Nenda kwa yaliyomo

Mtawa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Utawa)
Watawa
Watawa wa kike wa dini mbalimbali katika sehemu tofauti za dunia.

Mtawa ni mtu anayejitenga na ulimwengu ili kuishi maisha maadilifu.

Katika dini mbalimbali, mfano mmojawapo wa utawa ni ule wa wamonaki. Lakini katika Ukristo, hasa wa Magharibi historia ya Utawa ilitokeza aina nyingine mbalimbali.

Watawa wa Kanisa Katoliki

[hariri | hariri chanzo]

Katika Kanisa Katoliki, mtawa ni mwamini yeyote aliyejiweka wakfu kwa Mungu hasa kwa kushika useja mtakatifu, lakini kwa kawaida pia ufukara na utiifu.

Mara nyingi watawa wanaunda mashirika yenye karama moja inayofafanuliwa na kuratibiwa katika kanuni na katiba maalumu.

Mtawa anaweza kuwa mwanamume au mwanamke, mwenye daraja takatifu au la.

Wakristo wote wanavyopaswa kulenga ukamilifu kutokana na amri kuu ya upendo, lakini mtawa ana wajibu wa pekee wa kufanya hivyo kwa kuwa adili la ibada linahitaji kuhuishwa na upendo kwa Mungu ulio safi na wa nguvu zaidi na zaidi.

Msingi wa wajibu huo ni nadhiri za kitawa, ambazo neema zake si za muda, bali za kudumu mtu akizidi kuwa mwaminifu. “Wengine wako katika hali ya ukamilifu, si kwa sababu ya kufanya tendo la upendo kamili, bali kwa kujifunga moja kwa moja, kwa fahari fulani, washike kile kinachoelekeza kwenye ukamilifu… Kwa kuwa watawa wanajifunga kwa nadhiri kujinyima malimwengu ambayo wangeruhusiwa kuyatumia kwa hiari; wanafanya hivyo ili kushughulikia mambo ya Mungu kwa urahisi zaidi… Vilevile maaskofu wanajifunga kushika ukamilifu wanapokubali daraja ya uaskofu, kwa sababu mchungaji anapaswa kutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake” (Thoma wa Akwino).

Mtawa anatamka atalenga ukamilifu: “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo, kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu” (Fil 3:12). Hatendi kosa la unafiki kama hajawa mkamilifu, ila analifanya asipolenga ukamilifu kwa unyofu. Kwake wajibu huo wa pekee na ule wa kushika nadhiri zake na kanuni aliyoahidi ni mamoja. Lakini wajibu huo uzingatiwe daima kuhusiana na ule wa jumla unaotokana na amri kuu ya upendo; hapo utawa hautatazamwa upande wa sheria tu, bali utaonekana katika upana wa maana yake ya Kiroho.

Kwa mtazamo huo tu utaeleweka kweli neno zito la Thoma wa Akwino: “Kufanya tendo kwa nadhiri kunastahili kuliko kulifanya bila nadhiri”. Si kwamba tuzidishe nadhiri ili kustahili zaidi, bali mtawa atekeleze nadhiri zake vizuri zaidi na zaidi, akizidi kuchimba sababu tatu alizozitoa mtakatifu huyo katika ufafanuzi wake:

  1. Nadhiri ni tendo la adili la ibada, ambalo ni bora kuliko yale ya utiifu, ufukara na usafi wa moyo ambayo linamtolea Mungu yawe ibada.
  2. Kwa nadhiri ya daima mtu anamtolea Mungu si tendo mojamoja, bali uwezo wenyewe wa kutenda, na kwa hakika ni afadhali kutoa mti na matunda yake kuliko kutoa matunda tu.
  3. Kwa nadhiri utashi unaimarishwa katika kutenda mema, na kwa hakika kutenda kwa msimamo kunastahili zaidi, kama vile ni vibaya zaidi kutenda dhambi kwa utashi ulioshupalia uovu.

Mtu akiishi kwa roho hiyo ataelewa kwa namna hai fundisho la kwamba, kwa kujifunga kushika mashauri matatu, yaliyo kiini cha utawa, mtu anajitenga na yale yanayoweza yakazuia mapendo yake yasimuelekee Mungu tu, halafu asipofuta uamuzi huo anajitoa kwake kama sadaka ya kuteketezwa. Hivyo hali yake ni ya kujitenga na ulimwengu na ya kuwekwa wakfu kwa Mungu.

Hasa mambo matatu yanaweza kuzuia mapendo yake yasimuelekee Mungu: tamaa za macho (yaani za vitu vinavyoonekana), tamaa za mwili na kiburi cha maisha (yaani kupenda awe huru tu). Mtawa anayakataa hayo matatu kwa nadhiri zake, akimtolea Mungu mali kwa ufukara, mwili na moyo kwa useja mtakatifu na matakwa yake kwa utiifu. Asipojitwalia tena chochote, bali akitekeleza vizuri, kwa upendo mkubwa zaidi na zaidi, maadili matatu yanayohusiana na nadhiri za kitawa, basi anamtolea kweli Mungu sadaka ile kamili inayostahili kuitwa ya kuteketezwa. Hapo maisha yake yanatolewa kila siku pamoja na sadaka ya misa kwa adili la ibada. Ni hivyo hasa kama mtawa anarudia mara nyingi ahadi zake kwa namna inayostahili kuliko alipozitoa kwa mara ya kwanza. Stahili zinakua ndani mwake pamoja na upendo na maadili mengine, hivyo hali yake ya kuwekwa wakfu kwa Mungu inazidi kuwa ya dhati na kamili.

Lengo la kujinyima pande tatu na kujitoa pande tatu ni kuungana na Mungu kila siku zaidi, kama utangulizi wa uzima wa milele. Mtawa anaitwa kuufikia muungano huo kwa kumuiga Yesu aliye “njia, na kweli, na uzima” (Yoh 14:6). Yeye, katika ubinadamu wake, alitenganika na roho ya ulimwengu akaunganika na Mungu vizuri iwezekanavyo. Mtawa anatamka hadharani nia ya kumfuata, lakini Yesu alitoka juu, kumbe mtawa ametoka duniani, palipotawaliwa na dhambi, hivyo anapaswa kujitenga zaidi na zaidi na mambo yote ya dunia, kadiri ya maneno haya: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu” (Kol 3:1-4). Thoma wa Akwino alifafanua hivi, “Msionje malimwengu kwa kuwa mmefia ulimwengu; uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo; mwenyewe amefichika kwetu, kwa kuwa yuko katika utukufu wa Mungu Baba yake, na hivyo uhai… tulionao kutoka kwake umefichika, kadiri ya maneno ya Maandiko matakatifu, ‘Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako ulizowawekea wakuchao; ulizowatendea wakukimbiliao mbele ya wanadamu!’ (Zab 31:19). ‘Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa’ (Ufu 2:17)”. Hiyo mana ya Kiroho, ambayo ile ya jangwani ilikuwa mfano wake tu, ndiyo chakula cha roho: kujaliwa kuzama katika mafumbo ya imani. Hivyo utekelezaji wa maadili unaandaa kumiminiwa sala; kwa namna ya pekee “ubikira unalenga ustawi wa roho katika maisha ya kuzamia sala” (Thoma wa Akwino). Hivyo tena maisha ya kitawa yanalenga zaidi na zaidi utekelezaji kamili wa amri ya upendo na undani wa muungano na Mungu.

Wajibu wa pekee alionao mtawa wa kulenga ukamilifu uzingatiwe daima kuhusiana na wajibu wa waamini wote unaotegemea amri kuu ya upendo. Amri hiyo inatawala mashauri ya Kiinjili, kwa kuwa hayo ni njia na vyombo tu kwa ajili ya kufikia ukamilifu wa upendo kwa kasi na hakika zaidi. Hivyo, maadili matatu ya kitawa yanatekelezwa kikamilifu kwa maadili matatu ya Kimungu. Kati ya hayo yote kuna fungamano la dhati, hivi kwamba tumaini la heri ni kama uhai wa ufukara mtakatifu ambao unaachana na mali ya dunia na kutufanya tuzidi kumtumainia Mungu ili kupata ya milele; upendo ndio uhai wa useja unaojinyima mapendo ya chini ili kupata upendo wa juu kabisa: unapotekelezwa sawasawa unastawisha ndani mwetu upendo kwa Bwana na kwa watu; imani ndiyo uhai wa utiifu unaotekeleza maagizo ya wakubwa kana kwamba yamefunuliwa na Mungu: utekelezaji huo unakuza roho ya imani. Hivyo maisha ya kitawa yanafikisha kwenye sala ya kumiminiwa na muungano wa dhati na Mungu unaozidi kustawisha ule na jirani.

Adili la ibada linadhihirika kuwa la kishujaa mtu anapotimiza wajibu alionao upande huo bila kujali upinzani mkali wa ndugu wa ukoo na wengineo. Linadhihirika vilevile katika utekelezaji wa nadhiri ya kutenda yaliyo bora, na katika uanzilishi wa familia ya kitawa kati ya matatizo makubwa ambayo kwa kawaida yanaendana nao.

Ufukara wa kishujaa unajinyima vyote, ukiridhika na riziki za lazima tu, ili kufanana na Bwana ambaye hakuwa na mahali pa kupumzikia. Asiyetamani chochote hakosi kitu, ni tajiri Kiroho na mwenye heri. Usafi wa moyo wa kishujaa unadhihirika hasa katika ubikira wa kudumu, mtu anapoishi mwilini maisha ya Kiroho tu hata akasahau vurugu zote za hisi kwa kuzoea kuzishinda. Hatimaye utiifu wa kishujaa unadhihirika katika kujikatalia kikamilifu matakwa ya binafsi, mtu asipofanya chochote bila ruhusa ya wakubwa, akiwatii wote bila kujali walivyo, hata wasipomuonyesha wema. Pengine anadaiwa kutii maagizo magumu, kama vile Abrahamu alivyodaiwa sadaka ya mwanae pekee. Hapo anahitaji imani kubwa ambayo imuonyeshe Mungu ndani ya wakili wake. Ni nafasi ya giza ambayo ikivukwa vizuri inaleta mwanga mkubwa, kwa kuwa Bwana anamlipa kwa ukarimu yule anayetii hivyo.

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy