa akiwainua kutoka mavumbini kwa njia ya kuwashusha… Watu wanatamani kuwa wakamilifu lakini hawakubali kupitishwa katika njia ya majaribu inayowaunda wakamilifu”. Ni lazima kupitia tabu nyingi ili kufikia “maisha kamili ya Kiroho ambayo ni kumpata Mungu kwa njia ya muungano wa upendo” (Yohane wa Msalaba). Mambo ya Kiroho yaliyo matamu kweli yanatokana na msalaba na moyo wa sadaka unaofisha ndani mwetu yale yasiyoratibiwa ili upendo kwa Mungu na kwa jirani ushike nafasi ya kwanza.

“Moyo unapowaka hivyo kwa upendo wa Mungu wake, mtu anaona taa za moto zinazoangaza yote kutoka juu; hizo ndizo sifa za Mungu: hekima, wema, huruma, haki, maongozi, umilele, enzi kuu. Ni kama rangi za upinde wa mvua wa Kimungu ambazo zinaunganika ndani ya umungu bila kuangamizana, kama vile rangi saba za upinde wa mvua angani zinavyounganika katika nuru nyeupe inayozisababisha. Taa hizo zote zinaunganika katika nuru moja, katika tanuri moja, ingawa kila sifa inadumu kuwa na mwanga wake na moto wake” (Yohane wa Msalaba).

Kinachoshangaza katika watu wa namna hiyo ni jinsi wasivyojijali na wanavyotamani kuteseka kwa mfano wa Yesu. Wanashiriki nguvu yake na upendo wake mkuu kwa ajili ya jirani. Wanafikia kutekeleza kwa pamoja maadili yanayoonekana kupingana; wanaunganisha sala ya hali ya juu na utendaji bora unaowapasa katika malimwengu. Hivyo wamefananishwa na Kristo moja kwa moja. Maisha ya kitume au maisha ya malipizi yanafurika kutoka ukamilifu wa muungano wao na Mungu.

Kutamani muungano unaotugeuza

[hariri | hariri chanzo]

Je, mtu anayeonekana kuwa amevuka usiku wa roho walau kiasi, anaweza kutamani na kuomba neema ya muungano unaotugeuza? Bila shaka, tujue tusijue, neema hiyo ni kilele cha matamanio yetu hapa duniani; lakini inafaa tuitokeze hamu hiyo kwa namna tofauti, kwa kutamani Mungu azidi kutawala ndani mwetu nasi tufanane na Yesu kikamilifu zaidi. Teresa wa Yesu alialika wafuasi wake kuutamani muungano huo wa dhati, lakini kwa unyenyekevu mkubwa, wasitake kulazimisha: “Mkiona pingamizi lolote toka kwa Mungu, nawashauri msijaribu kwenda mbele. Mngemchukiza kiasi kwamba angewafungia mlango moja kwa moja. Yeye anapenda sana unyenyekevu. Mkijiona hamstahili kuingia hata katika makao ya tatu, mtajaliwa mapema kuingia katika yale ya tano. Mtaweza kuyazoea na kumtumikia humo vizuri hivi kwamba atawaruhusu muingie katika yale aliyojiwekea… Kwa kweli nyinyi hamtaweza kuingia makao yote kwa nguvu zenu, hata mkiziona ni kubwa sana: ni juu ya mwenye jumba kuwaingiza”.

“Enyi mnaoota kutembea kwa utulivu na faraja kwenye njia za Kiroho, laiti mngejua ilivyo lazima mjaribiwe ili kufikia hizo hakika na faraja kwa njia ya mateso… Lo! Kama tungeelewa kwa dhati kwamba haiwezekani kufikia unene yaani vilindi vya hekima na utajiri wa Mungu pasipo kupenya unene wa aina elfu za mateso, kwa furaha na hamu kubwa ya roho! Mtu anayetamani kweli hekima, kwanza anatamani sana kuzama kabisa katika unene wa msalaba unaofikisha kwenye uzima… Wengi wanataka kufikia mwisho bila kupitia njia inayofikisha huko” (Yohane wa Msalaba).

Udhati wa muungano huo

[hariri | hariri chanzo]

Udhati wa muungano unaotugeuza unatokana na neema inayotenda ya hali ya juu. Tofauti na neema inayosaidia tu kutenda, ile inayotenda tokeo lake ni la kumpatia Mungu, kwa sababu hapo hatutendi, bali tunatendewa naye, ingawa kwa kukubali wenyewe, kwa sababu utashi wetu utadumu hata katika heri ya milele. “Hapo utashi wa mtu haupotei, bali unaunganika kwa nguvu na utashi wa Mungu anayempenda hivi kwamba unapenda kwa nguvu na ukamilifu ambavyo anapendwa naye… Nguvu hiyo ndiye Roho Mtakatifu, na hapo roho inageuzwa ndani yake. Mwenyewe anatolewa kwake ili kuipatia hiyo nguvu ya upendo, naye anatolea na kufidia yale iliyopungukiwa nayo” (Yohane wa Msalaba).

Usawa wa upendo

[hariri | hariri chanzo]

Mtu anafikia usawa fulani na Mungu: “Roho inatenda ndani ya Mungu na kwa njia yake yale ambayo Mungu mwenyewe anayatenda ndani ya roho na kwa namna anayoyatenda; utashi wa pande mbili ni kama mmoja tu, na utendaji wa Mungu umeunganika na ule wa roho. Tangu hapo, kwa kuwa Mungu anajitoa kwake kwa uhuru na pasipo kujitafutia faida, pia roho, iliyo na utashi huru na mkarimu kadiri ilivyounganika vema na Mungu, inampatia Mungu mwenyewe, kwa njia ya Mungu, na ndiyo zawadi halisi na kamili ya roho kwa Mungu… Hivyo roho inampatia kwa mikono miwili yale inayoyapokea toka kwake, na katika zawadi hiyo inayompatia Mungu, roho inampatia, kwa utashi wake wote ulio huru, Roho Mtakatifu aliye wake, ili kwa njia yake ajipende anavyostahili. Nayo roho inapata furaha na raha isiyopimika kwa sababu inaona kuwa inampatia Mungu kitu cha kwake kinacholingana na ukuu wa Mungu usio na mipaka” (Yohane wa Msalaba).

Hatima ya “Wimbo wa Kiroho” wa Yohane wa Msalaba ni: “Enyi watu mlioumbwa kwa ajili ya vilele hivyo na mlioitwa kuvipata, mnafanya nini? Mnashughulikia nini? Mnayoyatamani ni ya chini tu, mali yenu ni umaskini mtupu! Lo! Upofu wa kusikitisha! Ingawa kuna mwanga mkubwa hivi, macho yenu hayaoni, nanyi mnabaki viziwi wakati zinaposikika sauti kubwa hivi!”

“Mwaliko huo, ambao mtakatifu wetu aliwaelekezea watu kwa jumla, unatuonyesha kuwa hakudhani makuu hayo aliyotueleza yako nje ya kawaida… Hakika kuchanua kwa mbegu ya uzima upitao maumbile, iliyo neema inayotia utakatifu ndani mwetu, kumeandaliwa kwa wote waliyo nayo” (Gabrieli wa Mt. Magdalena).

  • F. VAN VLIJMEN, W.F., Safari ya Kiroho, Mafundisho kwa Watawa (vitabu 2) – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1978
  • R. GARRIGOU-LAGRANGE, O.P., Hatua Tatu za Maisha ya Kiroho, Utangulizi wa Uzima wa Mbinguni – tafsiri fupi ya Rikardo Maria, U.N.W.A. – ed. Ndugu Wadogo wa AfrikaMorogoro 2006

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
  •  "Ascetical Theology" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  •  "Mystical Theology" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  •  "Christian and Religious Perfection" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  •  "Beatific Vision" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  •  "Asceticism" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  •  "State or Way (Purgative, Illuminative, Unitive)" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  •  "Sanctifying Grace" . Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  • Ascetic theology from 1902 Catholic dictionary
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hatua ya muungano kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy