Misa
Misa ni adhimisho la ekaristi hasa likifuata mapokeo ya Kiroma.
Mbali ya ibada za mwanzo na mwisho, sehemu kuu ni mbili: Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi. Ya kwanza inafanyika hasa mimbarini, ya pili altareni. Ndizo meza mbili ambapo Mungu Baba analisha wanae.
Jina
[hariri | hariri chanzo]Jina linatokana na maneno ya mwisho ya ibada hiyo ambayo shemasi anaruhusu waamini kuondoka kisha kubarikiwa na askofu au padri aliyeongoza misa hiyo: Ite, Misa est (kwa Kilatini: "Nendeni, Misa imekwisha", au "Nendeni, sasa mnatumwa").
Wengi wanahusisha neno hilo na lile la Kilatini missio, kwa maana ya utume: kwamba aliyeshiriki ibada, mwishoni anatumwa kuwashirikisha wengine matunda yake, hasa amani ya Yesu Kristo.
Ushiriki na maisha ya Kiroho
[hariri | hariri chanzo]Utakatifu unapatikana katika kuungana na Mungu kwa dhati zaidi na zaidi kwa njia ya imani, tumaini na upendo. Kutokana na ukweli huo, chombo kikuu kimojawapo kadiri ya Kanisa Katoliki ni kushiriki misa, tendo bora la adili la ibada na la liturujia ya Kikristo. Misa inatakiwa kuwa chemchemi kuu ya neema zinazohitajika maishani, chemchemi ya mwanga na joto upande wa roho, kwa mfano wa pambazuko la jua ambalo, baada ya usiku na usingizi ulio mfano wa kifo, ni kana kwamba linavirudishia uhai vyote vinavyoamka duniani. Mfiadini Yohane Fisher aliwajibu Waprotestanti, “Misa ni kama jua ambalo kila siku linaleta mwanga na joto katika maisha yote ya Kikristo”.
Hatuwezi kuendelea katika maisha ya Kiroho tusipopenya kila siku zaidi kile kinachofanya sadaka ya altare iwe na thamani isiyo na mipaka. Tungeelewa kwa undani thamani hiyo tungeona inavyotengeneza upya na kudumisha na kustawisha uzima wa Mungu ndani mwetu. Kumbe mara nyingi mazoea ya kushiriki sadaka hiyo takatifu kwa imani haba yanafanya tendo hilo liwe la kawaida, tusipate matunda yale yote yanayotarajiwa. Hilo liwe tendo kuu la siku zetu zote, hivi kwamba mengine yote yawe ya kulisindikiza tu, hasa sala nyingine na sadaka ndogondogo tunazopaswa kumtolea Bwana mfululizo.
Moyo wa Kristo kujitoa kwa kudumu
[hariri | hariri chanzo]Ukuu wa misa unatokana na kwamba kwa dhati ni sadaka ileile ya msalabani, kwa sababu kuhani yuleyule ndiye anayeendelea kujitoa kwa njia ya watumishi wake, na kafara ileile ndiyo inayotolewa kwa kuwepo kweli altareni. Tofauti ni namna ya kuitoa tu: huko Kalivari ilitolewa kwa kupokea ukatili, kumbe katika misa inatolewa kisakramenti kwa njia ya mageuzo mawili yanayotenganisha kifumbo Mwili na Damu ya Mwokozi.
Sadaka hiyo ni ishara ya Yesu kujitoa moyoni, na ni ukumbusho wa sadaka aliyoitoa Kalivari kwa kupokea ukatili. Sadaka hiyo ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ingawa inatolewa kisakramenti tu, ina uzito mkubwa kuliko ile ya mwanakondoo wa Pasaka na nyingine zote za Agano la Kale. Kwa kuwa ishara ina thamani kulingana na ukuu wa jambo inaloashiria: bendera inayotukumbusha nchi yetu, hata kama imeshonwa kwa kitambaa cha kawaida, kwetu ina thamani kuliko vitambaa vyovyote vile. Sadaka za Agano la Kale zilikuwa mifano ya mbali ya ile ya msalabani, kumbe ekaristi inatokeza kule kujitoa kwa ndani kunakodumu katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kiini hicho cha misa kina thamani isiyo na mipaka kutokana na Nafsi ya Kimungu ya Neno aliyefanyika mwili, aliye kuhani mkuu na kafara.
“Mnapomuona altareni mtumishi wa Mungu akiinua hostia takatifu kuelekea mbinguni, msidhani ndiye kuhani halisi, bali mkiinua mawazo yenu juu kuliko yanayogusa hisi, mzingatie mkono wa Yesu Kristo unaojinyosha bila kuonekana” (Yohane Krisostomo). Padri tunayemuona hawezi kupenya fumbo hilo mpaka ndani, lakini juu yake vipo akili na utashi wa Yesu. Ikiwa mtumishi si daima anavyotakiwa kuwa, kuhani mkuu ni mtakatifu tu. Ikiwa mtumishi, hata kama ni mwema, anaweza akapitiwa kidogo au akazingatia taratibu za ibada kuliko maana yake, juu yake yupo asiyepitiwa, naye anamtolea Mungu kwa ujuzi kamili ibada ya fidia, dua na shukrani ambayo ina thamani na upana pasipo mipaka.
Huku kujitoa kwa kudumu ni mwendelezo wa Yesu kujitoa sadaka maisha yake yote, kuanzia alipoingia ulimwenguni na hasa msalabani. Alipokuwa duniani sadaka hiyo ilikuwa na stahili; sasa inaendelea pasipo stahili, kama ibada ya fidia na dua ili kutugawia stahili za msalabani. Baada ya ulimwengu kwisha, hakutakuwa tena na misa wala sadaka halisi, ila utimilifu wake: Kristo ataendelea kujitoa kwa Baba si kama fidia na dua, bali kama ibada na shukrani. Wimbo wa “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu” unatufanya tuhisi kidogo ibada ya milele. Tungejaliwa kuona moja kwa moja upendo unaomfanya Kristo ajitoe kwa kudumu tungeshangaa mno! “Sina dhana tu, bali hakika kabisa ya kwamba roho ingeona na kutazama kwa dhati kiasi fulani cha uangavu wa ndani wa sakramenti ya altare, ingewaka moto kabisa, kwa kuona upendo wa Mungu. Naona kwamba wanaotoa sadaka au kuihudhuria wanatakiwa kutafakari kwa dhati ukweli mkuu wa fumbo takatifu mno, ambalo tuzame ndani yake na kutulia tusigeuke” (Anjela wa Foligno).
Matokeo ya sadaka ya Misa na misimamo inayohitajika moyoni
[hariri | hariri chanzo]Yesu Kristo kujitoa kwa dhati, ambako ndiko kiini cha sadaka ya ekaristi, kuna malengo yaleyale na matokeo yaleyale ya sadaka ya msalabani, ila tutofautishe matokeo yanayomhusu Mungu na yale yanayotuhusu sisi. Matokeo ya misa yanayomhusu Mungu moja kwa moja yanapatikana daima kwa hakika na kikamilifu pasipo haja ya mchango wetu, hata akiadhimisha padri asiyestahili, kwa kuwa sadaka hiyo inampendeza Mungu kuliko dhambi zote pamoja zinavyomchukiza. Kumbe matokeo yanayotuhusu wenyewe yanapatikana tu kadiri ya misimamo yetu.
Hivyo misa kama sadaka ya upatanisho inawapatia wakosefu wasiokaidi (hasa wale wanaoihudhuria au wale ambao inatolewa kwa ajili yao) neema inayowafanya watubu na kuamua waungame, kama sadaka ya msalabani ilivyomsababishia mhalifu mwema. Misa kama sadaka ya fidia inawaondolea waliotubu, kadiri misimamo yao ilivyo kamili, walau sehemu ya adhabu za muda zinazowapasa kutokana na dhambi: ndiyo sababu inatolewa kwa kuokoa roho za toharani. Hatimaye misa kama sadaka ya dua inatupatia neema zote tunazohitaji tuwe watakatifu. Ndiyo sala kuu ya Kristo aliye hai daima, sala ambayo haikomi bali inaongozana na ile ya Bibi arusi wake. Matokeo yake yanalingana na ari yetu, hivyo anayejiunga nayo vizuri ana hakika ya kupata neema kwa wingi kwa ajili yake na ya wapendwa wake.
Ndiyo sababu watakatifu, waliojaa vipaji vya Roho Mtakatifu, walikuwa wakijikokota kuihudhuria misa hata wasipojiweza kwa ugonjwa. Wengine walikuwa wakitokwa na machozi ya upendo au kujisahau wakati wa misa. Wengine walimuona Bwana badala ya padri, au damu kikombeni kufurika na kutiririkia mikono yake na hekalu, huku malaika wakiikinga kwa vikombe vya dhahabu ili kuifikisha popote walipo wenye kuhitaji wokovu.
Namna ya kujiunga na sadaka ya ekaristi
[hariri | hariri chanzo]Maneno ya Thoma wa Akwino kuhusu sala ya midomo yanafaa kwa jambo hilo pia: “Unaweza kuelekea ama maneno ili uyatamke vema, ama maana ya maneno, ama lengo la sala, yaani Mungu na jambo tunaloliomba… Uzingatifu huo wa mwisho, ambao hata watu wanyofu wasio na elimu wanaweza kuwa nao, pengine ni mkubwa hivi hata roho ni kana kwamba inainuliwa kwa Mungu na kusahau mengine yote”. Vilevile kuna namna mbalimbali za kushiriki misa kwa imani, tumaini na upendo. Tunaweza kuzingatia sala za liturujia, ambazo ni nzuri ajabu na katika usahili wake zinatokeza mawazo makuu. Tunaweza kuzingatia Pasaka ya Bwana, ambayo misa ni ukumbusho wake hai, tukijiona chini ya msalaba pamoja na Bikira Maria na Mtume Yohane. Tunaweza pia kumtolea Mungu, pamoja na Yesu, malengo manne ya sadaka, yaani ibada, fidia, dua na shukrani. Tunafaidika na misa mradi tusali, hasa tukijisikia kuvutwa na upendo safi wa nguvu, kidogo kama Yohane alipoegemea moyoni pa Yesu.
Kwa vyovyote tusisitize tunavyopaswa kuungana kwa dhati na Mwokozi katika kujitoa kwa Baba yake, hasa kwa tabu na matatizo, tukimtoa na kujitoa kila siku vizuri zaidi, padri anavyosema ameinama wakati wa matoleo, “Ee Bwana, utupokee sisi tunaokunyenyekea na kutubu moyoni”. Katika Kumfuasa Yesu Kristo, Bwana anasema, “Kwa ajili ya dhambi zako nimejitoa kwa Mungu Baba kwa hiari yangu, nikinyosha mikono msalabani na mwili uchi… Vivyo hivyo inafaa na wewe kwa hiari yako ujitoe kwangu kila siku katika misa kama sadaka safi na takatifu, kwa nguvu zako zote… Siombi zawadi yako, nakutaka mwenyewe tu” (IV,8:1-2). Mfuasi anamjibu, “Bwana wangu, kwa unyofu wa moyo najiweka leo mikononi mwako niwe wako siku zote, nikutumikie, niwe daima sadaka ya utukufu wako. Unipokee nikijitoa pamoja na mwili wako mtakatifu” (IV,9:1).
Kutembelea sakramenti kuu kutukumbushe misa na kwamba katika tabenakulo, ingawa hakuna sadaka halisi (kwa sababu inakwisha pamoja na misa), Yesu yumo kweli akiendelea kuabudu, kutuombea na kushukuru. Kila saa tuungane naye katika kazi hiyo. Kwenye tabenakulo tunyamaze ili tumsikilize, tujisahau ili tuzame ndani mwake.
Utekelezaji
[hariri | hariri chanzo]Tunaweza kuyachimba mafundisho ya Kikatoliki juu ya sadaka ya misa ama kinadharia tu ama kimaisha, yaani kwa kujiunga nayo na kumtolea Mungu pamoja na Yesu yale yote yanayoweza yakatupata siku hiyo, hadi kufa, na hata kuingia mbinguni. Inafaa mtu atangulize kutoa sadaka ya uhai wake ili kujaliwa kifo chema, yaani katika neema inayotia utakatifu. Kwa kuwa maendeleo ya Kiroho yanalenga hasa tendo la mwisho la upendo hapa duniani ambalo, likiandaliwa na maisha yote na kufanywa kikamilifu, linatarajiwa kutufungulia mara milango ya mbinguni.
Ili tupenye dhati ya misa tunapaswa kujifunza kwa Mama wa Mungu. Baadhi ya watakatifu, hasa wale waliojaliwa majeraha ya Yesu, waliunganika na mateso na stahili zake kwa namna ya pekee; hata hivyo muungano huo haukulingana na ule wa Maria. Kutokana na ujuzi na mang’amuzi ya dhati, Maria chini ya msalaba alipenya fumbo la ukombozi, kadiri ya imani yake na ya vipaji alivyokuwa navyo kulingana na upendo wake mkubwa.
Walio mahututi wanahimizwa kutoa sadaka ya uhai wao ili mateso ya mwisho yawe na thamani, fidia, stahili na dua. Ili tangu sasa tutoe sadaka hiyo vizuri, tunapaswa kuitoa pamoja na ile ya Mwokozi inayodumu kisakramenti altareni, na pamoja na sadaka ya Maria aliyeishiriki kwa namna bora. Ili tuelewe toleo hilo linadai nini, inafaa tukumbuke malengo manne ya sadaka: kuabudu, kufidia, kudua na kushukuru.
Kuabudu
[hariri | hariri chanzo]Yesu msalabani alifanya kifo chake kiwe sadaka ya kuabudu, utekelezaji bora wa amri ile aliyomjibu mshawishi, “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake” (Lk 4:8). Ibada ni haki ya Mungu kutokana na ukuu wake kama Muumba, kwa kuwa mwenyewe tu yupo milele. Inatakiwa kuwa ya nje na ya ndani kwa pamoja, kuongozwa na upendo, kufanyika katika Roho na ukweli. Yesu bustanini alitoa ibada yenye thamani isiyo na mipaka aliposujudu kifudifudi akisema, “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Math 26:39). Ibada hiyo ilikiri kimatendo na kwa dhati ukuu wa Mungu, Bwana wa uhai na wa kifo, ambaye “hushusha hata kuzimu, na kuinua tena” (Tob 13:2).
Ibada hiyo ilipoendelea msalabani, Maria aliishiriki kadiri ya ujazo wa neema ambao alijaliwa na ambao ukazidi kuongezeka. Mbele ya msalaba aliabudu haki ya Mungu aliyetaka kifo cha Mwanae asiye na kosa kiwe malipizi ya dhambi kwa wokovu wa milele wa watu. Tunaweza kumuabudu kwa namna nyingi, lakini hakuna iliyo bora kuliko kujiunga kila siku na sadaka ya Mwokozi. Tangu sasa ibada yetu hiyo iwe nyofu na ya dhati, kiasi cha kuongoza kweli maisha yetu na kutuandaa kwa ile itakayotupasa kuwa nayo moyoni saa ya mwisho.
Kufidia
[hariri | hariri chanzo]Lengo la pili la sadaka ni kufidia chukizo la dhambi kwa Mungu, na kulipa adhabu inayodaiwa na dhambi. Bwana alilipa kupita kiasi kwa makosa yetu, kwa sababu alipotoa uhai wake kwa ajili yetu alifanya tendo la upendo linalompendeza Mungu kuliko jinsi jumla ya dhambi zote inavyomchukiza. Upendo wake ulikuwa mkubwa mno kuliko uovu wetu watesi wake; ulikuwa na thamani isiyopimika kwa kuwa ulitoka katika Nafsi ya Neno. Lakini, kwa vile sababu asili haifuti sababu shiriki, sadaka ya Mwokozi haifuti sadaka yetu, bali inaichochea na kuitia thamani.
Maria alitupatia kielelezo akiungana na mateso ya Mwana na kutoa fidia kwa ajili yetu hata akaitwa pengine “mkombozi mshiriki”. Alikubali kifodini cha Mwanae mpenzi ambaye alimuabudu kwa haki na kumpenda kwa hisani isiyosemeka. Shujaa kuliko Abrahamu aliyekuwa tayari kumchinja Isaka, Maria alipomtoa Mwanae kwa wokovu wetu alimuona akifa kwa mateso ya kutisha ya mwili na roho. Hakuna malaika aliyeingia kati kuisimamisha sadaka ya Maria na kumuambia, “Sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee” (Mwa 22:12). Maria aliona ilivyotimia sadaka ya Yesu, ambayo sadaka ya Isaka ilikuwa kidokezo chake tu, akateseka kwa ajili ya dhambi kadiri ya upendo wake kwa Mungu anayechukizwa nazo, kwa Mwanae aliyesulubiwa nazo, na kwa roho zetu zinazoangamizwa nazo. Kwa kuwa upendo wa Bikira ulizidi ule wa Abrahamu, maneno aliyoambiwa babu huyo yanamfaa zaidi Mama yetu: “Kwa kuwa umetenda neno hili… katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni” (Mwa 22:16-17).
Sadaka ya Yesu na Maria ilikuwa fidia ya dhambi na malipizi ya adhabu iliyodaiwa nazo. Tangu sasa tuombe saa yetu ya mwisho iwe na stahili na kufidia, tena tujaliwe neema ya kutoa sadaka hiyo kwa upendo mkubwa ambao uzidishe thamani yake. Tufurahi kulipa deni hilo kwa haki ya Mungu ili utaratibu wake urekebishwe kikamilifu ndani mwetu. Tukiungana hivyo kwa ndani na misa zote zinazoadhimishwa kila siku ulimwenguni kote, tukiungana hasa na kiini cha misa hizo, yaani sadaka iliyo hai daima moyoni mwa Kristo, tutajaliwa kuungana nazo hata saa ya mwisho. Muungano huo wa upendo na Yesu ukiwa wa ndani zaidi kila siku, fidia ya toharani itafupika, na pengine tutajaliwa kutakata tayari hapa duniani kwa kukua katika upendo, badala ya kutakaswa pasipo stahili kisha kufa.
Kuomba
[hariri | hariri chanzo]Yesu “siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii” (Eb 5:7-9). Tukumbuke sala yake ya kikuhani aliyoitoa kati ya karamu ya mwisho na sadaka ya msalabani, alipowaombea mitume wake hata sisi pia, “wao wamjiao Mungu kwa yeye”; sasa “yu hai sikuzote ili awaombee” (Eb 7:25), hasa katika sadaka ya misa, ambayo ndiye kuhani wake mkuu. Pamoja naye tunaombewa na bikira Maria akiitikia maombi tuliyomtolea mara nyingi. Kufani mtu anatakiwa kuungana na misa zinazotolewa wakati huohuo akijiombea neema ya kifo chema, kutokana na thamani ya hizo na ya sala ya Kristo inayoendelea kwa njia ya hizo. Tena inafaa awaombee wale wote wanaokaribia kufa neema hiyo bora ya wateule. Ili tujiandae kuomba dua hiyo saa ya kufa, tuwaombee mara nyingi katika misa watakaokufa siku hiyohiyo, pia tuagize pengine misa ili tujaliwe kifo chema pamoja na ndugu na marafiki wanaotutia wasiwasi zaidi kuhusu wokovu wao, na wale ambao tuliwakwaza na kuwapotosha.
Kushukuru
[hariri | hariri chanzo]Hatimaye kila mmoja anatakiwa kujiandaa kila siku kufanya kifo chake katika Bwana kiwe sadaka ya shukrani kwa fadhili zote alizojaliwa. Sadaka halisi itakapokoma, utimilifu wake utadumu ukiwa na ibada za wateule ambao, kwa kuungana na Yesu na Maria, wataimba na malaika wimbo wa Mtakatifu, na kumtukuza Mungu kwa shukrani. Tuitoe sadaka hiyo mara nyingi kwa kuungana na misa zinazotolewa siku hiyo, kama ingekuwa ya mwisho, ili kuitoa vema saa ya kufa kwetu, tukiwaalika Mwokozi na Mama yake waje kutuchukua na kutujalia neema kuu itakayohakikisha moja kwa moja wokovu wetu kwa tendo la mwisho la imani, tumaini na upendo.
Hayo tuliyoyasema kuhusu kutoa sadaka ya uhai wetu kwa kuungana na ile ya misa, yaeleweke kimatendo kama alivyoandika Mtume Paulo, “Ninakufa kila siku” (1Kor 15:31). Ni kupokea mapema, kwa upendo na subira, si mateso ya dakika za mwisho tu, bali yale yote ya mwili na roho ambayo Mungu ametupangia tangu milele ili kututakasa na kutufanya tuchangie wokovu wa watu. Pengine udhaifu wetu unafanya mateso hayo ya aina mbalimbali yaonekane mazito, lakini ni madogo yakilinganishwa na yale aliyoyavumilia Yesu kwa upendo mkuu. Nasi tutayapokea tukijiombea tuanze kuupenda msalaba, yaani kumpenda kweli msulubiwa, kwa kuwa tunapaswa kumrudishia upendo kwa upendo.
Turudie kusoma maneno yake kwa mwanafunzi mwaminifu katika Kumfuasa Yesu Kristo (III,47:1-3), “Mwanangu, kazi nzito uliyokubali kwa ajili yangu isikuvunje. Usipoteze moyo kutokana na mashaka. Maagano yangu yakutie nguvu na kukutuliza daima. Mimi naweza kulipa yote kupita kiasi na bila kipimo. Hutahangaika hapa muda mrefu mno… Siku moja tabu yote na machungu yatakoma… Kazi unayoifanya, uifanye vizuri. Lima shamba langu kwa bidii, mwenyewe nitakuwa tuzo lako. Andika, soma, imba, juta, nyamaza, sali, vumilia kiume pingamizi; inafaa kujipatia uzima wa milele kwa masumbuko hayo, na hata kwa makubwa zaidi. Siku moja amani itakuja… Laiti ungewaona watakatifu mbinguni na mataji yao ya milele, jinsi wanavyofurahi sasa katika utukufu mkuu! Kumbe, ndio waliopata dharau duniani, wakatupwa kama wasiostahili kuishi… Hungetamani siku ya furaha duniani, la; bali ungependa kuvumilia mengi kwa ajili ya Mungu; ungeona ni faida kubwa kutupwa na watu kama takataka”.
Katika misa tuunganishe hivyo sadaka yetu na ya Mwokozi; tumtolee pingamizi na tabu zitakazotupata, tukifikiri zitatuletea faida kubwa, hata vizuio vikawa vyombo. Msalaba ulikuwa ndio kizuio kikuu walichotaka kumwekea Yesu, kumbe akaufanya chombo kikuu cha wokovu. Katika mwili wake wa fumbo, kila kiungo kikiwajibika kwa imani, vingine vyote vinafaidika. Ndiyo sababu hata kitu kidogo kinakuwa kikubwa tukikifanya kwa upendo wa Mungu na wa jirani katika muungano na Yesu, kuhani wa milele.
Tuzingatie sehemu za misa zinavyolingana na upendo unaotakata, unaoangaza na unaojitoa mhanga kwa kuungana na Mungu. Zinaanza kwa kututia toba na majuto (Nakuungamia), ibada na shukrani (Utukufu), dua (Sala) na imani (Masomo, Nasadiki) ili tuwe tayari kumtoa Mwanakondoo wa Mungu, halafu kumpokea na kushukuru. Hivyo zinatukumbusha hatua za kuinuka kwa Mungu: utakaso wa wanaoanza, mwanga wa wanaoendelea, na muungano wa waliokamilika.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]THE GENERAL INSTRUCTION OF THE ROMAN MISSAL (PDF). Canadian Conference of Catholic Bishops Publication Service. ISBN 978-0-88997-655-9. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2012-04-25. Iliwekwa mnamo 19 Novemba 2011. {{cite book}}
: Unknown parameter |dead-url=
ignored (|url-status=
suggested) (help)
- Baldovin,SJ, John F., (2008). Reforming the Liturgy: A Response to the Critics. The Liturgical Press.
- Bugnini, Annibale (Archbishop), (1990). The Reform of the Liturgy 1948-1975. The Liturgical Press.
- Donghi, Antonio, (2009). Words and Gestures in the Liturgy. The Liturgical Press.
- Foley, Edward. From Age to Age: How Christians Have Celebrated the Eucharist, Revised and Expanded Edition. The Liturgical Press.
- Fr. Nikolaus Gihr (1902). The Holy Sacrifice of the Mass: Dogmatically, Liturgically, and Ascetically Explained. St. Louis: Freiburg im Breisgau. OCLC 262469879. Iliwekwa mnamo 2011-04-20.
- Johnson, Lawrence J., (2009). Worship in the Early Church: An Anthology of Historical Sources. The Liturgical Press.
- Marini, Piero (Archbishop), (2007). A Challenging Reform: Realizing the Vision of the Liturgical Renewal. The Liturgical Press.
- Martimort, A.G. (editor). The Church At Prayer. The Liturgical Press.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Mafundisho ya Kanisa Katoliki
- Catechism of the Catholic Church, 1322-1419
- "Liturgy of the Mass". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- Why Fast Before Communion? by Fr. William Saunders Ilihifadhiwa 13 Desemba 2007 kwenye Wayback Machine.
- Catholic Apologetics of America
- Links to documents on the Mass Ilihifadhiwa 24 Februari 2012 kwenye Wayback Machine.
- Celebrate The Liturgy
Ibada ya Kiroma ilivyo leo
- The Order of Mass Ilihifadhiwa 2 Julai 2011 kwenye Wayback Machine.
- Fr. Larry Fama's Instructional Mass Ilihifadhiwa 19 Julai 2011 kwenye Wayback Machine.
- Today's Mass readings (New American Bible version)
- The Readings of the Mass (Jerusalem Bible version)
- Mass Readings Ilihifadhiwa 17 Desemba 2007 kwenye Wayback Machine. (text in official Lectionary for Ireland, Australia, Britain, New Zealand etc.)
- Forum about Liturgy Ilihifadhiwa 27 Machi 2010 kwenye Wayback Machine.
Ibada ya Kiroma ilivyokuwa
- Latin Mass § CatholicLatinMass.org Ilihifadhiwa 25 Februari 2012 kwenye Wayback Machine.
- SanctaMissa.org: Multimedia Tutorial on the Latin Mass
- The Holy Mass: A Pictorial Guide with Text
- Text of the Tridentine Mass in Latin and English
Mafundisho na taratibu vya Ushirika wa Anglikana
- The Anglican Missal online Ilihifadhiwa 24 Februari 2009 kwenye Wayback Machine.
Mafundisho ya Kilutheri
- Article 24 of the Augsburg Confession Ilihifadhiwa 15 Septemba 2008 kwenye Wayback Machine., regarding the Mass
- Article 23 of the Defense of the Augsburg Confession Ilihifadhiwa 24 Julai 2008 kwenye Wayback Machine., regarding the Mass
- The Church of Sweden Service Book Ilihifadhiwa 30 Juni 2007 kwenye Wayback Machine. including the orders for High and Low Mass