Nenda kwa yaliyomo

Sala ya Kanisa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Waimbaji Waorthodoksi kwenye Kanisa la Mt. George, Istanbul, Konstantinopoli, Uturuki.
Wamonaki wa Mt. Benedikto wa Nursia wakiimba kipindi cha Magharibi kwenye Jumamosi Kuu.

Sala ya Kanisa ndiyo sala rasmi ya madhehebu fulani ya Ukristo iliyopangwa ifanyike mara kwa mara kila siku.

Kwa kawaida sala hizo zinapatikana katika kitabu kilichoandaliwa au kupitishwa na mamlaka ya Kanisa (walau dayosisi au shirika la kitawa).

Kwa njia hiyo Kanisa linahakikisha kwamba haliachi kamwe kusali, kama Yesu alivyoagiza, na kufuatana na desturi ya Wayahudi wakati wake, na ya Mitume wa Yesu kadiri ya Matendo ya Mitume.

Ni hasa wamonaki na watawa wengine waliotimiza kwa bidii kubwa wajibu huo.

Inawezekana kwamba Muhammad katika safari zake aliguswa na juhudi hizo akaziagiza kwa Waislamu wote wasali mara tano kwa siku.

Liturujia ya vipindi

[hariri | hariri chanzo]

Katika utaratibu wa Kanisa la Roma, unaofuatwa na majimbo karibu yote ya Kanisa Katoliki la Kilatini, sala hiyo kwa sasa inaitwa "Liturujia ya vipindi".

Vipindi hivyo ni: Kipindi cha masomo, Masifu ya asubuhi, Sala ya mchana (Kabla ya adhuhuri, Adhuhuri na Baada ya adhuhuri), Masifu ya jioni na Sala ya mwisho.

Katika maisha ya Kiroho

[hariri | hariri chanzo]

Sala ya Kanisa ambayo kila siku inaendana na misa takatifu ni kati ya njia kuu za kuungana na Mungu. Misa ndiyo sala kuu ya Kristo inayoendelea hadi mwisho wa dunia, ambapo kwa huduma ya mapadri wake tendo la Mungu-mtu kupenda na kujitoa linapaa mfululizo toka moyo wake wa kikuhani kama ibada, fidia, dua na shukrani za thamani isiyo na mipaka. Liturujia ya Vipindi ndiyo sala kuu ya Bibi arusi wa Kristo, ambayo haitakiwi kukoma duniani, kama vile misa isivyokoma kamwe. Kwa waliojaliwa heshima ya kuishiriki, inatarajiwa kuwa shule nzuri ajabu ya sala hasa, ya kujitoa na ya utakatifu. Lakini ikipotewa na roho yake na kubaki na mwili tu, isizame katika mafumbo, badala ya kuwa mruko, mwinuko na pumziko la mtu kwa Mungu, inakuwa mzigo na uchoshi usiozaa tena matunda yake bora.

Haraka ndiyo kifo cha ibada, kwa kuwa inaizuia isiwe na undani. Hapo maneno yanatamkwa vibaya, pasipo mdundo wala kipimo. Antifona na tenzi hazieleweki, ingawa mara nyingi ni nzuri kama nini. Masomo yanafanyika pasipo kuzingatia vituo, kama mambo yasiyo na maana, kumbe ndiyo mng’ao wa hekima ya Mungu. Kwa kisingizio cha kuokoa muda (labda dakika tano zitakazotumika kwa upuuzi) unapotezwa muda ulio bora, ule uliotolewa kwa Mungu. “Kama tajiri angesema na mtumishi wake vile wengi wanavyosema na Mungu wakisali Liturujia ya Vipindi, mtumishi angedhani tajiri amerukwa na akili kwa jinsi anavyoropoka” (Ch. wa Condren). Liturujia iliyolipuliwa inafanana na mashine: sehemu zake zimepangwa moja karibu na nyingine pasipo kufungamanishwa na uhai. Maneno yanafuatana tu, bila kutokeza maana yake ya Kimungu, hivi kwamba anayetaka kuielewa na kuifuata analazimika kujichosha kwa kuwa anazuiwa badala ya kusaidiwa kusali.

Pengine zinakumbushwa taratibu za liturujia, lakini hizo peke yake hazitoshi. Ugonjwa ni wa ndani zaidi, hivi kwamba ni lazima tung’oe mizizi yake. Dawa ya kufaa kweli, inayowezesha kufaidika na nyingine pia, ni roho ya sala, kama vile roho inavyohitajika kumrudishia uhai maiti. Kwa mtu asiyesali peke yake pia, Sala ya Kanisa ni kazi ya mwili, ibada ya nje tu. Kwa kukosa mazoea ya kujikusanya, anashambuliwa na mawazo yasiyohusika na liturujia: kazi, masomo, shughuli na pengine upuuzi tu. Hata wanasala wanapatwa nayo, lakini kwake ni hali ya kawaida ya uzembe, na ndani yake mtawanyo wa mawazo haubaki katika ubunifu bali unaenea katika akili na utashi. Katika hali hiyo atawezaje kufurahia maneno ya Mungu, maandishi bora ya mababu wa Kanisa na maisha ya watakatifu tunayoyapitia kila siku? Hauzingatii uzuri huo wote, kwake ni kama vitu visivyo na rangi wala ladha. Ubora wa ushairi wa Mtungazaburi na milio ya moyo wake vinaonekana vya kawaida na vya kukinaisha. [1]

Kinachofanya liturujia iwe ya kuzama ndani yake ndicho roho ya sala, au walau hamu ya kuwa nayo ambayo inaitafuta na hatimaye itaipata. Kuzama katika mafumbo ndiyo njia pekee ya kuona katika liturujia mwanga, amani, furaha ya ukweli. Hiyo roho ya sala inachotwa hasa katika sala ya moyo na inapotea tukiwa na haraka ya kumaliza sala kana kwamba isingekuwa pumzi ya roho, fungamano na Mungu na uhai wetu. Ndiyo roho ambayo ilizaa Zaburi na inahitajika ili kuzielewa na kuzishika maishani: “Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji, vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu” (Zab 42:1). Liturujia ikiwa na roho hiyo ni hai, haihitaji kukumbushwa mfululizo taratibu zake, kwa sababu hizo zinalingana na maelekeo yetu ya ndani. Hapo, bila kwenda polepole mno, maneno yanatamkwa vizuri, vituo vinazingatiwa, antifona zinafurahiwa, na tunajilisha kweli ujumbe wa matini. Msomaji anajiandaa mapema asije akasoma kwa shida na namna isiyoeleweka; katika matamshi anakwepa kujitokeza mno binafsi. Kisha kusali Zaburi tunajisikia kuirefusha kwa kitambo cha sala ya moyo, kama walivyofanya watawa wa zamani ambao mara nyingi walipata hapo mianga mikuu walioitafuta kwanza kwa saa na saa za juhudi. Hapo tunaelewa kuwa sala ya moyo ndiyo roho ya Sala ya Kanisa, ambayo upande wake ndiyo lishe bora ya sala ya moyo, kwa kuwa ndiyo Neno la Mungu lililopangwa na kufafanuliwa kadiri ya mzunguko wa mwaka wa liturujia, yaani kadiri ya wakati halisi unaolingana na uzima wa milele.

Hapo kweli sala ni kuzidi kumuinulia Mungu roho ambayo inawaka na kumalizika kitakatifu kama mshumaa altareni. Kwetu ni heri kushiriki Sala ya Kanisa ikiadhimishwa hivyo: hapo tunahisi uhai halisi wa Kanisa, tunatambua wimbo wake mnyofu na papo hapo wa fahari ambao unatangulia na kufuata maneno bora ya Bwana arusi, yale ya mageuzo katika ekaristi. Hapo tunasahau huzuni za duniani na masharti ya kinafiki ya maisha ya jamii. Sala ya namna hiyo inavuta miito mizuri, wakati liturujia iliyolipuliwa inaisogeza mbali. Mungu atujalie idumu usiku na mchana katika nyumba za kitawa, kwa sababu sala hai haitakiwi kukoma, na sala ya usiku ina neema za pekee kwa kuzama katika mafumbo, kutokana na kimya kikuu kilichopo na kwa sababu nyingine nyingi. Sala hiyo ndiyo pumziko takatifu ambalo watu wanalihitaji baada ya kupatwa na uchovu, mahangaiko na fujo ulimwenguni. Ni pumziko ndani ya Mungu lililojaa uhai na linalofanana kidogo na pumziko lake ambaye anao kwa mara moja uhai wote usio na mwisho katika nukta ile isiyopita kamwe na iliyo kipimo cha utendaji mkuu na cha utulivu mkuu katika upendo.

Sala ya Kanisa ambayo inaandaa na kutimiliza misa ni njia kuu ya kuinuka juu ya mawazo ya kibinadamu hadi kuzamia mafumbo na kuungana na Mungu. Hata mtu anayesoma kirefu teolojia anahitaji kuinuka juu kuliko ujuzi wa vitabu, kukusanya mawazo mpaka ndani, kupokea nuru ya Mungu katika sala. La sivyo anadumaa, hawezi kuwashirikisha watu nuru ya kutosha, kazi yake haina uhai, mawazo yake hayapandi juu inavyotakiwa yaone mandhari yote, na polepole yanaacha kuvutia. Ni lazima aone mara nyingi mafumbo anayoyasoma yanavyojitokeza kwa namna hai na angavu katika maneno ya Mungu ambayo liturujia inatufanya tuyaonje na kuyapenda. Neno lake tunalokumbushwa hivyo katika sala linahusiana na vitabu vya teolojia kama vile duara nyofu inavyohusiana na umbo la pembe nyingi lililomo ndani mwake. Pengine ni lazima kusahau pembe zote za umbo hilo na kufurahia kitakatifu uzuri wa duara tu.

Hatimaye Sala ya Kanisa ni kanuni ya hakika dhidi ya udanganyifu wa binafsi: inatuponya mapendo ya juujuu kwa kutukumbusha mfululizo kweli kuu kwa lugha ya Maandiko. Wanaojiamini kipumbavu inawakumbusha ukuu wa haki ya Mungu, kumbe wanaomuogopa mno inawakumbusha huruma isiyo na mipaka na thamani ya mateso ya Mwokozi. Inawainua wanaofuata miguso na hisi tu hadi vilele vya imani na upendo halisi. Inatukumbusha hatua zote za maisha ya Kiroho, zikiwa ni pamoja na mafumbo ya furaha, mwanga, uchungu na utukufu ya Rozari. Hivyo inatupatia furaha halisi ambayo inapanua moyo na kutuandaa kwa sala ya kimya zaidi, yaani sala ya moyo.

  1. Siku fulani, wakati wa kuimba Zaburi kwa pamoja, Bernardo aliona juu ya kila mtawa malaika mlinzi akiandika maneno yake, lakini kwa namna tofauti: kwa herufi ya dhahabu, ya fedha, ya wino au ya maji tu; tena mwingine alishika peni asiandike.
  • Тvпико́нъ сіесть уста́въ (Title here transliterated into Russian; actually in Church Slavonic) (The Typicon which is the Order), Москва (Moscow, Russian Empire): Синодальная типография (The Synodal Printing House), 1907, uk. 1154
  • The Unabbreviated Horologion, Jordanville, New York: Holy Trinity Monastery (ilichapishwa mnamo 1997), 1992
  • On-line text (in Church Slavonic Часослов – Chasoslov, Horologion, Retrieved 2011-12-31
  • Saint Symeon of Thessaloniki (c. 1420), Treatise on Prayer: An Explanation of the Services Conducted in the Orthodox Church, Translated by Harry L.N. Simmons, Brookline, Massachusetts: Hellenic College and Holy Cross Greek Orthodox School of Theology Press (ilichapishwa mnamo 1984), ku. 132–136, ISBN 0-917653-05-X
  • Sokolof, Archpriest Dimitrii (1899), Manual of the Orthodox Church's Divine Services, Jordanville, New York: Holy Trinity Monastery (ilichapishwa mnamo 2001), ku. 132–136, ISBN 0-88465-067-7
  • Archpriest Alexander Schmemann (1963), Introduction to Liturgical Theology (Lib. of Orthodox Theol.), Faith Press Ltd (ilichapishwa mnamo 1987), uk. 170, ISBN 978-0-7164-0293-0
  • Ware, Timothy (1963), The Orthodox Church, London, UK: Penguin Books (ilichapishwa mnamo 1987), uk. 193, ISBN 978-0-14-013529-9
  • Archimandrite Robert F. Taft, S.J. (1986), The Liturgy of the Hours in East and West: The Origins of the Divine Office and Its Meaning for Today, Collegeville, Minnesosta: The order of Saint Benedict, Inc., uk. 423, ISBN 978-0-8146-1405-1, JSTOR 1291596
  • Archimandrite Robert F. Taft, S.J. (1988), "Mount Athos: A Late Chapter in the History of the Byzantine Rite", Dumbarton Oaks Papers, 42: 179–194, JSTOR 1291596

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Madhehebu ya Kiroma
Madhehebu ya Kigiriki
Waorthodoksi wa Mashariki
Anglikana
Waprotestanti wengine
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy